Bundi aanze kuinyemelea Manispaa ya Bukoba

Bundi ni ndege mwenye macho makubwa na uwezo wa kusafiri bila shida usiku wakati wa giza. Katika maeneo mengi duniani kote, ndege huyu hutazamwa kiimani kama kiumbe chenye mikosi kinachobashiri misiba na visirani.

Ndege huyo kwa sasa ni kama anaonekana kwenye viunga vya mji wa Bukoba akitafuta mti wa kutua. Anataka kupiga kambi ili usiku wakati wa giza nene atoe mlio utakaowachanganya wenyeji na waanze kushikana uchawi.

Akiwa bado angani, kivuli chake tayari kimeanza kuwachanganya viongozi ambao wameanza kutofautiana hadharani kwa kauli kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi.

Hii ni miradi kiporo ambayo ilikwama kwa miaka mitano iliyopita baada ya viongozi walewale waliompa ‘bundi’ makazi ya kudumu katikati ya mji na kujikuta wanaingia kwenye mkwamo wa kisiasa.

Miradi hiyo ni ujenzi wa soko jipya la kisasa na kituo cha mabasi cha Bukoba ambacho kingejengwa nje kidogo ya mji.

Pamoja na kukwama kwa miradi hii muhimu, mahitaji ya huduma hizo yanaongezeka kila siku, hivyo kuwa na ulazima wa kuwa na maeneo yaliyoboreshwa.

Baraza la Madiwani

Tofauti na kipindi kilichopita (2010-2015), Baraza la Madiwani sasa linaonekana kuunganika. Lina lugha moja kwenye miradi ya maendeleo kwa kuwa baadhi ya madiwani waliorejea wanajua chanzo cha anguko la wenzao katika uchaguzi uliopita. Ni tatizo lilile na miradi hii mikubwa.

Pamoja na kuwa manispaa hiyo inaongozwa na wapinzani, ni vigumu kumsikia diwani wa CCM akipinga hadharani utekelezaji wa miradi waliyopitisha, tofauti na hali ilivyokuwa kwenye Baraza lililopita.

Tahadhari ya kudhibiti mgawanyiko ilichukuliwa kuanzia kwenye usukaji wa kamati. Mpaka sasa wamefanikiwa kudhibiti sauti ya bundi isipenye kutoka nje kupitia kwenye nyufa ambazo zingeachwa wazi.

Mgogoro wa awali kwenye Baraza la Madiwani lililopita uligharimu Taifa, hususani Manispaa ya Bukoba, baada ya mamilioni ya shilingi yaliyokuwa yametolewa na Benki ya Dunia (WB) kujenga barabara kurejeshwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni kwenye Baraza hilo, WB tayari imetoa kiasi cha Sh6 bilioni kwa ajili ya barabara kwa kuamini kuwa madiwani wamejirekebisha na wanahudhuria vikao na kushirikiana uamuzi kama kipimo cha utawala bora.

Pamoja na utulivu uliopo miongoni mwa madiwani, mambo ni tofauti nje ya ukumbi wa Baraza. Kuna dalili zote za kutaka kuwaingiza kwenye mtego wa kupinga maamuzi yao wenyewe. Na hapa ndipo bundi anapotaka kupitia.

Hofu imeanza

Hata kabla ya kuanza upya utekelezaji wa miradi iliyochacha, Kamati ya Siasa ya CCM Manispaa ya Bukoba imetangaza kunusa ufisadi kwenye miradi ambayo hata mikataba haijasainiwa.

Katika kikao kilichofanyika kujadili utekelezaji wa ilani ya chama hicho, baadhi ya wajumbe waliomba Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG) aitwe kuchunguza miradi ya soko na stendi mpya la sivyo hawawezi kuipokea.

Mwenyekiti wa chama hicho katika Manispaa ya Bukoba, Joas Muganyizi aliunga mkono kuwepo kwa harufu ya ufisadi akisema kuwa mpango wa kukopa Sh14 bilioni kutoka Benki ya Raslimali (TIB) kwa ajili ya mradi huo utakuwa ni mzigo kwa watumiaji wa soko.

Hii ni benki inayotoa mikopo kama zilivyo benki nyingine ingawa ni chombo cha Serikali, kwenye huu mradi kuna watu wana masilahi yao mkopo wa Sh14 bilioni utakuwa mzigo wa walioko sokoni,” alisisitiza Muganyizi.

Anaona kwamba ni bora soko jipya lisijengwe kwa kuwa mradi huo utaathiri wafanyabiashara wanaounga chama mkono wakati mikakati yao ni kutaka kulikomboa Jimbo la Bukoba kutoka upinzani.

Kauli ya Polepole

Suala la miradi mikubwa ya Manispaa ya Bukoba kukwama linajulikana vema hata kwa viongozi wa CCM ngazi ya Taifa kwa kuwa ilikuwa ni miongoni mwa kero sugu zilizojadiliwa kwenye vikao vyao.

