Bei ya muhogo sokoni yaamsha ari ya wakulima wa Handeni

Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (Mari), Dk Joseph Ndunguru (anaye andika) akikagua shamba la muhogo la Shule ya Sekondari Komnyang’ wilayani Handeni mkoani Tanga, ikiwa ni mpango wa kujua ni magonjwa gani yana athiri zaidi zao hilo.Picha na Rajabu Athumani

Muktasari:

  • Miongoni mwa mazoa hayo ni pamoja na mbaazi, alizeti,korosho na hata ufuta.
  • Kwa mujibu wa wakaazi wilayani humo, hivi sasa wameamua kujikita katika kilimo cha muhogo na kampeni hiyo inaongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe.

Wilaya ya Handeni ni moja ya zilizojaliwa kuwa na ardhi yenye rutuba na inayostawisha mazao ya aina mbalimbali ya chakula na biashara.

Miongoni mwa mazoa hayo ni pamoja na mbaazi, alizeti,korosho na hata ufuta.

Kwa mujibu wa wakaazi wilayani humo, hivi sasa wameamua kujikita katika kilimo cha muhogo na kampeni hiyo inaongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Godwin Gondwe.

Zao la muhogo linaonekana mkombozi kwa wakazi wa Handeni hasa wale walioamua kujikita kwenye kilimo hicho, hususan wale wanaoishi maeneo ya Kwamsisi, Kabuku, Kwamgwe, Mazingara, Kwaludege, Mkata na sehemu za jirani.

Kwanini Muhogo na siyo mazao mengine

Akizungumzia sababu ya kuibua kilimo cha muhogo katika Wilaya ya Handeni, Mkuu wa Wilaya Gondwe anasema wananchi wengi wilayani humo walikuwa wanategemea zao la mahindi kama zao kuu la biashara na chakula, hali iliyokuwa ikisababisha ikumbwe mara kwa mara na upungufu wa chakula.

Anasema mafanikio ya kilimo cha mahindi mara zote hutegemeana na hali ya hewa, kwani asilimia kubwa hulima kipindi cha mvua na zikiwa chache, hushindwa kuvuna mazao ya kutosha. “Lakini kitu kingine ni kwa wakulima kuamua kuuza mahindi tangu yakiwa machanga hadi kukomaa na hujikuta wameyamaliza shambani hawana cha kuvuna na kujikuta wakikosa chakula,” anasema Gondwe.

Makuu huyo wa wilaya anasema baada ya kulitafakari hilo kwa kina, akaamua kubuni zao mbadala la biashara ambalo litawasaidia kulifanya la biashara na la chakula ambalo ni muhogo.

“Niwashukuru shirika la World Vision na wabunge wa Handeni wa Handeni Mjini, Omari Kigoda na wa Handeni Vijijini, Mboni Mhita waliosaidia kufanikisha mkakati huu, shule zetu karibu zote zilipata mbegu zikapanda, asilimia kubwa zimeota na vijana wamepata chakula cha shule cha kutosha,” anasema Gondwe.

Anasema wabunge hao wamechangia Sh19 milioni na Shirika la World Vision limetoa Sh60 milioni kwa ajili ya kununulia mbegu za muhogo zilizosambazwa kwenye taasisi mbalimbali zilizoko wilayani Handeni.

Kwanini fedha zilichangishwa

Mratibu wa Shirika la World Vision Tarafa ya Kwamsisi, Jackline Kaihula alisema baada ya Mkuu wa wilaya kuwashirikisha kuhusiana na mpango wa kutafuta zao mbadala la biashara, waliliafiki na kuamua kutafuta njia ya kupata fedha za kununulia mbege.

Anasema shirika liliafiki na kuamua kutoa fedha hizo ambazo mbali ya kununua mbegu, pia zilitumika kugharamia usafirishaji wa mbegu kwenye maeneo mbalimbali wilayani humo. “Tulipoyatembelea maeneo zilikosambazwa mbegu hizo, tulishuhudia zimepandwa na mazao yamestawi na kuleta mafanikio,” anasema mratibu huyo wa World Vision.

