Bodi ya TRA haikuvunja sheria, ilikiuka maagizo

Muktasari:

Novemba 20, Rais Magufuli alifanya hivyo na siku nne baadaye akiwa kwenye sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania alibainisha sababu za kufanya hivyo.

Rais John Magufuli hakuvunja sheria alipotengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuivunja bodi hiyo hata bodi nayo haikwenda kinyume kufungua akaunti maalumu kwenye benki ya biashara.

Novemba 20, Rais Magufuli alifanya hivyo na siku nne baadaye akiwa kwenye sherehe za mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Tanzania alibainisha sababu za kufanya hivyo.

“Tumekuta kiasi cha Sh26 bilioni zilizokuwa zimetolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya matumizi zimewekwa kwenye Fixed Deposit Account za benki tatu tofauti na bodi ikapitisha. Ndiyo maana nilipozipata hizo taarifa, fedha nikachukua na Bodi kwa heri,” alikaririwa Rais Magufuli.

Vilevile alikumbusha: “Waziri upo hapa, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ambayo ilianzishwa kwa sababu maalum, inachangiwa wakati kuna fedha zao wameziweka kwenye Fixed Deposit Account…waziri, hiyo ni message ‘sent and delivered.’”

Katika hotuba yake Rais Magufuli aliwaonya watendaji wa taasisi za Serikali kuweka fedha zao katika akaunti za muda maalum (Fixed Deposit Account) kwenye benki za biashara kwamba hujipatia kipato binafsi kutokana na riba inayopatikana.

Siku chache baadaye, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema si kosa kisheria kwa taasisi za umma kutunza fedha zao kwenye akaunti za muda maalumu zilizopo katika benki za biashara.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 15 cha Sheria ya Fedha ya mwaka 2001, kwa tafsiri isiyo rasmi: “Hakuna taasisi ya umma inayoruhusiwa kufungua akaunti kwenye benki yoyote isipokuwa kwa kibali cha maandishi kutoka kwa Mhasibu Mkuu wa Serikali.”

Kwenye mkutano wake na wafanyabiashara, muda mfupi baada ya kuapishwa Rais Magufuli aliziagiza taasisi zote za umma kufungua akaunti BoT kwa maelezo kwamba kutunza fedha kwenye benki za biashara kunailazimu Serikali kufanya biashara na fedha zake yenyewe.

Wengi hawaelewi kwanini Rais ametoa maelekezo hayo na wanawataka washauri wake kumshauri abatilishe agizo hilo kwani utaratibu huo unatumiwa na taasisi nyingi kwa muda mrefu.

Mwanasheria wa Mahakama Kuu, Hashimu Rungwe anaungana na Profesa Ndulu kwamba hakuna kosa lolote kwa TRA kuweka fedha zake kwenye akaunti maalumu.

“Fedha nyingi kiasi hicho huwezi kukiweka sehemu nyingine zaidi ya kwenye akaunti kama hiyo. Hata faida itakayopatikana itaisaidia taasisi husika kulipia baadhi ya gharama za kila siku,” anasema wakili huyo wa kujitegemea.

Anafafanua kuwa wajumbe wengi wa bodi hiyo ni wasomi na wenye madaraka nyeti serikalini hivyo ni vigumu wote kwa pamoja kuwa na wazo la kumuibia mwajiri wao kwa manufaa binafsi.

Kwa kilichofanywa na Rais anasema kimepunguza morali wa watendaji hao na wengine huku kikitia doa heshima yao kwenye jumuiya ya wanataaluma. “Washauri wake (Rais) wanapaswa kumshauri sana juu ya masuala haya ambayo wengi tunaona hayaendi sawa,” anasema Rungwe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Umma (Chaumma) Taifa.

Mmoja wa wenyeviti wa bodi za taasisi za umma ambaye ni mhadhiri wa masuala ya uchumi na biashara anasema haoni kosa lolote la kiuchumi lililofanywa na bodi ya TRA kwani taasisi nyingi hufanya hivyo.

