CAG amebainisha ukosefu wa wataalamu, ukiukaji sheria

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,Profesa Musa  Assad (aliyeshika kalamu) akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha ripoti yake ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30,2017 bungeni mjini Dodoma hivi karibuni.Picha na Maktaba.

Muktasari:

  • Kwenye ukaguzi wa Serikali na taasisi zake, CAG Profesa Mussa Assad anasema alifika katika ofisi 241 ingawa ni 237 ndizo alizitolea maoni.

Ingawa mengi yamebainishwa na kuelekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwenye ripoti yake ya mwaka 2016/17, kutofahamika matumizi ya Sh1.5 trilioni kumewashtua wadau wengi.

Kwenye ukaguzi wa Serikali na taasisi zake, CAG Profesa Mussa Assad anasema alifika katika ofisi 241 ingawa ni 237 ndizo alizitolea maoni.

Kati ya alizozikagua kuna ofisi za wizara 65,  39 za ubalozi, taasisi nyinginezo 38 na wakala 35. Kulikuwa na sekretarieti 26 za mikoa, mifuko  maalumu 17, bodi na wakala wa maji 13 na vyama kumi vya siasa.

Matokeo ya ukaguzi huo yalikuwa hati mbaya saba, zisizoridhisha nne na zenye mashaka 22 wakati zinazoridhisha zilikuwa 204.

Kwa miaka mitatu iliyopita, taasisi zilizokaguliwa zimeongezeka kutoka 199 za mwaka 2014/15 mpaka 244 mwaka 2016/17.

Mjadala wa Sh1.5 trilioni unatokana na maelezo aliyoyatoa CAG alipokagua usimamizi na utekelezaji wa bajeti ya mwaka huo ya Sh29.5 trilioni.

Mkaguzi huyo anasema katika bajeti hiyo, Sh18 trilioni zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida Sh17.2 trilioni zilitumika na kati ya Sh11.4 trilioni zilizoidhinishwa kufanikisha miradi ya maendeleo, Sh6.4 trilioni zilitolewa.

Kwa miezi yote 12, CAG anasema jumla ya Sh23.79 trilioni zilitolewa na kutumika ingawa Serikali ilikusanya Sh25.3 trilioni ikiwa chini kwa asilimia 14.3 ya kukusanya kiasi kilichokusudiwa baada ya kuzikosa Sh4.2 trilioni.

 

Mapendekezo

Upo upungufu mwingi uliogunduliwa na CAG ambaye anasema kutofanyiwa kazi kwa mapendekezo anayoyatoa kila mwaka ni miongoni mwa sababu za kujirudia kwa baadhi ya makosa ya kiutendaji.

Anasema ili kuwa na uwazi, uwajibikaji, utawala bora, usimamizi na kufuata sheria na kanuni kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali za umma, ni muhimu kutekeleza mapendekezo yake na maelekezo ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kulifanya jukumu la CAG na uwajibikaji kwa PAC kuwa na maana.

CAG ameshauri kuanzishwa kwa vitengo imara vya ukaguzi vitavyokuwa na wataalamu ili kutekeleza mapendekezo na maelekezo anayoyatoa pamoja na yale ya PAC.  “Hii iendane na kuimarishwa kwa mifumo ya udhibiti wa ndani ambao huchangia udhaifu  katika usimamizi,"ameshauri CAG.

Tangu ripoti itoke na kuwasilishwa bungeni, mawaziri kadhaa wamechukua hatua kwa maeneo yaliyo chini ya mamlaka zao baada ya Rais John Magufuli kuonyesha mfano alipoipokea awali, ambapo aliwawajibisha wakurugenzi wa halmashauri za Kigoma, Kigoma Ujiji na Pangani zilizopata hati chafu.

Kwenye taarifa yake, Profesa Assad anasema kati ya maoni 85 yaliyotolewa katika ripoti ya mwaka 2015/15 ni 14 (sawa na asilimia 16.5) yaliyofanyiwa kazi wakati 51 (sawa na asilimia 60) yanaendelea kutekelezwa, tisa ambayo ni asilimia 10.6 hayajafanyiwa kazi na 11 (sawa na asilimia 12.9) yalipitwa na wakati.

Hata hivyo, CAG ameendelea kutoa mapendekezo ya jumla yanayohitaji kushughulikiwa na Serikali, Bunge na menejimenti za taasisi za Serikali.

Mapendekezo hayo yametokana na taarifa zilizowasilishwa wakati wa ukaguzi na masuala mengine muhimu ambayo umma unapaswa kuyafahamu.

Mikopo

Ingawa makusanyo ya ndani yameonyesha mwenendo mzuri kwa miaka minne mfululizo, mkaguzi huyo anasema Serikali imekusanya asilimia 62.50 ya Sh29.5 trilioni zilizoidhinishwa mwaka 2016/17 wakati ilikusanya asilimia 62.58 ya Sh22.49 trilioni za mwaka 2015/16.

Makusanyo yameendelea kuwa sawa licha ya hatua zilizochukuliwa na Serikali kuongeza vyanzo vya mapato hasa ya kodi.

Anasema katika utoaji leseni kwa migodi iliyopo Mwanza, Kahama na Shinyanga kuna upungufu wa usimamizi kwa kuwa zipo kampuni zinachenjua madini bila kuwa na leseni, hivyo kuikosesha Serikali Dola 104,400 za Kimarekani (zaidi ya Sh231.6 milioni) kwa mwaka.

