Bonsai: Kilimo rafiki wa mazingira

Bustani yake imesheheni  mazao mbalimbali aliyopanda kwa kutumia teknolojia ya bonsai.

Muktasari:

Mmoja wa wataalamu wa kilimo cha bonsai nchini, Mini Gopal anasema kilimo hicho cha bustani kinalimwa  katika nchi za Japan, China na India.

Je, una shauku na mapenzi ya kilimo cha mazao ya bustani, lakini unakwazwa na ukosefu wa ardhi ya kutosha?

Kilicho muhimu ni dhamira yako, kwani hivi sasa baada ya kukua kwa teknolojia, binadamu hahitaji kuwa na eneo kubwa kwa ajili ya kulima.

Ua wako unatosha kuwa bustani na hata kwa wakazi wa maghorofani wanaweza kulima wakiwa hukohuko ‘hewani’.

Kilimo cha Bonsai

Kilimo cha  bonsai  (neno lenye asili ya Kijapan), kinatumia zana rahisi zinazopatikana katika mazingira yetu kama masufuria, vyungu, makopo, ndoo.

Ndani ya zana hizi unaweza kulima mazao ya mboga, matunda, viungo vya kupikia, miti ya kivuli na mengineyo.

Teknolojia hiyo ni mpya nchini na walioanza kuitumia wanasema hilo ni suluhisho kwa watu ambao hawana ardhi ya kutosha.

Mmoja wa wataalamu wa kilimo cha bonsai nchini, Mini Gopal anasema kilimo hicho cha bustani kinalimwa  katika nchi za Japan, China na India.

Anasema  ulimaji wa kilimo hicho katika nyumba unasaidia mambo mengi ikiwamo  kuongeza uzuri wa mazingira, hewa nzuri ya asilia na kupunguza gharama za ununuzi wa matunda na mboga.

 “Nina miaka 10 katika kilimo hiki ambacho nilianza kulima tangu nikiwa Uganda kabla ya kuhamia hapa, hivyo siyo lazima uwe na shamba kubwa. Unaweza ukawa na eneo lako nyumbani na kuanzisha kilimo cha bonsai ambacho hakina gharama kubwa,” anasema Gopal.

mwanamke huyo ambaye amesomea masuala ya kilimo nchini India anasema  kimemsaidia kutimiza malengo ya kuwa na nyumba yenye bustani ya miti ya matunda,  ya kivuli na mbogamboga.

“Mapenzi yangu ndiyo yamenifanya nipende kilimo hiki na hii inatokana na wazazi wangu kuwa wakulima wazuri wa kilimo cha bonsai nchini India,” anasema.

Jinsi ya kulima

Anasema ili mti ustawi vizuri kama  mwingine uliopandwa katika ardhi, hukatia mizizi mara moja kwa mwaka na mmea unaweza kustawi na kuishi zaidi ya miaka mitano bila kuzeeka.

Katika kazi hiyo hutumia mikasi na visu vyenye ncha kukatia mizizi na huchimbua chini ya mti na kukata mizizi, kisha hupanda tena bila kusahau kukatia matawi ya juu ili mmea uweze kuzaa vizuri.

“Siyo vyungu vyote vinatumika kupandia mimea hii kwani kuna mingine inahitaji kupandwa katika vyungu maalumu na siyo kwenye makopo na baadhi ya vyungu huagiza kutoka China, ” anaeleza.

Anasema ili mti wa matunda uweze kustawi vizuri na kutoa matunda yenye ubora, ni lazima akate mizizi na ndiyo njia pekee inayotofautisha kati ya kilimo cha bonsai na aina nyingine za kilimo.

“ Miti yote niliyopanda ya matunda, kivuli na mboga za majani mbegu yake nimenunua Soko la Kariakoo. Ni mbegu halisi na wala siyo za kisasa,” anaongeza.

Ili kuandaa kilimo hicho, anasema huchukua udongo wa kawaida na kuuchanganya na takataka kama zipo na zisipokuwa hupanda katika makopo au vyungu na kumwagia maji wiki nzima kabla ya kupanda miche ya matunda au maua. Baada ya hapo huendelea kumwagia maji ya kawaida kwa siku mara mbili, yaani asubuhi na jioni.

“Teknolojia ninayotumia katika kilimo hiki, mbali na kukata mizizi ni kwamba mmea ukishakua kidogo lazima niufunge kamba chini kama tunavyofunga kuku mgeni, ili mti uweze kuwa na umbo la namba nane na hii husaidia mmea kutokuwa mkubwa kama ile tunayopanda katika ardhi,” anaeleza na kuongeza:

 “Hapa nyumbani kwangu nimefanikiwa kupanda miti 500 ya aina tofauti kwa maana ya miti ya matunda, kivuli na ya maua bila kusahau mbogamboga.’’

Katika bustani ya Gopal amepanda  maembe, ndizi, makomamanga, matopetope, ukwaju, mastafeli,  machungwa, malimao, mapera, mlonge, zabibu, tende, zambarau, ‘bitruit’ na matango yakiwamo wanayotumia wagonjwa wa kisukari na shinikizo la damu.

Kwa upande wa viungo, mtaalamu huyo amelima hiliki, tangawizi yenye harufu ya embe, karafuu,  michaichai, pilipili manga, binzari, abdalasini, pilipili hoho, pilipili mbuzi na majani ya nana (mint).

Pia, amelima magimbi, viazi vitamu,  viazi mviringo, kabichi,  matembele, spinachi, maharage marefu ambayo huzaa ndani ya miezi miwili na mchicha.

Upandaji wa maua

Anasema pia hupanda maua katika makopo ambayo hukaa zaidi ya miaka mitano bila kuharibika.

“Tofauti na maua mengine tunayopanda katika makopo au vyungu, maua ninayopanda kupitia kilimo cha bonsai - napanda kwa kupandikiza, nakata ua kubwa napanda kama muhogo, lakini juu nalichana kidogo halafu napandikiza tawi kwa juu na ndiyo maana maua yote yana umbo kama namba nane. Yote hiyo ni kutokana na teknolojia hii kupandikiza na kukata mizizi,” anasema.

Pia, kuna maua ambayo hayatumii udongo badala yake yanatumia maganda ya nazi na mkaa na kumwagiliwa maji mara mbili kwa siku kama ilivyo kwa maua mengine.

Mikakati yake                                                         

“Mikakati yangu ni kuendelea kutoa elimu kwa watu wengine ambao wanavutiwa na wanapenda kujifunza kuhusu kilimo hiki ikiwamo kufundisha wanafunzi wa Jiji la Dar es Salaam kilimo cha bustani aina ya bonsai,” anasema.

Kwa sababu hiyo, anasema yupo mbioni kufanya maonyesho ya kilimo hicho nyumbani kwake kwa  lengo la  kutoa elimu ya namna ya kulima na manufaa yake.

“Nimeona watoto wa shule ninaowafundisha pale Tambaza wamevutiwa na kilimo hiki, hivyo nitaendelea kutoa elimu kwa shule mbalimbali za hapa jijini bila gharama yoyote,” anasema.

Unaweza kuwasiliana naye kuhusu kilimo hiki kwa barua pepe: [email protected]