Katika kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa St. Francis Aprili 28, 2017, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole pamoja na mambo mengine alisema suala la ubovu wa stendi ya Bukoba si mzigo wa kubebwa CCM.

Kauli hiyo aliyoitoa zaidi ya mwaka mmoja uliopita inatakiwa kupimwa kwa uzito wake hasa katika kipindi hiki ambacho tayari kuna kivuli cha bundi kinachozunguka utekelezaji wa miradi hiyo.

Mkandarasi akimbia

Lipo tukio la ajabu ambalo kama yapo mengine, yatakuwa machache nchini ya aina hii, ambayo mkandarasi aliyepatikana kwa njia halali ya ushindani na kushinda zabuni baadaye anakimbia kusaini mkataba.

Ndivyo ilivyokuwa uongozi wa Manispaa ya Bukoba umelalamika kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali (mstaafu), Salum Kijuu kuwa umepata hasara kwa kuwa aliyeshinda tenda ya ujenzi wa barabara ameukimbia mkataba bila maelezo.

Kutokana na hatua hiyo mchakato wa kutangaza tenda ni lazima urudiwe, jambo linalochelewesha kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo wa Sh6 bilioni wa ujenzi wa barabara chakavu za Manispaa ya Bukoba.

Pamoja na mkuu wa mkoa kuagiza mkandarasi huyo akamatwe na kupelekwa ofisini kwake, bado hakijasikika kishindo cha kumkimbiza bundi ili asikwamishe mradi huo.

Bundi ndani ya Kaitaba

Uzinduzi wa michuano ya soka ya ‘Kamala Cup’ katika uwanja wa Kaitaba mwezi Februari, ulitumiwa na mmoja wa viongozi wa chama cha soka Manispaa ya Bukoba kupinga mradi wa stendi mpya ya mabasi eneo la Kyakailabwa.

Mashabiki wa soka walibaki kwenye mshangao baada ya kiongozi huyo kuongeza msisitizo bila kuwaeleza kama yalikuwa ni maoni yake binafsi au msimamo wa chama anachoongoza.

Kiongozi huyo aliyepo safu ya juu kwenye wilaya badala ya kuzungumzia umuhimu wa michuano husika, aliwaomba wana CCM kupinga uhamishaji wa stendi, akisema hilo likitokea mji utadumaa na kubaki ukiwa.

Meya afunguka

Meya wa Manispaa ya Bukoba, Chief Karumuna ndiye alipewa nafasi mara nyingi zaidi kuongea kwenye Kikao cha Ushauri wa Mkoa hivi karibuni, fursa ambayo hutokea mara moja kila mwaka.

Alitumia fursa hiyo ‘kukiteka’ kikao na kuwaonyesha wajumbe jinsi miradi ya maendeleo ya wananchi ilivyoanza kuhujumiwa. Alishangaa mkandarasi anawezaje kushinda tenda, lakini akakimbia kusaini na Serikali ikawa kimya.

Bila kupepesa macho aliwatuhumu baadhi ya viongozi kutaka kuwagawa madiwani na wananchi kwa kusambaza propaganda kuwa fedha za miradi zimetafunwa ili wafadhili wakate tamaa na miradi ikwame.

Alionya na kutahadharisha kuwa Manispaa ya Bukoba imejikwaa mara nyingi na ndiyo sababu leo hii inaonekana hivi ilivyo na kuwa miradi inalenga maendeleo ya wananchi na sio kwa manufaa ya chama chochote cha siasa.

Kwamba Bukoba imekuwapo kabla ya vyama vya siasa na viongozi wanaopinga Bukoba isiwe katika hali iliyoboreshwa kwa kutanguliza masilahi ya vyama vyao kisiasa utafika wakati wataondoka.

Alikijulisha kikao kuwa Baraza la Madiwani limeungana kwa kujua makosa yaliyofanyika awali na kuwa maamuzi ya Baraza hayawezi kupingwa kwenye vijiwe vya kahawa.

Katika kikao hicho kinachojumuisha viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka wilaya zote, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Costancia Buhiye alisema ana imani timu hiyo itawaandalia njia ya kujibu maswali ya wananchi kuanzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani.

Ufa kiutendaji

Kwa upande wa pili watumishi wa Manispaa wanategemewa kusukuma ajenda za maendeleo ya wananchi kwa kufanya utekelezaji baada ya kupata baraka za Baraza la Madiwani.

Hata hivyo, kwa Manispaa hii ambayo haijapata Mkurugenzi mpya baada ya aliyekuwepo uteuzi wake kutenguliwa na Rais John Magufuli, si rahisi mtumishi anayekaimu nafasi hiyo kutoa uamuzi kwenye mambo mazito.

Suala la kukaimu nafasi kwa muda mrefu linadhoofisha utendaji, aliyekalia kiti hicho kwa muda hawezi kuwa na msukumo wa kufanya ubunifu ili kuleta ufanisi.