Bocco, Okwi utawaambia nini Simba?

Muktasari:

  • Msimu huu sasa, kila mahali John Bocco na Emmanuel Okwi. Ndiyo habari ya mjini.

Msimu uliopita wa 2016/17 ishu ilikuwa Kichuya. Kila kona Kichuya, Kichuya. Utawaambia nini Simba.

Msimu huu sasa, kila mahali John Bocco na Emmanuel Okwi. Ndiyo habari ya mjini.

Wakati wanasajiliwa Simba, unajua kila mmoja alikuwa akipondea. Bocco walisema makapi ya Azam lakini wapo waliosema Okwi mzee, Okwi mhenga, lakini wenyewe wakalifuta jina la mhenga kimyakimya.

BOCCO SI CHOCHOTE

Bocco alikataa dharau za mashabiki kisomi na kuwaonyesha kwamba kamati ya usajili chini ya Zacharia Hanspoppe, haikukosea kumleta Msimbazi baada ya kuanza kuzifumania nyavu kwa kasi na kuamua baadhi ya mechi ngumu. Bocco ana mabao 14 hadi sasa.

KAULI YA BOCCO

Alitaja vitu viwili kuhakikisha Simba inachukua ubingwa na kiatu cha ufungaji kinaenda kwa Okwi.

“Nilikuwa najitahidi kumtengenezea Okwi nafasi za kufunga nikimuona ndani ya 18, lengo nilitaka vitu viwili muhimu vitimie, ubingwa na mfungaji bora vitoke Msimbazi,” anasema.

OKWI MHENGA

Tangu Okwi aondoke Simba, msimu wa 2014/15 na kujiunga na Sønderjyske ya Sweden, Wanamsimbazi walikuwa wanatamani arejee ili aongeza nguvu baada ya kuukosa ubingwa ndani ya miaka minne mfululizo.

Okwi hakutaka kujibizana na mashabiki waliomtunga jina la mhenga, badala yake aliwaonyesha kazi iliyowafanya wanyamaze nakuendelea kumuona mfalme ndani ya kikosi hicho.

KAULI YA OKWI

Anasema kila anachokifanya ni kwa ajili ya maendeleo ya Simba na sio yeye binafsi, akisisitiza hata mabao aliyofunga yametokana na ushirikiano wa timu nzima.

“Furaha yangu ni Simba kuchukua ubingwa na sio kuonekana mimi niwe zaidi ya timu na hilo ndio kiu ya mashabiki ndani ya miaka minne,” anasema.