Bila kurahisisha biashara magendo yatakithiri

Muktasari:

Wakati huo nchi ilikuwa kwenye kipindi cha uaminifu na utiifu mkubwa juu ya nadharia ya ujamaa na kujitegemea.

Mwanzoni mwa miaka ya 1980, msamiati uliochukua nafasi ni ‘uhujumu uchumi’. Tanzania ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha maumivu ya kiuchumi baada ya kumaliza vita ya Kagera kwa kumwondosha aliyekuwa Rais wa Uganda, Iddi Amin Dada.

Wakati huo nchi ilikuwa kwenye kipindi cha uaminifu na utiifu mkubwa juu ya nadharia ya ujamaa na kujitegemea. Hivyo, Serikali ilikuwa ndiyo mfanyabiashara mkuu. Kutokana na athari za vita, uwezo wa Serikali kununua na kuuza bidhaa uliporomoka kwa kiasi kikubwa.

Matokeo ya jumla ya hali hiyo ni maduka ya Serikali kukosa bidhaa nyingi muhimu. Sabuni, dawa za meno, mafuta, nguo na kadhalika viliadimika. Mateso yalikuwa makubwa kwa wananchi. Watu wenye mitaji yao waliona hiyo ni fursa ya kuwafanya watengeneze fedha.

Kwa vile haikuwa rahisi, bidhaa nyingi ziliingizwa kwa njia ya magendo. Na kwa kawaida uagizaji na uuzaji batili wa bidhaa nje nchi kwa magendo, ndiyo huamsha kwa kiasi kikubwa ukuaji wa soko haramu na uchumi wa gizani.

Soko haramu au uchumi wa gizani ni maneno yenye tafsiri pana. Dawa za kulevya, biashara ya watu, utakatishaji wa fedha haramu ni sehemu ya mambo yenye kuujenga uchumi wa gizani. Hata hivyo, zipo bidhaa halali kwa matumizi hupitia soko haramu kwa sababu huuzwa na kununuliwa katika mifumo ambayo si halali.

Kwa muktadha huo, bidhaa zilizouzwa baada ya kuingizwa nchini kwa magendo nyakati za uhujumu uchumi, soko lake lilikuwa haramu, ingawa hazikuwa haramu kwa matumizi. Hoja hapo ni kuwa inapotokea mazingira ya kibiashara kuwa magumu, uchumi wa gizani hushika kasi.

Halali kama haramu

Bodaboda ni usafiri halali kwa abiria. Kwa Dar es Salaam ni mafurufuku bodaboda kuingia mijini, hasa Kariakoo na Posta. Anayekamatwa akikiuka katazo hilo hupigwa faini. Hata hivyo, madereva wa bodaboda hawakomi, maana wanaona fursa ya kutengeneza fedha na wanaichangamkia.

Kwa maana hiyo, kupanda bodaboda kwenda Posta au Kariakoo ni usafiri haramu. Madereva wa bodaboda wanapokuwa Posta na Kariakoo wakivizia abiria, kwa usahihi ni kwamba huwa wapo katika soko haramu. Mantiki ni kwamba bidhaa halali zinazouzwa katika njia zilizoharamishwa na mamlaka, hilo ni soko haramu.

Magendo na soko haramu huzaa uchumi wa gizani kwa sababu wafanyabiashara hutengeneza fedha ambazo huwa hazina baraka za Serikali, zaidi hakuna mapato ambayo Serikali hupata au kunufaika moja kwa moja.

Tatizo la mafuta

Tutazame kiini cha tatizo lililosemwa na Sirro. Ni kuhusu kuadimika kwa mafuta ya kula. Ikiwa anachokisema Sirro ni sahihi kwamba watu wameficha mafuta kwenye maghala yao ili kuyafanya yawe adimu, tunapaswa pia kutazama chanzo cha tatizo kwa vipimo vya kweli.

Mafuta ya kula yamekuwa adimu kwa sababu vyombo vya Serikali vinasigana. Taarifa iliyotolewa bungeni na Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage ni kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), haikubaliani na majibu ya kimaabara yaliyotolewa na Shirika la Viwango (TBS) pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Kwamba TBS na Mkemia Mkuu walitoa majibu kuwa mafuta yaliyopo bandarini ni ghafi, wakati TRA walisema si ghafi wala safi. Na kutokana na mkanganyiko huo, imeshindikana kuyashusha kwa wakati kwa sababu kuna mkanganyiko wa namna ya kutoza kodi. Maana viwango vya kodi hutofautiana kulingana na daraja la bidhaa.

Mvutano wa kimaabara kati ya idara hizo za Serikali ni sababu ya mafuta kuadimika mtaani na bei kupaa. Hivyo, si jambo geni wala halishindikani kwa wafanyabiashara kuficha mafuta ili kusababisha yawe adimu ama kama njia ya kuilazimisha Serikali iyaelekee matakwa yao au kuanza kuuza kupitia soko haramu.

