Wednesday, December 13, 2017

Biashara ya utumwa na dhambi ya Marekani, Libya

 

Tangu Machi 19, 2011, mataifa makubwa, Marekani, Ufaransa, Uingereza, Italia na mengineyo, wakitumia Jeshi la Kujihami la Nchi za Magharibi (Nato), walianza chokochoko kuifanya Libya iwe hivi ilivyo sasa.

Kabla ya hapo vikundi vya uasi vilikuwa vimeshaanza harakati za kumpindua aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi. Mataifa hayo kwa kuitumia Nato, walivifadhili na kuvipa ulinzi vikundi hivyo vya uasi dhidi ya Gaddafi.

Hata baada ya Gaddafi kukubali kuachia nchi watu hawakuridhika, walimuwinda na walipomkamata Oktoba 20, 2011 walimuua. Miaka sita tangu Gaddafi alipouawa, Marekani na nchi washirika wanaishuhudia Libya iliyogeuka soko la biashara ya utumwa.

Watu wanauliza biashara ya utumwa Libya ni kweli au siyo kweli? Jawabu ni kweli kabisa Libya kwa sasa ni soko la biashara ya watu. Mtu mmoja anapigwa mnada na kuuzwa kwa dola 200 (Sh448,500).

Novemba mwaka huu, kituo cha televisheni cha CNN, Marekani, kiliripoti habari ya watu wawili ambao inadhaniwa asili yao ni Nigeria, waliouzwa kwa dola 400 (Sh897,000). Habari hiyo ndiyo ambayo iliushitua ulimwengu.

Baada ya habari hiyo, Rais wa Marekani, Donald Trump aliitangaza CNN kuwa adui wa Wamarekani kwa sababu inaripoti habari zenye kuichafua nchi hiyo kwenye jumuiya za kimataifa.

Hata hivyo, huo ndiyo ukweli kwamba Libya baada ya Gaddafi imekuwa nchi ya vikundi vya waasi na jamii za makabila. Imeshindikana kuwa na Serikali moja ambayo inaweza kuratibu masuala ya nchi.

Kutokana na hali hiyo, sasa hivi Libya kikundi cha watu 50 wenye silaha kinaweza kuamua kuwa na utawala wake kwenye eneo fulani na ikawezekana. Na hiyo ndiyo sababu ya biashara ya utumwa kushamiri Libya, maana imekuwa nchi ya wenye silaha.

Asili ya biashara

Tangu kupinduliwa kwa Gaddafi na Libya kukosa Serikali yenye jeshi moja, watu wengi Kusini mwa Jangwa la Sahara walibaini uchochoro wa kwenda Ulaya kutafuta maisha bora kupitia Bahari ya Mediterranean.

Inakadiriwa kuwa mamia ya vijana wasio na vibali huingia Libya kila mwaka kutafuta njia ya panya kwenda Ulaya. Inakisiwa pia kuwa watu 150,000 wameshasafikiri kwenda Ulaya kwa njia ya boti kupitia Mediterranean ndani ya miaka mitatu iliyopita, huku watu 3,000 wamekuwa wakizama baharini kila mwaka ndani ya miaka minne iliyopita.

Kuanzia Aprili mwaka huu, askari wanaolinda pwani za Libya walipata msaada kutoka Italia kuhusu namna ya kuboresha ulinzi baharini na kudhibiti wahamiaji haramu na usafirishaji wa biashara yoyote haramu ikiwamo watu (human trafficking).

Kutokana na kuimarishwa kwa ulinzi, watu wengi walikamatwa baharini kwenye maboti wakisafirishwa kwenda Ulaya. Inakadiriwa watu 400,000 mpaka milioni moja wapo Libya ama baada ya kukamatwa baharini na kurudishwa nchi kavu au wakiwa wamekwama kusafiri kutokana na mazingira kuwa magumu kutokana na ulinzi wa Waitaliano.

Watu hao ambao wameshindwa kusafiri na kujazana Libya ndiyo ambao wanageuka watumwa. Wanauzwa kwenye mnada ili kutumika kwenye shughuli mbalimbali za uzalishaji mali, huku wanawake wakigeuzwa watumwa wa ngono.

Pamoja na kuuzwa kama watumwa, unyanyasaji unaofanywa dhidi ya watu ambao wamekosa nafasi ya kusafiri kwenda Ulaya ni mkubwa. Wanatumikishwa kufanya shughuli za aibu bila ridhaa yao, wanaume kwa wanawake wanabakwa na hata kuuawa.

Biashara inavyofanyika

Kwanza ni namna wahamiaji haramu wanavyogeuka watumwa. Zipo njia mbili za kufikia hatua ya kuuzwa. Ya kwanza ni hiari, maana mhusika anakuwa hana jinsi, pili ni kwa lazima, kwamba mtu anakamatwa na kuingizwa sokoni bila kupenda.

Wanaokubali kuuzwa kama watumwa kwa hiari ni wale ambao walifika Libya ili kusaka njia ya panya kwenda Ulaya. Baada ya kukuta mazingira magumu wamejikuta wakiuza kila kitu wakihangaika kujikimu kimaisha. Hivyo wanajiona hawana namna zaidi ya kukubali matokeo.