Hamasa ya Rais Magufuli kuzitaka ofisi za ubalozi kuimarisha diplomasia ya uchumi imeshuhudia zaidi ya Sh14.5 bilioni zikikusanywa kwenye ofisi 21, lakini mapato hayo hayakuhamishiwa Hazina, hivyo kuinyima Serikali fursa ya kuzitumia huku kukiwa na ushawishi wa kutumika vibaya.

Mikopo ya ndani

Kukopa kutoka vyanzo vya ndani kuna athari kubwa kwenye uchumi. Serikali hutakiwa kulipa riba na kuathiri kiwango cha kuikopesha sekta binafsi kwa benki za biashara.

Katika mwaka huo wa ukaguzi, Serikali imekopa ndani kwa asilimia 10.08 zaidi ya bajeti iliyopitishwa na inatakiwa kulipa riba ya asilimia 11.51 kwa amana za muda mfupi na asilimia 30.25 kwa zile za muda mrefu.

Anasema deni la nje huathiriwa na kiwango cha ubadilishaji wa fedha, hivyo kutahadharisha kuwa kugharamia bajeti kwa kutumia mikopo ni ghali.

“Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato, iingie ubia na sekta binafsi kupunguza gharama za utekelezaji wa bajeti kwa kutumia mikopo na misaada,” anashauri Profesa Assad.

Pamoja na hayo, anapendekeza shughuli nyingi za maendeleo zifanywe kwa ubia na sekta binafsi kwa ajili ya kuchochea ajira na kuongeza ubora wa maisha.

Deni la Taifa

Mkaguzi anasema upungufu mwingi uliojitokeza umejirudia kuashiria kutokuwapo umakini kwa Serikali kutekeleza mapendekezo anayoyatoa.

Upungufu kwenye Deni la Taifa unasababishwa na kukosekana kwa muundo imara wa kufuatilia mambo yanayojumuisha kushushwa kwa kiwango cha deni na kutoongezeka kwa dhamana za Serikali katika soko la mtaji.

Sababu nyingine ni kutopokelewa kwa mikopo husika licha ya kusaini mikataba, upungufu katika kuingiza kumbukumbu za kupokea mikopo na usimamizi usioridhisha wa mikataba ya mikopo iliyofaulishwa.

Kwa kuzingatia hayo, CAG ameitaka Serikali kuweka utaratibu wa kufuatilia na kutathmini matumizi ya fedha zitokanazo na Deni la Taifa ambalo mpaka Juni, 2017 lilikuwa Sh46 trilioni na kupata uhakika wa kupokewa kwa fedha kabla ya kuingiza kumbukumbu zake.

Anaitaka Serikali kuanzisha ofisi ya pamoja ya kusimamia Deni la Taifa.

Rasilimali watu

Wizara na idara za Serikali zikiwamo ofisi za ubalozi zimeendelea kuwa na upungufu kwenye usimamizi wa rasilimali watu na mishahara.

Upungufu uliojirudia upo kwenye usimamizi wa mishahara, malipo kwa kwa wafanyakazi waliostaafu na kutokuwa na tathmini ya utendaji wa watumishi hao.

Vilevile, kuna ucheleweshaji wa makato ya mishahara kwenda mifuko husika, mishahara chini ya kiwango kinachokubalika kisheria, upungufu wa watumishi kwenye taasisi nyingi na kutofanyika kwa mikutano ya mabaraza ya wafanyakazi.

Utegemezi wa wakala

Kwa muda mrefu, wakala wa umma umeendelea kutegemea fedha za Serikali kujiendesha. CAG anashauri wakala kuboresha huduma, kuangalia upya tozo wanazotoza, kutumia njia za kisasa kibiashara, kubuni vyanzo vya mapato ili kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka serikalini.

Udhaifu wa ununuzi

CAG anasema licha ya kuwapo kwa sheria, baadhi ya wizara, sekretarieti za mikoa na ofisi za ubalozi haziizingatii kikamilifu.

Anaeleza kuwa kuna ununuzi ulifanyika bila kuidhinishwa na bodi na ikabainika kazi zimefanyika, bidhaa zimenunuliwa na huduma kutolewa bila ya kuwapo mkataba wa aina yoyote kati ya taasisi na wazabuni au wakandarasi.

Pia, imebainika kufanyika kwa malipo ya kazi, huduma na bidhaa mbalimbali kabla ya utekelezaji huku kukiwapo bidhaa na huduma zilizopokewa lakini hazikukaguliwa na kamati ya ununuzi wakati baadhi ya huduma na bidhaa zilinunuliwa kutoka kwa wazabuni wasiojasajiliwa.

Imebanika, baadhi ya mikataba na miradi haikutekelezwa vizuri huku kukiwa na miradi iliyochelewa kukamilika na kuleta mashaka ya bei kubadilika. Kulikuwapo ununuzi uliofanywa kwa fedha taslimu na nje ya mpango wa mwaka.

“Ununuzi wa umma ni nguzo muhimu katika utoaji huduma serikalini kwani hutumia kiasi kikubwa cha fedha, hivyo usimamizi wake unahitajika kukuza ufanisi. Matukio mengi yaliyopita yalibaini ununuzi ndiyo eneo hatarishi kwa rushwa na ufujaji wa fedha,” anatahadhalisha Profesa Assad.