Uzuri wa kauli ya Sirro ni kuonyesha namna ambavyo mamlaka za nchi zinavyotambua hali halisi kwamba kukiwa na mvutano wa kibiashara kati ya Serikali na wafanyabiashara, ambacho hutokea mara nyingi ni bei ya bidhaa yenye mgogoro kuadimika kisha kupanda bei.

Aprili 2016, uliibuka mgogoro wa sukari. Serikali ilizuia vibali vya uingizaji sukari kutoka nje, hoja ikiwa kuvisaidia viwanda vya ndani. Ukweli ukawa kwamba viwanda vya ndani havina uwezo wa kuzalisha sukari hadi kutosheleza mahitaji ya nchi. Sukari ikaadimika, ikapanda bei. Ilifikia hatua kilo moja kuuzwa Sh5,000.

Hoja ya Serikali kwa jumla ilikuwa kuwatuhumu wafanyabiashara kuficha sukari. Ukishasema bidhaa inafichwa, maana yake unakubali kuwa itauzwa katika soko haramu. Hivyo, kama ilivyokuwa kwa sukari, hata sasa kama kweli mafuta yamefichwa, ni wazi yatauzwa kwa njia haramu na kujenga uchumi wa gizani.

Ni vema kukumbusha au kuweka mkazo kwamba wakati wowote ambao wafanyabiashara wataona wanakabiliana na wakati mgumu katika biashara zao, watatumia njia mbadala ambazo mara nyingi huwa si halali. Mkusanyiko wa njia hizo huipeleka nchi kwenye uchumi wa gizani.

Suluhu ni nini?

Machi 12, mwaka jana, katika mkutano wa kutiliana saini makubaliano ya kutotoza kodi mara mbili kwa bidhaa ziingiazo na kutoka kati ya Ghana na Mauritius, uliofanyika Mauritius, Makamu wa Rais wa Ghana, Dk Mahamudu Buwamia alisema, waliamua kufuta kodi nyingi ili kuipa uhai sekta binafsi.

Bawumia alisema, wamefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika biashara nyingi, ushuru, vilevile Kodi ya Ongezeko la Mtaji (Capital Gains Tax) ili kuifanya sekta binafsi ipumue, ifanye biashara na ipate fedha, kutokana na malengo kuwa wafanyabiashara wakiwezeshwa kimazingira na biashara zikistawi, nchi inapata zaidi.

Nimegusa mfano wa Ghana ili kutuleta kwenye tafakuri kuhusu nini ambacho Serikali ikikishika mambo yanaweza kuwa mazuri pande zote mbili; kwa Serikali kupata mapato mengi, vilevile wafanyabiashara kukua zaidi kibiashara. Kwamba dawa ya magendo, soko haramu na uchumi wa gizani kwa jumla ni Serikali kujenga mazingira yenye kuwawezesha wafanyabiashara.

Hii inanikumbusha wimbo wa mwanamuziki mkongwe nchini, Bizman unaoitwa Naomba. Bizman aliyepata kutamba na Bendi ya In Africa, ndani ya wimbo huo anaimba: “Naomba naomba, ukinipa mama, sitoiba.” Maudhui ya wimbo ni kuhusu mtoto, kwamba akipewa hatoiba.

Inafundisha kwamba kumbe mtoto anaweza kuwa mdokozi kwa sababu anaona akiomba hapewi. Hivyo, hata wafanyabiashara mara nyingi wanaweza kuona bora watumie soko haramu kufanikisha biashara zao kwa sababu wanaona utaratibu halali ama wanawabana au unawaumiza.

Tanzania imekuwa ikipitia vipindi vigumu vya misuguano kati ya Serikali na wafanyabiashara kwa sababu za kimazingira. Wafanyabiashara wanakuwa na malalamiko ya kuumizwa, matokeo yake bidhaa zinaadimika, mwisho wananchi wanaumia kwa kukosa huduma au kuzipata kwa bei kubwa.

Wakati wananchi wakiumia, Serikali inakuwa haipati kitu. Mwisho kabisa inakuwa hasara kwa nchi. Hili ni jambo la kulitazama kwa umuhimu mkubwa. Serikali itengeneze mazingira bora kwa wafanyabiashara ili wastawi. Kuwabana ni kuwaumiza wananchi na Serikali inakosa mapato.

Serikali imekuwa na mwendelezo wa kutoza kodi badala ya kurahisisha mazingira ya kibiashara. Leo hii akina Mohamed Dewji, Salim Bakhresa, Reginald Mengi na wengine wakubwa wanatoa kodi kubwa kwa sababu ni wafanyabiashara wakubwa. Nchi inatakiwa kuzalisha akina Rostam Aziz wengi ili iwe na walipa kodi wakubwa wa kutosha.

Hivi karibuni hata wamiliki wa blogu wameambiwa wawe wanalipa ada za usajili na uendeshaji, wakati wanaweza kurahisishiwa kazi ili wakipata biashara, walipe kodi, Serikali ipate na wao wapate. Kuwabana sasa ni kusababisha washindwe. Wakishindwa Serikali haitopata kitu. Kimsingi kuweka mazingira magumu ya kibiashara kutafanya wananchi wazoee magendo na soko haramu.