HEKAYA ZA MLEVI: Bucha tofauti lakini nyama ileile

Muktasari:

Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili ni nadra kukuta maneno yenye herufi X na Q ila tu kwenye majina tuliyoyakopi kwa wenzetu. Lakini kwenye baadhi ya jamii unaweza kuyakuta maneno yanayobeba herufi hizo na zingine tusizoweza kuziandika kwa sababu hazimo kwenye A-Z.

Wabantu tunatumia mfumo wa herufi ishirini na sita kutoka A mpaka Z. Matumizi ya herufi hizi hutegemea lugha ya jamii husika; zipo jamii zinazotumia herufi zote kwa usawa na zingine hazitumii baadhi ya herufi.

Kwa mfano katika lugha ya Kiswahili ni nadra kukuta maneno yenye herufi X na Q ila tu kwenye majina tuliyoyakopi kwa wenzetu. Lakini kwenye baadhi ya jamii unaweza kuyakuta maneno yanayobeba herufi hizo na zingine tusizoweza kuziandika kwa sababu hazimo kwenye A-Z.

Mgiriki ana A (Alpha) mpaka Ω (Omega). Mchina ana zake. Mrusi, Mhindi na Muarabu pia wana zao ambazo kimsingi zinaweza kufanana na zetu lakini kwa muonekano tofauti. Katika picha ya Kihindi lilikuwepo kubwa la maadui tuliloliita Shotgan Singh (Shatrughan Sinha). Lilimwambia mtu “Banduki Chin!” na aliyeambiwa hivyo aliweka bunduki chini. Ila kauli hiyo ikiandikwa hapa hatutaelewana!

Wahenga wetu walitumia maneno haya haya tunayotumia leo kutoa elimu katika kizazi chao. Kadhalika nasi tukaendeleza yote mazuri yanayotufaa hadi sasa katika kizazi chetu. Tunaona haya katika mila, tamaduni, miiko na kadhalika.

Katika mchanganyiko wa jamii ulioanzishwa kwa kiasi kikubwa na wafanyabiashara, dunia ilijikuta ikiwa tena kitu kimoja. Wauza viungo vya chakula kama pilipili manga, amdalasini na iliki walisafiri kutoka Mbali kuja kubadilishana na pembe za wanyama na madini. Tukagundua kuwa sisi na wao tunatofautiana lugha na rangi tu, lakini ubinadamu na mafundisho ni yale yale.

Kama ijulikanavyo watoto wachanga wanapokutana huanza kuwasiliana hata kama hawajui lugha. Na wafanyabiashara wale walipokuwa huku walivutiwa na mabinti wetu na kuanza uchokozi. Mambo yaliendelea hadi tukawa na wakwe na mashemeji Wahindi, Waarabu na Wazungu.

Hapa ndipo mchanganyiko wa tamaduni ulipoanza. Tukaanza kuona matumizi ya vitambaa vya kitani na hariri, vipini vya pua na vinginevyo visivyorithiwa kutoka ezi za wahenga wetu. Hata wao walihamisha baadhi ya tamaduni zetu zilizowapendeza na kuendelea kuzitumia.

Lakini pamoja na yote hayo, mambo ya msingi ya kibinadamu yaliendelea. Watu wa jamii yetu waliendelea kuoana na kulea familia kama awali, na wale waliochanganyika na wageni hawakutofautiana sana na wenyeji katika mambo ya msingi.

Hata hivyo waliibuka malimbukeni waliozua taharuki kwenye jamii. Baadhi ya wenzetu hasa Wazungu walitokea kwenye nchi zenye ubaridi sana. Kwa kutokuizoea kwa haraka hali ya fukuto huku kwetu, walipendelea kushinda ufukweni baada ya kazi na siku za mapumziko.

Baadhi ya wahanga wa tamaduni za kigeni walipowaona Wazungu wakitembea ufukweni wakiwa mavazi ya kule nao waliingia barabarani wakiwa hivyo kwa madai ya kuwa nao walielekea ufukweni. Nawaita malimbukeni kwa sababu lile ni vazi la ufukweni, sio la kuendea ufukweni.

Na kwa bahati mbaya kila wenzetu wakianzisha jambo, sisi tunalichukua na kuongeza majanga. Wao wanaweza kuwa na sababu inayowalazimisha kuanzisha, lakini sisi sijui inakuwaje!

Wakati mwingine unaweza kudhani kuwa herufi zetu 26 zinatofautiana maana na zao. Kwa mfano wao walitengeneza “swimming cost” kwa maana ya “chupi za kuogelea”. Sasa utashangaa zilivyogeuzwa kuwa “chupi za kuendea kuogelea”!

Wale wapenda maisha ya Insta angalieni hili linalokuja hivi sasa:

Siku hizi habari mpya ni ndoa za mikataba. Binti ana hiyari kuolewa na mume asiyempenda kwa sababu tu anataka mali. Wanaandikiana mbele ya mashahidi pale Bomani na kwenda kuishi kwa matarajio ya kugawana majumba na magari.

Naam… Wabongo wameshazinasa za Marekani ambako wadada warembo wanaweza kuolewa na matajiri zaidi ya kumi kwa mikataba ya vipindi tofauti. Tena anaweza kuvunja mkataba baada ya kupandiwa dau na tajiri mwingine.

Kama kawaida yetu, hili nalo tunalichukua bila ya kulifanyia utafiti wa kina. Mikataba ya wenzetu huainisha muda, shughuli atakazofanya binti, idadi ya watoto na matunzo yake wakati wote wa mkataba. Tumeona mifano ya mikataba hii kupitia kwa Robbin Givens na Jlo.

Jlo ameshasaini na vidume zaidi ya ishirini ukijumlisha wale maarufu zaidi kama Alex Rodriguez, Drake, Maksim Chmerkovskiy, Casper Smart, Bradley Cooper, Rodrigo Santoro, Marc Anthony, Ben Affleck, Cris Judd, P Diddy, Ojani Noa, David Cruz, Wesley Snipes na Chris Paciello. Na bado!

Sasa hapa kwetu kumekuwepo habari nyingi sana za mavunjiko ya ndoa baina ya vijana wafanyabiashara na wasanii wenye ukwasi. Mwisho wa yote kwa sababu mkataba wetu haufanani na wa wenzetu, binti anaishia kulia akidai “matunzo ya mtoto.”

Ukweli haipendezi kufikia huko. Hebu fikiria mtoto wenu akigundua kuwa alizaliwa kutokana na mkataba na si mapenzi, atakuwa mtu wa aina gani huko ukubwani mwake? Siwashauri kabisa mabinti zetu kuparamia ndoa za mchepuo huu.

Lakini kama hapana budi basi wahakikishe wanapata nakala ya mkataba wa Jlo. Ni kweli kidume kinaweza kutumia “kiki” ya ndoa kuuza albamu zake na kikishaona kimepanda chati kinampiga mwenzie kibuti. Muwe makini sana binti zangu.