Betrida msichana aliyekonga nyoyo za wana-Hisabati

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kilakala, Betrida Muganda,akizungumza na wadau wa Hisabati, baada ya kuibuka mshindi wa mashindano ya somo hilo. Mashindano hayo yaliandaliwa na Chama cha Hisabati Tanzania. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Mbele ya umati wa wataalamu wa hesabu nchini, mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Kilakala, mkoani Morogoro Betrida Muganda, alipewa dakika 10 kuelezea siri ya kufanya vizuri katika somo la Hisabati.

Kila aliyekuwamo ndani ya ukumbi wa mikutano wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alitulia tuli kumsikiliza.

Mbele ya umati wa wataalamu wa hesabu nchini, mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya Sekondari ya Kilakala, mkoani Morogoro Betrida Muganda, alipewa dakika 10 kuelezea siri ya kufanya vizuri katika somo la Hisabati.

Huyu ndiye mwanafunzi aliyeibuka kinara katika mashindano ya Hisabati yaliyoendeshwa na Chama cha Hisabati nchini (Mat/Chahita) mwaka 2016, akiwashinda wenzake zaidi ya 200 kutoka shule mbalimbali nchini.

Kwake, siri ni hii: ‘’… siri ya kujua ni kuzipenda tu na si vinginevyo.’’

Wakati Betrida akisifia urahisi wa Hisabati,wapo wanafunzi wengi wanaolikimbia somo hilo kwa madai kuwa ni gumu na hawalimudu.

Uhaba wa walimu, mazingira yasiyo rafiki kutokuwapo kwa walimu wa kutosha, ukali kwa baadhi ya walimu, vinaelezwa kuwa visababishi vya wanafunzi kukosa hamasa ya kujifunza hesabu..

Katika mkutano huo wa walimu wa Hisabati, kinara huyu alipewa zawadi, akiaswa kutumia uzoefu wake kuhamasisha wenzake kutolikimbia.

Betrida anasema hajawahi kufeli hesabu. Alifaulu kwa kupata alama A darasa la saba na kidato cha nne. Anatarajia kupata alama hiyo hiyo atakapohitimu kidato cha sita.

Hamasa ya kujifunza hesabu

Mwanafunzi huyo anayesoma mchepuo wa Fizikia, Kemia na Hisabati (PCM) anasema tangu utotoni alipenda kujifunza hesabu.

“Tangu chekechea nilikuwa nafanya hesabu, ilifikia hatua mgeni yeyote anayeingia nyumbani kututembelea ili nimwamkie, nilimwambie anipe swali la hesabu,”anasema.

Anasema mapenzi ya dhati kwa somo hilo yalisababisha alione rahisi kuliko masomo mengine. Kilichomvutia zaidi kwenye anasema ni hamasa kutoka kwa baba yake mzazi Adson Mganda.

“Baba yangu alikuwa mwalimu wa hesabu na mdau mkubwa wa somo hilo, hivyo yeye ndio sababu kubwa ya kuona somo hili rahisi,”anasema.

Betrida anasema kilichokuwa kikimfurahisha kutoka kwa baba yake ni namna alivyokuwa akijitoa kumfundisha hata wakati akiwa na uchovu wa kazi.

“Kuna siku unaona kabisa baba amechoka na kazi, lakini akifika nyumbani ananifundisha bila wasiwasi tena kwa mapenzi makubwa.

Anatoa maswali, nafanya na anasahihisha,”anasema na kuongeza kuwa misingi miziri ya maendeleo ya mtoto shuleni huanza kwa mzazi.

“Unakuta mzazi mwingine hapendi Hisabati kwa hiyo anawafanya wengine pia wasizipende. Ni vizuri wazazi wawe chachu ya watoto kupenda hili somo, wakiwajengea mazingira mazuri watawasaidia,” anaeleza.

Anasema siri nyingine ya ufaulu wake ni mazoezi ya kila siku. Kila asubuhi, msichana huyo huamka na kufanya maswali si chini ya 25 kabla ya kuanza kazi nyingine yoyote.

“Mtihani kawaida ni saa tatu kwa hiyo, kila siku nilijiwekea ratiba ya kutumia muda mfupi kufanya maswali kuanzia 25 hadi 5o,”anasema.

Anasema mazoezi ya kila siku huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufaulu wa somo hilo.

Mwanafunzi huyo anasema upo uhusiano mkubwa baina ya hesabu na masomo mengine.

“Mara nyingi watu wanaofaulu hesabu hawawezi kufeli masomo mengine. Somo hili linaingia kotekote,”anasema.

Ratiba yake ya kila siku

Kuishi kwenye ratiba ni siri nyingine ya mafanikio kwenye masomo yake darasani. Anasema kila siku huamka saa 10.30 asubuhi.

“Muda huo najiandaa na ikifka saa 11.30 naingia darasani kusoma. Nakaa hapo hadi saa 1.00 kisha naungana na wenzangu kufanya usafi wa kawaida wa asubuhi,”anaelezea.

Utaratibu mkubwa aliojiwekea ni kuhakikisha kuwa hakosi kufanya maswali ya hesabu hata kama ratiba ya siku hiyo itamwelekeza asome somo jingine.

Anasema darasa lao lina ratiba ya kujisomea na kujadili maswali magumu, ambalo huwa wanaanza saa 3.00 usiku hadi saa tano usiku. Huendelea tena kusoma peke yake kabla ya kulala ifikapo saa saba.

Ratiba hiyo ni ngumu lakini anasema lazima ahakikishe kila siku anaikamilisha ili aweze kutimiza ndoto zake.

“Ukiwa na malengo lazima ujue kujitosa tu vinginevyo hutofanikiwa. Natamani ndoto zangu za kuwa mhandisi au mhasibu siku moja zitimie ndio maana nasoma kwa bidii,”anaelezea.

Kaka yake, Adeck Muganda anayesoma masuala ya uhandisi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anajivunia namna ambavyo mdogo wake anafanya vizuri kwenye somo hilo.

“Japo namimi nilipata A, mdogo wangu anafanya vizuri zaidi na ikizingatiwa ndiye msichana pekee kwenye familia yetu; najivunia kuwa naye,”anasema.

Mwenyekiti wa Mat/Chahita Dk Said Sima anasema kuwa msichana huyo aliweza hesabu kwa sababu ya kuwa na misingi mizuri kutoka kwa wazazi na walimu wake tangu mwanzo

“Mfano ni nyie wataalamu wa hesabu, itakuwa aibu kama watoto wenu wakifeli. Wazazi ni chachu ya kwanza ya ufaulu kwa mwanawe,”anasema.