Thursday, November 9, 2017

Benki ya NMB, I&M zajipanga kuwateka wanachama wa Vicoba

By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya kuona fursa kubwa iliyopo, Benki ya NMB imeandaa mpango wa kuwapa fursa kubwa zaidi wanachama wa Vicoba kufanikisha miradi yao ya kijasiriamali.

Licha ya kutokuwepo kwa kanzidata rasmi, inakadiriwa vikundi hivyo vina zaidi ya wanachama milioni mbili ambao ni wanachama wa Vicoba zaidi ya 100,000 ambavyo mtaji wake ukikadiriwa kuwa zaidi ya Sh1.2 trilioni.

Mkurugenzi mtendaji wa benki ya NMB, Ineke Bussemaker anasema kundi hilo ni wateja muhimu ambalo likipewa nafasi inayotakiwa kwenye taasisi za fedha litakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi.

“Hawa ni wateja muhimu na kwa kutambua hivyo mwakani tutatarajia kuanzisha huduma maalumu kwa ajili yao. Watu walipo kwenye Vicoba watakuwa na upendeleo maalumu kwani dhamana yao ni shughuli wanazofanya,”  alisema Ineke.

Vilevile, alisema utaratibu mwingine utaandaliwa kwa ajili ya kuwahamasisha wajasiriamali hawa kuwa na akaunti za benki kwa kuondoa makato ya kila mwezi na kila atakayepitishia mkopo wake kwenye akaunti hiyo hatokatwa gharama za kufanya hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya I&M,  Mohammed Baseer alisema ingawa benki yake haina matawi mengi mikoani, wanaitambua fursa hiyo na wanajitahidi kuifikia kwa kuwahamasisha wajasiriamali wadogo.

“Bado haijafika sana mikoani lakini tunayo huduma ya mtandao inayowasaidia wajasiriamali wadogo kupata mikopo. Lakini, tunajipanga kuwafikia wengi zaidi kwa njia zote,” alisema Basser.

Mipango hii ya taasisi za fedha inabainishwa baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa wito kwa benki za biashara kuwapa kipaumbele wajasiriamali wadogo kupitia vikundi vyao. Alisema hayo kwenye maadhimisho ya siku ya Vicoba.

-->