Bunge kutochunguza kupotea Azory, Saanane ni kukata kitovu cha Katiba

Muktasari:

  • Katiba ya nchi yetu inatamka kwenye utangulizi kuwa malengo ni kujenga jamii yenye misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Mambo hayo manne ndiyo yenye maana ya kulileta pamoja Taifa lenye kujali utu. Hivyo, kutosimamia misingi ya utu wa Mtanzania ni kukata kitovu cha Katiba.

Mtoto anapozaliwa, kitovu chake huchukuliwa na kufungwa kwa umakini, maana ni uhai wake. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua kitovu cha ujenzi wa Taifa ni utu, ndiyo sababu ni kitu cha kwanza na kimewekewa mkazo katika makabila mbalimbali.

Katiba ya nchi yetu inatamka kwenye utangulizi kuwa malengo ni kujenga jamii yenye misingi ya uhuru, haki, undugu na amani. Mambo hayo manne ndiyo yenye maana ya kulileta pamoja Taifa lenye kujali utu. Hivyo, kutosimamia misingi ya utu wa Mtanzania ni kukata kitovu cha Katiba.

Zaidi ya miezi sita imepita tangu mwandishi wa habari wa kujitegemea, anayeripoti gazeti la Mwananchi, Azory Gwanda achukuliwe na watu wasiojulikana. Zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa umekatika, tangu kada wa Chadema, Ben Saanane alipotoweka. Utowekaji wao ni tata. Na ni suala lenye kuhusu uhuru wa Mtanzania. Kutojali kupotea kwao ni kukata kitovu cha Katiba.

Kilichotokea bungeni

Hivi karibuni, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe, alieleza bungeni kuhusu kupotea watu takriban 380 Pwani na kuomba Bunge lichunguze kadhia hiyo. Kabla ya Zitto, Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara ‘Bwege’, alieleza kupotea watu wawili jimboni kwake baada ya kukamatwa na polisi. Mpaka leo hawajulikani walipo.

Zitto alipokuwa anawasilisha hotuba yake, aliweka nia ya kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kuliomba Bunge lichunguze matukio hayo ya kupotea watu na mengine ya ukiukwaji wa haki za binadamu kama kupigwa risasi mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuuawa kwa kupigwa risasi, mwanafunzi Akwilina Akwilini na mengine.

Katika kipindi hiki Bunge la Bajeti likishika kasi, Zitto aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuwa wabunge wa CCM, walitumia mtaji wao wa kuwa wengi bungeni kuzima hoja hiyo ya kuchunguza matukio hayo.

Wabunge wanapaswa kukumbuka kuwa kukataa kuchunguza au kukalia kimya matukio yenye viashiria vya kupoka uhuru wa watu pasipo haki ni kukata kitovu cha Katiba. Wabunge waondoe siasa kwenye masuala yenye kuhusu utu.

Vyama vya siasa kwa historia ya kuanzishwa kwake ni kutetea maslahi ya watu. Bunge pia katika msingi wa kuanzishwa kwake ni kuhakikisha nchi na jamii zote zinaongozwa kwa matakwa ya watu.

Kuongoza kwa mifano

Karne tano kabla ya ujio wa Kristo, aliyekuwa kiongozi wa Ugiriki ya kale, Solon alikataa kuwa mtawala bali kiongozi. Na katika uongozi huo, alipenda kushirikisha watu.

Kwa mahitaji hayo, Solon aliunda chombo ambacho kiliitwa Bunge la wananchi, kikaitwa Ekklesia, yaani Bunge la Waathen. Watu wote maskini na matajiri, walijumuika katika Ekklesia kutoa mawazo yao ya jinsi ya kuongoza jamii yao.

Nyakati zikapita, ukafika wakati kwamba Bunge haliwezi kushirikisha watu wote, hivyo wananchi huchagua wawakilishi wa kwenda kutetea maslahi yao. Hivyo, msingi wa Bunge kwa uwepo wake, ni chombo cha kutetea maslahi ya watu. Na katika maslahi ya watu, utu ndiyo kitu chenye kutangulia.

Vyama vya siasa

Mpaka kufikia Karne ya 17, yaani miaka ya 1,600, duniani kote hakukuwa na vyama vya siasa, ingawa siasa zilizungumzwa na kujadiliwa tangu Karne ya 5 baada ya Kristo.

Mwanzoni kabisa katika uliokuwa utawala wa Roma ya kale, seneti yake iliwakilishwa na makundi mawili; kundi la viongozi na watu wenye hadhi kubwa kwenye jamii na kundi la wafanyabiashara wakubwa.

Hivyo, makundi hayo huwezi kuita mwanzo wa vyama vya siasa kwa sababu makundi mawili ya watu waliojiona wapo daraja la juu, walikutana kujadili maslahi yao na jinsi ya kuwatawala wananchi maskini.

Vyama vya siasa vilianza mwaka 1678 kutokana na nadharia inayoitwa Popish Plot. Kwa ufafanuzi ni kuwa Popish Plot ni uzushi uliotungwa na Mwingereza Titus Oates, ukieleza kuwa Kanisa Katoliki lilipanga kumuua aliyekuwa Mfalme wa England, Charles II.

Katika uzushi huo, alilitumia Kanisa Katoliki kumchonganisha Mfalme Charles II na mdogo wake, James au Duke wa York. Alisema kuwa Kanisa lilipanga kumuua Mfalme Charles II kisha kumsimika ufalme Duke wa York ambaye alikuwa Mkatoliki.