Hata hivyo, anasema bado wanalo jukumu la kusimamia masuala ya maendeleo hasa katika nyanja ya kilimo ambacho kinategemewa kutoa mazaoya chakula na ya biashara kwa wananchi wilayani humo.

“Ni wajibu wetu kusaidia upatikanaji wa chakula cha wanafunzi wilayani hapa kama sera yetu inavyotuelekeza,” anasema Kaihula.

Wakulima wanalizungumziaje zao hilo jipya

Asilimia kubwa ya wakulima waliokubali kulima muhogo kwenye msimu uliopita, wamekiri kunufaika kwa kuuza kwa bei ya faida.

Adamu Mkono mkulima wa Kata ya Kwamsisi aansema alilima eka mbili na nusu za muhogo kwa awamu ya kwanza msimu uliopita zilizomuingizia Sh2.15 milioni kabla ya wateja kuongezeka katika awamu ya pili nay a tatu. “Sikutarajia kupata fedha nyingi kiasi hiki, tulizoea kuuza mahindi ambayo faida yake ni ndogo sana. Gunia moja tunaliuza kwa Sh60,000, lakini siyo kwa muhoga, unafaida kubwa sana,” anasema mkulima huyo.

Mkono anatoa wito kwa Serikali iangalie utaratibu wa kuwakopesha matrekta ya kulimia ili walime mashamba makubwa kwakuwa wanauhakika wa kulipa baada ya mavuno. “Kama eka mbili na nusu nimepata Sh2 milioni, nikilima zaidi ya eka hizo nitakuwa na faida zaidi, sitashindwa kulipa mkopo wa laki mbili wa kulimiwa na trekta, serikali itusaidie kupata mikopo ya kulimiwa tutalipa,” alisema Mkono.

Anasema licha ya soko kuonekana halina shida, ni vema kama watajengewa kiwanda cha kusindika zao hilo kwenye moja ya eneo linalozalisha muhogo ili wakulima wawe na uhakika wa soko kuliko ilivyo sasa.

Anasema hivi sasa kuna walanguzi wameanza kuvamia soko la zao hilo.

Ufumbuzi wa soko la uhakika

Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni (Mari), kimewatoa hofu wananchi wanaolima muhogo kuhusu wapi soko litapatikana sambamba na upatikanaji wa mbegu bora za zao hilo kwa kuahidi uwapo wa soko mbegu bora.

Mkuu wa Kituo hicho, Dokta Joseph Ndunguru, alifika Handeni kwa mwaliko wa Mkuu wa Wilaya, Gondwe na kutembelea mashamba kadhaa kuona mwamko wa wananchi na kuridhika nao.

Anasema wameshaandaa mpango kazi na viongozi wa baadhi ya halmashauri za Mkoa wa Tanga ikiwamo ya Handeni kuhakikisha wanadhibiti magonjwa yanayoharibu mihogo.

Anasema wamebaini muhogo unalimwa moani Tanga inaathiriwa na ugonjwa wa batobato, hivyo taasisi yake itapeleka mbegu ambayo haiwezi kupata ugonjwa huo na wakulima watakuwa na uhakika wa kuvuna muhogo wa kutosha kwa chakula na biashara. Akizungumzia soko, Dk Ndunguru anasema tayari China imeshatangaza nia ya kufanya biashara ya muhogo na Tanzania.

“Wakulima wanatakiwa kulima kwa wingi cha msingi ni kuzingatia ubora, soko halina shida,” anasema Dk Ndunguru.

Wilayani Handeni mwamko wa wananchi kulima Muhogo ni mkubwa baada ya kuona wenzao wanapata faida kubwa.

Zao hilo sasa litalinusuru zao la mahindi ambalo familia nyingi sasa litalitumia kuwa la chakula zaidi tofauti na awali.