Wanaouzwa kwa lazima ni ambao wanatekwa na vikundi vya waasi na kuingizwa mnadani bila kupenda. Wote wanapouzwa, wale wenye kuridhia au wasioridhia, ambaye huchukua fedha ni yule aliyemfikisha muuzwaji kwenye mnada.

Kuna wafanyabiashara ya kusafirisha watu (people smugglers), nao wanapokutana na mazingira magumu ya kuwapitisha watu baharini kuwapeleka Ulaya, huwauza watu waliokuwa wanawasafirisha kama watumwa ili kufidia gharama walizotumia.

Wanaonunua watumwa ni wale ambao hawana uwezo wa kupata watu, kwa maana hawana nguvu ya silaha ya kuteka wahamamiaji haramu waliokosa uelekeo Libya, hivyo wanaamua kununua ili wawatumie kwenye shughuli zao mbalimbali.

Wauzaji wakuu wa watu ni wapiganaji wa vikundi vya uasi vilivyobaki na silaha baada Gaddafi kuangushwa, wameona kwao hiyo ni njia sahihi kupata fedha kwa kuteka wahamiaji hao haramu na kuwauza kwenye minada ya watumwa.

Wapiganaji hao wa vikundi vya uasi, wanapokuwa wameshawateka wahamiaji haramu, huwalazimisha watoe mawasiliano ya familia zao kisha huwapigia simu kuwataka watume fedha ili kuwakomboa watoto au ndugu zao, vinginevyo wanawaua.

Kutokana na hali hiyo, si tu kwamba watu wengi wanauzwa kama watumwa, bali pia vifo ni vingi. Watu wengi wanauawa kwa sababu ya familia zao kushindwa kutuma fedha au kufanya ukaidi mbele ya watekaji na kujaribu kutoroka.

Katika idadi ya mamia mpaka maelefu ya watu ambao hupoteza maisha, wapo hufikwa na mauti kutokana na kunyimwa au kukosa chakula wakiwa mateka, wengine hufa kwa kushindwa kuhimili mateso ya watekaji.

Aprili mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), lilikuwa la kwanza kuchapisha ripoti inayobainisha kuwa Waafrika (weusi) wengi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, wanauzwa kama watumwa baada ya kushikiliwa na wasafirishaji haramu wa binadamu au wapiganaji wenye silaha.

Libya imefikaje huko?

Miezi saba ya kumuondoa Gaddafi madarakani, Machi 19 mpaka Oktoba 20, 2011 ndiyo ambayo imeifikisha Libya ilipo sasa. Marekani na mataifa mengine makubwa washirika, walifadhili vikundi vingi vya uasi ili kufanikisha lengo.

Vikundi hivyo walivipa silaha na kuvilinda vilipokuwa vinachanja mbuga kushikilia miji mbalimbali mpaka vilipofika mji mkuu na makao makuu ya nchi, Tripoli. Nato ilikuwa imara kuyakabili majeshi ya Serikali, yalipotaka kuwakabili waasi.

Kutokana na hali hiyo, waasi waliua watu hususan walioonekana kuwa wafuasi wa Gaddafi. Majeshi ya Serikali yalipotaka kujibu yalikutana na Nato pamoja na mkwara wa Marekani, Ufaransa, Italia, Uingereza na nchi nyingine.

Baada ya Gaddafi kupinduliwa na kuuawa, ndipo dhambi iliyotendeka ya kugawia silaha vikundi vya uasi ilipodhihirika. Wito wa kuweka silaha chini na kuunda Serikali moja haujawahi kuitikiwa. Sababu ni moja tu, kwamba baada ya Gaddafi kupinduliwa nchi haikuwa na jeshi la kusimamia kile kinachotamkwa na waliokabidhiwa mamlaka na Serikali.

Vikundi vya wapiganaji wenye silaha viligoma kuweka silaha chini, matokeo yake nchi imekuwa “na majeshi mengi”, kila kikundi chenye silaha kilichohusika wakati wa vita ya kumpindua Gaddafi kinajiona ni jeshi kamili. Hiyo ndiyo sababu ya utulivu kukosekana Libya.

Oktoba 23, 2011 (siku mbili baada ya Gaddafi kuuawa), Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC) liliitangaza Libya kuwa imekombolewa. Kiongozi wa NTC, Mahmoud Jibril alisema mashauriano ya ujenzi mpya wa Libya yameanza. Baadaye Jibril alijiuzulu na NTC ilimchagua Abdurrahim el-Keib kuwa Waziri Mkuu wa Libya. Aprili 26, 2012 el-Keib aliondolewa madarakani na wajumbe wa NTC.

Julai 2012 uchaguzi ulifanyika kwenye maeneo machache, ikachaguliwa Serikali ya Baraza Kuu la Taifa la Congress (GNC) na Novemba mwaka huo, Ali Zeidan alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu. Machi 2014 GNC walimtoa Zeidan madarakani na kusabisha machafuko.

Agosti 4, 2014, uchaguzi mwingine ulifanyika na Baraza la Manaibu (CoD) ambalo hutambulika zaidi kama Baraza la Wawakilishi (HoR), lilichaguliwa kuunda Serikali, lakini GNC wakamtangaza Omar al-Hasi kuwa Waziri Mkuu.

Kutokana na mvutano huo, Libya ikawa na Serikali kuu mbili, moja ni ya GNC ambayo makao yake makuu yapo mji mkuu wa Tripoli na ile ya CoP au HoR inayoendesha Serikali ku