Kutokana na uzushi huo, Bunge la England liliamua Wakatoliki wote waondoke kwenye ofisi za umma, vilevile walifanya jaribio la kutaka kumwondolea Duke wa York haki ya kurithi kiti cha Ufalme. Hali ilikuwa hivyo kwa sababu Mfalme Charles II na wabunge wengi walikuwa Anglikana.

Damu nzito kuliko maji

Mfalme Charles II alikataa mdogo wake kuondolewa kwenye haki ya kurithi ufalme, alipinga pia Wakatoliki kuondolewa kwenye ofisi za umma.

Hata baada ya uchunguzi kuthibitisha kuwa Titus alisema uongo chini ya kiapo, wabunge walisisitiza Wakatoliki waondolewe, hivyo ukatokea mgawanyiko mkubwa. Wabunge walisema wana haki zote za kuuagiza utawala, wakati Mfalme Charles II alisema, uamuzi wa wabunge ulikuwa unaingilia mamlaka ya ufalme.

Kutokana na hali hiyo, wananchi waligawanyika. Waliomuunga mkono Mfalme Charles II kuwa ufalme usiingiliwe, walijiita Tories, jina ambalo asili yake ni Wakatoliki walioteseka sana Ireland. Upande wa wabunge walijiita Whigs, ambalo ni msamiati wa zamani wa Scotland wenye maana ya kuipinga Serikali.

Kwa mvutano huo, kwamba ama mfalme ndiye awe na nguvu za kuamua katika ufalme wake bila kuingiliwa au wananchi kupitia wawakilishi wao, yaani wabunge ndiyo wawe na nguvu ya kumpangia mfalme, ndiyo mwanzo wa kuzaliwa kwa vyama vya kisiasa vya Whigs na Tories.

Tafsiri ya mfumo huo

Mpaka hapo utaona kuwa Whigs na Tories kama vyama vya kisiasa vya mwanzo kabisa duniani, asili yake ni kushindanisha mawazo ili kuona upande upi unakubaliwa zaidi. Kwamba je, wananchi wengi wapo kwa Mfalme au Bunge?

Hali hiyo utaiona pia katika Karne ya 18 mwishoni, wakati Rais wa kwanza wa Marekani, George Washington alipokuwa anaondoka madarakani. Vyama viwili vilianzishwa, kimoja kikitetea Serikali kujiamulia, kiliitwa Federalists. Hicho kilianzishwa na Alexander Hamilton.

Kingine kilichoanzishwa na Thomas Jefferson, kiliitwa Democratic-Republicans, chenye kutaka sauti ya umma iwe na nguvu kwenye vyombo vya uamuzi. Democratic-Republicans kilipitia nyakati za kugawanyika mara kadhaa mpaka kupata vyama viwili vilivyopo sasa, Democrats na Republican.

Kwamba ama Serikali ijiamulie au wananchi sauti zao ndiyo zisikike kupitia wawakilishi wao, huo ndiyo ukawa mwanzo wa vyama nchini Marekani.

Tafsiri ya uwepo wa vyama vya siasa kwa jumla ni kushindanisha sera zenye kulingana na maslahi ya watu na kuyaelekea. Chama chenye kuungwa mkono na wengi ndicho hupewa dhamana ya kuongoza dola.

Bunge na vyama

Bunge ni chombo cha uwakilishi wa wananchi na vyama vipo kwa ajili ya maslahi ya umma. Hivyo, wabunge wanapokuwa bungeni wanatakiwa kusukumwa zaidi kuzungumzia maslahi ya wananchi.

Bunge la Tanzania linakutanisha vyama vinne vya siasa kwa wakati huu, CCM, Chadema, CUF, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi. Kuwapo vyama hivyo ndani ya chombo hicho, ni rahisi kuamini kuwa maslahi ya umma yatamulikwa zaidi.

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti. Ndani ya Bunge, mijadala ya kutetea vyama imekuwa mikubwa na yenye kuchukua nafasi kuliko ambavyo inapaswa kuwa.

Kila chama kinaingiza misimamo ndani ya Bunge, badala ya kushikamana kuibana Serikali iweze kuwahudumia wananchi inavyotakiwa, kundi moja linaitetea Serikali, lingine linaishambulia tu.

Tabia hiyo inakwenda mpaka kwenye masuala mazito yenye kuhusu kupotea watu.

Ukifuatilia mijadala ya Bunge la Tanzania, ni rahisi kuona vikao vya vyama vina nguvu kuliko kusukuma maslahi ya umma. Vikao vya kambi za vyama, vina maamuzi makubwa kuliko sauti za wengi mitaani.

Hii ni dhambi ambayo inatendwa na vyama vyote. Bunge halipaswi kuwa hivyo, bali linatakiwa kuonekana likichakata na kukijenga kile ambacho kipo kwenye fikra za wananchi. Kinachozungumzwa bungeni, kinatakiwa kifanane na mawazo ya wananchi walio wengi.

Vyama vya siasa kucheza na siasa za Bunge kwa ajili ya kupitisha au kugomea mijadala kwa sababu tu za kisiasa na siyo sababu za umma, ni usaliti mkubwa kwa wananchi, vilevile ni kutoka nje ya mstari wa kuanzishwa kwake ambao ni maslahi ya umma.