Bright Masambu; Kijana anayekuja juu katika ushonaji suti

Sunday November 19 2017

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mmoja kati ya vijana wanaosifika kwa uhodari wa kutengeneza suti kali ni Bright Masambu. Pamoja na mavazi maridadi anayowabunia wateja wake, nyuma yake ipo historia ambayo vijana wengi wanapaswa kuisikia ili iwasaidie kupigania ndoto zao.

Kama ilivyo kwa wajasiriamali wengi, safari ya Masambu kufikia alipo sasa imekuwa ndefu yenye milima na mabonde. Njia alizopitia ndizo zinazomfanya afurahie kila shilingi inayotokana na jasho alilovuja.

Miaka mitano iliyopita aliingia jijini Dar es Salaam akitoka mkoani Mara alipoishi maisha yake yote. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 26 aliingia jijini siyo kwa lengo la kufanya biashara ya kutengeneza nguo bali kujiendeleza na elimu ya juu katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).

“Nilifika IFM kwaajili ya kuanza masomo hata hivyo sikuwa na mkopo. Nilianza masomo lakini baada ya miezi kadhaa ilibidi nisitishe kwa kuwa sikuwa na uwezo wa kulipa karo na kujikimu. Hata hivyo, ilibidi nitafute namna ninayoweza kujiinua na baadaye kuendelea na masomo, ndipo nilipoanza kuuza vipodozi na baadaye nguo,” anasema Masambu.

Kwa bahati nzuri juhudi hizo zilimwezesha kurudi chuo mwaka uliofuata na huku akiendelea na biashara zake aliweza kulipa karo na kujikimu.

Biashara ya nguo

Anasema utanashati wake ndio uliompeleka katika kona ya ubunifu wa mavazi ya kiume: “watu wanaonifahamu wanajua ninavyopenda kuwa nadhifu na hiki ndicho kilichonichagiza kuingia katika biashara hiyo.”

Nembo yake ya Bright Wear ilizaliwa baada ya kupata uwezo wa kukodi chumba kimoja ambacho aliweka cherehani na kuanza kushona mashati ya kiume kisha akaongezea na suti.

“Sikuwa na ujuzi wowote wa kushona wakati naanza lakini asikwambie mtu penye nia pana njia, pia sikuwa na mtaji.” anafafanua.

Alianza kwa kuchukua sample za vitambaa kutoka katika maduka mbalimbali na kuwapelekea wateja wachague, wanapotoa kianzio (advance) yeye huitumia kununua kitambaa na kumshonea mteja wake kisha anapomkabidhi huchukua fedha iliyobaki.

Mpaka sasa anajivunia kuwavalisha wabunge wakiwamo Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamis Kigwangallah, David Silinde, John Heche, Musa Ntimizi na wengine.

Anapataje wateja?

“Kwa mfano hawa wabunge niliwafuata Dodoma kwenda kujinadi ninachofanya, nashukuru Mungu wapo walioniamini na nikawafanyia kazi nzuri,” anafafanua.

Anasema hutumia njia hiyo ya kujitangaza kwa watu mbalimbali lakini anategemea zaidi wateja wake kuwa mabalozi.

“Mteja wangu akivaa suti au shati nililomshonea ananiwakilisha na kunitangaza, akipendeza watu wanamuuliza nani amekushonea na hiyo ndiyo namna ninayopata wateja, lakini huwa ninatumia mitandao kujitangaza na ninashukuru inaniletea wateja,” anasema.

Ana mpango wa kuajiriwa?

“Niajiriwe wapi tena na Bright Masambu imeshanipa ajira?” Anahoji Masambu ambaye ni muhitimu wa Shahada ya Masuala ya Bima.

Anasema anajiona akifika mbali na kile alichokianzisha kwani mpaka sasa amefanikiwa kuajiri watu wanne na kwamba kwa namna mambo yanavyozidi kumnyookea atapanua biashara yake.

Advertisement