Anaenda mbali zaidi na kusema hakuna uwezekano wa wakurugenzi hao au watendaji wa taasisi husika kujinufaisha kwani utunzaji wa fedha hizo hufuata na kuzingatia kanuni za fedha zinazopitishwa na bodi.

“Fedha hizo zinaweza kutolewa muda wowote zikihitajika na zipo benki ambazo hutoa riba hata endapo mkataba utavunjwa kabla ya muda wa makubaliano. Riba inayopatikana husaidia uendeshaji wa taasisi husika,” anasema.

Anasema umuhimu wa kufanya hivyo unatokana na ukweli kwamba hutoa taasisi hizo zikawa na fedha ambazo, kulingana na mipango iliyopo, zitatumika baada ya miezi kadhaa mbele hivyo namna nzuri ni kuzitunza katika akunti hiyo.

Naye anaona walakini kwenye uamuzi wa Rais na kuwataka washauri wa kumuongoza vyema katika masuala nyeti hasa yanayogusa wananchi wengi kama lilivyo hili la fedha.

Anafafanua kuwa menejimenti ya taasisi husika ndiyo inayofanya maamuzi ya namna ya kutunza fedha zake kwa kufuata kanuni na taratibu zilizopo: “Sioni sababu ya bodi hiyo kuvunjwa kwani uamuzi huo ulifanywa na menejimenti. Lakini, hata BoT huwekeza fedha inazokusanya kutoka kwenye vyanzo vyake.”

Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, anasema washauri wa Rais walipaswa kuliona hili mapema na kutoa maelekezo kwa wahusika.

Ofisa mmoja kutoka Hazina, ambaye si msemaji, anasema maelekezo yalishatolewa kwa waatendaji na wakuu wote wa mashirika ya umma.

“Kuna barua ilitumwa Januari 25 ikiwaelekeza kutunza fedha za matumizi yasiyozidi mwezi mmoja kwenye benki za biashara. kwa kiasi kilichosemwa na Rais, nadhani kinazidi muda huo,” anasema.

Mtaalamu wa masuala ya fedha na uhasibu, Audax Kamala anasema kila mwenye dhamana na fedha za mwajiri wake anapaswa kuzitumia kulingana na matakwa ya mwenye nazo.

Anasema licha ya ukweli kwamba TRA haikuvunja sheria yoyote kuweka fedha hizo kwenye akaunti maalumu ila ilipaswa kufuata matakwa ya Rais ambaye ndiye anayezitoa kwa matumizi yaliyoainishwa.

“Ni kweli hawajavunja sheria, hawajafuata agizo la mkuu wa nchi. Sheria inaziruhusu taasisi za umma kuweka fedha kwenye benki za biashara, lakini haizilazimishi kufanya hivyo. Hapakuwa na ugumu wowote kuzipeleka BoT,” anasema.

Audax anasema hata Rais pia hajavunja sheria yoyote ila ametoa maagizo ambayo anataka yatumike kutunza fedha zote za umma bila kuzishirikisha benki za biashara ambazo zitalazimika kutafuta vyanzo vingine vya mapato.

Kwa mujibu wa taarifa za BoT mwaka 2013, kuna zaidi ya benki na taasisi za fedha 50 nchini ambazo zinatoa huduma zake kwa asilimia 14 ya Watanzania wote na Audax anasema nyingi zilielekeza macho kuhudumia taasisi za umma.

“Wananchi wengi hawatumii huduma za benki kwa sababu hawakupewa nafasi hiyo. Huu ni muda mwafaka kwa wakurugenzi wa benki hizo kuwafikia na kuuza huduma walizonazo ili ziendelee kuwepo,” anasema.

Wahasibu wanaeleza, ipo misingi tofauti inayozingatiwa kwenye utunzaji wa fedha kati ya taasisi za umma na zile binafsi. Wakati ikionekana ni sifa ya ufanisi kuwa na ziada kwenye sekta binafsi, kitendo hicho kinaweza kumaanisha kutotekelezwa kwa baadhi ya miradi ya umma.

Na kwa kuwa Rais alishatangaza juu ya utunzaji wa fedha, kufanya kinyume na agizo lake inaweza ikamaanisha hujuma juu ya anachotaka kifanywe.