Bomoabomoa ya Kimara imezika zaidi ya Sh60 bilioni
Muktasari:
- Operesheni hiyo iliyoanza mwishoni wa Julai, inahusisha takriban nyumba 1,300 zenye thamani na matumizi tofauti ambazo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wamiliki, wengi wao wamedai zimewagharimu kati ya Sh40 milioni hadi zaidi ya Sh1.3 bilioni hadi kukamilisha ujenzi wake bila kuhusisha bei ya kiwanja.
Bomoabomoa inayoendelea kwa wakazi waishio pembezoni mwa Barabara ya Morogoro imeteketeza fedha zinazokadiriwa kufikia Sh60 bilioni na zaidi, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.
Operesheni hiyo iliyoanza mwishoni wa Julai, inahusisha takriban nyumba 1,300 zenye thamani na matumizi tofauti ambazo kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wamiliki, wengi wao wamedai zimewagharimu kati ya Sh40 milioni hadi zaidi ya Sh1.3 bilioni hadi kukamilisha ujenzi wake bila kuhusisha bei ya kiwanja.
Wote waliojenga ndani ya umbali usioruhusiwa wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara, watumishi wa umma, nyumba za ibada, hospitali na vituo vya mafuta, wanazungumza lugha moja, kupoteza mali. Wenye kipato cha chini wanakosa pa kwenda baada ya makazi hayo waliyoyategemea kubomolewa.
Kwa wiki mbili mfululizo, Mwananchi limezunguka na kuzungumza na waathirika 50 kati ya 1,300 walioguswa na wanaotarajia kuguswa na operesheni hiyo mpaka itakapokamilika.
Wamiliki wa nyumba hizo kutoka Kimara mpaka Kiluvya, pamoja na mambo mengine walielezea gharama walizotumia kufanikisha ujenzi huo.
Hamza Ismail, anayeishi Kibamba CCM alisema, alifanikiwa kuijenga nyumba yake baada ya kujibana kwa miaka 11 ingawa imebomolewa ndani ya muda mfupi.
“Inauma sana. Nilikuwa naitegemea kupata kodi. Nilitumia zaidi ya Sh95 milioni kuikamilisha,” alisema Hamza.
Anasema kwa muda wote tangu aikamilishe na kuanza kuishi alikuwa akilipa kodi ya majengo kama inavyotakiwa lakini ameshangazwa kuona inabomolewa.
Hata hivyo, wananchi hao wamefungua kesi Mahakama Kuu na inaendelea kusikilizwa wakisubiri hatma yao.
Endapo tathmini ya majengo na viwanja vilivyopo kwenye eneo ingefanyika, taarifa za wathamini zinaonyesha eneo la mita moja ya mraba ina thamani kati ya Sh50,000 hadi 80,000 kwa viwanja vya makazi au taasisi na vile vya biashara ni kati ya Sh70,000 hadi Sh112,000. Vile vya makazi na biashara vingelipwa kati ya Sh55,000 hadi Sh88,000.
Thamani hiyo kwa maeneo yaliyopo Kibamba kwa skwea mita moja ni kati ya Sh5,000 hadi Sh25,000 kwa viwanja vya makazi ni Sh7,000 hadi 35,000.
Kwa vile vya biashara, vikigharimu kati ya Sh55,000 hadi Sh110,000.
Bomoabomoa hiyo inayotekelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), haijalipa fidia na kama malipo hayo yangefanyika, fedha nyingi ambazo zinaweza kununua zaidi ya ndege moja aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba zaidi ya abiria 70, zingehitajika.
Na pia, kama fedha za thamani ya nyumba zilizobomolewa zingetumika kujenga barabara ya njia mbili; kwenda na kurudi, kwa kiwango cha lami, kwa gharama za sasa ambazo ni takriban Shilingi bilioni moja kwa kilomita, basi ingefika Mlandizi.
Fedha hizo pia zingeweza kumaliza uhaba wa madawati uliopo nchini.
Mwaka 2014, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda alisema kuna upungufu wa zaidi ya madawati 1.46 milioni baada ya kueleza yaliyokuwapo yalikuwa milioni 1.8 wakati mahitaji yalikuwa milioni 3.3. Kiasi hicho pia kingeziba upungufu uliopo baada ya Rais John Magufuli kuanzisha utengenezaji wa madawati kwa bei ya Sh120,000.
Basi fedha hizo zingeweza kununua zaidi ya madawati 500,000 na kero ya uhaba wa madawati na wanafunzi kukaa chini ingemalizika.
Lakini sheria lazima ifuate mkondo wake. Miradi ya maendeleo inapaswa kutekelezwa kwa faida ya kizazi cha sasa na baadaye kama Serikali ilivyopanga. Kwa kulitambua hilo, Tanroad wanaendelea kusafisha njia ili hifadhi ya barabara iwe wazi kuruhusu ujenzi wakati wowote itakapohitajika kufanya hivyo.
Endapo mipango iliyopo itatekelezwa, foleni iliyopo jijini hapa itapungua kama si kumalizika kabisa na kurahisisha usafiri kwa wananchi watakaoweza kuishi hata maeneo jirani ya Kibaha na Mlandizi yaliyoko mkoani Pwani na mkoani Morogoro.
Mmiliki wa Hoteli ya Peacock ya jijini Dar es Salaam, Joseph Mfugale naye ni miongoni mwa waathirika wa operesheni hiyo. Alisema alijenga nyumba yenye ghorofa moja tangu mwaka 1996, lakini hawezi kudai fidia kama Serikali ilivyoelekeza.
“Kwa kweli inaumiza kuona nyumba niliyoiijenga kwa taabu inabomolewa, lakini utafanyanini, ndiyo maendeleo. Ninachoomba Serikali iwaangalie waliojenga kabla ya kupitishwa kwa Sheria ya mita 30 kwa sababu walijua wako nje ya hifadhi ya barabara, ifikirie kuwalipa fidia,” alisema.
Hospitali ya Neema Health Service iliyopo Kimara Bakery, nayo imekumbwa na kadhia hiyo. Mmiliki wake, Dk Charles Koka alisema kwa sasa hana cha kufanya kwani ndiyo iliyokuwa ikimuingizia kipato cha familia yake na amewekeza fedha nyingi na ilikuwa bado haijaanza kurudisha faida kwa kuwa imejengwa hivi karibuni.
“Nimetumia takriban Sh200 milioni kuijenga, lakini leo inabomolewa, tena bila kulipwa fidia. Nitafanya biashara gani sasa wakati fedha zangu zote nimezizika hapo,” alilalamika daktari huyo.
Anasema ndoto zake zimepotea ghafla baada ya kubomolewa kwa hospitali hiyo ambayo haina muda mrefu tangu ianze kutoa huduma. Tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani imejielekeza kwenye kuimarisha miundombinu kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi.
Ndani ya takribani miaka miwili na nusu ya kuwapo madarakani, tayari miradi mikubwa ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro imeanza kujengwa.
Pia, barabara ya kutoka Morocco mpaka Mwenge, jijini Dar es Salaam imepanuliwa hivyo kupunguza foleni, wakati flyover za Tazara na Ubungo zikiendelea kujengwa katika hatua mbalimbali.
Daraja litakalopita Bahari ya Hindi kutoka ilipo Hospitali ya Aga Khan mpaka Coco Beach, Dar es Salaam, nalo litaongeza mvuto kama ilivyo kwa lile la Nyerere linalounganisha Eneo Kuu la Biashara (CBD) lililoko wilayani Kigamboni.