CAF ilipoziachia timu za Cecafa

Muktasari:

  • Msimu uliopita wa 2017 ni watoza ushuru wa Uganda, KCCA pekee kutoka ukanda huu ambao waliingia kwenye hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika huku Yanga na wengine wakiishia kwenye mchujo.

Kwa mara ya kwanza baada ya kipindi kirefu, Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, umetoa timu nne ambazo zimetinga hatua ya makundi ya Michuano ya klabu Afrika.

Msimu uliopita wa 2017 ni watoza ushuru wa Uganda, KCCA pekee kutoka ukanda huu ambao waliingia kwenye hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika huku Yanga na wengine wakiishia kwenye mchujo.

Yanga ilitinga hatua ya makundi kwa mara ya mwisho, 2016 kabla ya msimu huu kwenye kombe la Shirikisho na kuwa wawakilishi pekee wa ukanda huu, kutinga hatua hiyo.

Msimu wa 2015 ulikuwa msimu mbaya zaidi kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni kwa timu za ukanda wa Afrika ya Mashariki ambazo zilishindwa kutinga makundi ya mashindano hayo ya kimataifa.

Orodha kamili ya timu kutoka ukanda huu ambazo zimetinga makundi ya Klabu Bingwa na Shirikisho ni KCCA (Uganda), Yanga (Tanzania) , Gor Mahia (Kenya) na Rayon Sports (Rwanda).

CAF imetangaza droo hiyo ambayo Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga imepangwa Kundi D pamoja na Gor Mahia ya Kenya, Rayon Sport ya Rwanda na USM Alger ya Algeria katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika droo iliyopangwa juzi Makao Makuu ya CAF, Cairo, Misri imeshudia kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki ikiwa na timu tatu na zote zimepangwa katika kundi mmoja pamoja na miamba ya Algeria.

Yanga kupangwa kundi hilo imetoa mwanya kwao iwapo watajipanga vizuri wanaweza kufuzu kwa robo fainali na hata kutinga fainali na kuweka historia mpya katika mashindano hayo.

Katika kundi A zimepangwa timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Raja Club Athletic ya Morocco, As Vita ya DR Congo na Aduana Stars FC ya Ghana.

Kundi B lina timu za RS Berkane ya Morocco, El Masry ya Misri, UD Songo (Msumbiji) na Al Hilal ya Sudan.

Katika Kundi C ni Enyimba FC ya Nigeria, Williams Ville (Ivory Coast), CARA Brazaville (Congo) na Djoliba AC ya Mali.

Ratiba inaonyesha Yanga itachezwa kati ya Mei 4-6, wakati mechi ya marudiano itachezwa Mei 15-16, kabla ya mapumziko ya kupisha Kombe la Dunia.

Michuano hiyo itaendelea Julai 27-29 na Agosti 17-19 na mechi ya makundi ya mwisho itachezwa Agosti 28-29.

Baada ya mechi za makundi kuisha droo ya robo fainali na nusu fainali ya Kombe la Shirikisho itapangwa Septemba 03.

Mechi ya kwanza ya robo fainali itachezwa Septemba 14-16 huku zile za marudiano ni Septemba 21-23, wakati mechi za nusu fainali ya kwanza itachezwa Oktoba 2-3 na ile za marudiano ni Oktoba 23-24 wakati fainali itachezwa Novemba 23-25, na marudiano itachezwa Novemba 30 au Desemba 2.

Spoti Mikiki inakuletea mchanganuo wa namna timu hizo zilivyopambana kutinga hatua hiyo ya makundi.

Yanga-Tanzania

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara,Yanga waliangukia kwenye Kombe la Shirikisho katika hatua ya mchujo baada ya kufungwa na Township Rollers kwenye mchujo wa kuwania kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa jumla ya mabao 2-1.

Baada ya Yanga kutolewa na Township Rollers ya Botswana, wakapangwa na Welaytta Dicha ya Ethiopia.

Mchezo wa kwanza baina ya Yanga na Welaytta Dicha ambao Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 , ulichezwa Uwanja wa Taifa jijini hapa, Aprili 7 huku ule wa marudiano uliofanyika, Awassa,Ethiopia Aprili 18, Yanga ilipoteza kwa bao 1-0.

Matokeo ya jumla ya mabao 2-1 ndio yaliyoifanya Yanga kuingia kwenye hatua ya makundi.

KCCA-Uganda

KCCA yenye maskani yake mjini, Kampala ndio timu pekee iliyotinga hatua ya makundi upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika huku wengine wakiwa kwenye Kombe la Shirikisho.

KCCA iliitoa Saint George ya Ethiopia kwa jumla ya bao 1-0, baada ya mchezo wa kwanza kutoka suluhu na kumalizia nyumbani kwa ushindi wa bao hilo.

Mabingwa hao watetezi wa Uganda, walianza kupigania nafasi hiyo ya kuingia makundi kwa kucheza hatua ya awali dhidi ya CNaPS Sport ya Madagascar na kuiondoa kwa faida ya bao la ugenini baada ya sare ya jumla ya mabao 2-2.

Gor Mahia-Kenya

Mabingwa wa Kenya, Gor Mahia walitumia nguvu za ziada kuiondoa SuperSport United ya Afrika Kusini, mchezo wa kwanza baina yao ulichezwa, Kenya na Gor Mahia ilianza kwa ushindi wa bao 1-0.

Gor Mahia ilicheza mchezo wa marudiano na SuperSport United na kufungwa mabao 2-1, lakini kilichowavusha hatua hiyo ya mchujo na kuingia makundi ni faida ya kupata bao la ugenini kutokana na matokeo kuwa jumla ya mabao 2-2.

Hata hivyo Gor Mahia anayoifundisha kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr iliiondoa Espérance de Tunis ya Tunisia kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa kama ilivyokuwa kwa Yanga kwa jumla ya bao 1-0, walilofungwa kwenye mchezo wa marudiano.

Rayon Sport-Rwanda

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ndio iliyoing’oa Rayon kwa jumla ya mabao 2-0 kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho.

Mara baada ya kuangukia kwenye shirikisho walipangwa na Costa do Sol ya Msumbiji, mchezo wa kwanza kwenye hatua hiyo ya mchujo, Rayon iliifunga Costa do Sol mabao 3-0 na kwenye mchezo wa marudiano wakamalizia kwa ushindi mwingine wa mabao 2-0.

Rayon Sport ambao ni mabingwa watetezi wa Rwanda ndiyo timu pekee kutoka Ukanda Afrika Mashariki na Kati iliyotinga hatua hiyo ya makundi kwa ushindi mnono zaidi wa jumla ya mabao 5-0.