CCM ifanyie mabadiliko suala la kofia mbili

Muktasari:

Huo ndiyo utaratibu wa kawaida wa CCM kubadilisha nafasi ya uenyekiti kwa kila rais mpya anapoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu licha ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho anakuwa bado hajatimiza muda wake wa kukaa madarakani.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Jumamosi hii kitafanya Mkutano Mkuu Maalumu mjini Dodoma ukiwa na lengo kuu la kumkabidhi uenyekiti wa chama hicho Rais John Magufuli kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Kikwete.

Huo ndiyo utaratibu wa kawaida wa CCM kubadilisha nafasi ya uenyekiti kwa kila rais mpya anapoingia madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu licha ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho anakuwa bado hajatimiza muda wake wa kukaa madarakani.

Utaratibu huo unamfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mbali na kuwa Ikulu kuwa na kofia ya pili ya kuwa mwenyekiti wa chama hicho kinachotawala tangu Tanzania ipate uhuru.

CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 baada ya uamuzi wa kuviunganisha vyama vya siasa vya Tanu kilichokuwa kinatawala Tanzania Bara na Afro Shirazi Party (ASP) kilichokuwa kinaongoza Zanzibar.

Uamuzi huo ulifanywa wakati Tanu ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere na ASP ikiwa chini ya Aboud Jumbe Mwinyi na kuendelea kuitawala Tanzania wakati wa mfumo wa chama kimoja na hadi Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995.

Kofia mbili zitenganishwe

Linaonekana ni jambo la kawaida kwa CCM kuziunganisha kofia mbili za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya mwenyekiti wa chama hicho, lakini kuna haja ya kufikiria upya juu ya suala hilo.

Pamoja na kwamba hali halisi inaonyesha kuwa mkutano mkuu maalumu wa CCM kwa mazingira yaliyozoeleka hautaangalia suala la kuzitenganisha kofia mbili, lakini muda wa kufikiria hivyo umewadia.

Kuna umuhimu kwa ustawi wa Taifa na ustawi wa CCM na mwelekeo wa kuwa na utawala bora zaidi kofia hizo mbili zikatenganishwa ili Rais akabaki na shughuli zake za kusimamia Ikulu na mtu mwingine akawa na majukumu ya kusimamia CCM.

Pamoja na kwamba jambo hilo halijazoeleka, lakini ukweli ni kuwa linaweza kuwa na manufaa kwa vile katika historia ya Tanzania na jinsi wanasiasa walivyojengwa katika nchi hii hakuna siku ambayo itatokea watu hawa wawili wakatofautiana.

Faida kubwa ya kutenganisha kofia mbili itampa nafasi mwenyekiti wa CCM kuwa msimamizi na mshauri wa karibu wa Rais na kumwelekeza pale atakuwa hakwenda katika njia iliyonyooka.

Hata hivyo, ni wazi kwamba kofia mbili zikivaliwa na mtu mmoja kama ambavyo ilivyokuwa imezoeleka kunafanya awe hawajibiki kwa yeyote yule na kama atataka kuzitumia vibaya nafasi hizo anao uwezo wa kuivuruga nchi.

Itaongeza utendaji wa Rais

Iwapo Rais hatakuwa mwenyekiti wa chama itamfanya asijikite zaidi katika siasa hali ambayo itamwongezea nguvu na kutumia muda wake wote katika shughuli za Serikali na kwa hiyo kuongeza ufanisi.

Rais akiwa na kazi mbili kwa hali yoyote ile atalazimika kupanda farasi wawili na kuna sehemu anaweza asitende haki inavyotakiwa.

Kwa hiyo, kuna haja kwa Rais Magufuli kutokana na ari ya utendaji wake aliyoionyesha tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015 aachiwe aendelee kutumbua majipu Ikulu huku wakiwa na mipango ya kujenga uchumi wa Tanzania.

Hii ni fikra mpya ambayo inafaa wana CCM watakaokutana katika mkutano huo waipe nafasi ya kuijadili kabla ya kutekeleza wajibu wa kumkabidhi kiti cha uenyekiti wa CCM Rais Magufuli.

Inawezekana ikaonekana ni suala gumu, lakini siku zote mabadiliko siyo kitu chepesi na kina hitaji ujasiri kukifanya, ukiamua matokeo yake yanaweza yakawa mazuri.

Huu ndiyo muda mwafaka

Hakuna muda wowote mwingine mwafaka kwa CCM kuweza kuzitenganisha kofia mbili za urais na uenyekiti wa chama hicho kama muda huu Ikulu yupo Rais Magufuli.

Rais Magufuli amelipambanua kuwa ana dhamira ya kutekeleza mambo makubwa kwa ajili ya kuwaletea maendeleo Watanzania kwa hiyo lingekuwa jambo la busara kupewa muda zaidi wa kutekeleza azma hiyo.

Ili kumpa nafasi hiyo ni kutompa nafasi ya uenyekiti wa CCM ambayo nayo ina shughuli nyingi za kukisimamia chama hicho ambacho katika hali ya sasa kinahitaji usimamizi wa karibu ili kurudisha hadhi yake.

Pamoja na kwamba CCM imerudi madarakani kwa upande wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar, lakini chama hicho kinakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa vyama vya upinzani ambao unawalazimisha kufanya mageuzi katika chama chao.

Kwa upande wa Zanzibar hivi sasa kuna mpasuko wa kisiasa baada ya Chama cha Wananchi (CUF) kudai kwamba ilishinda Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015, lakini iliporwa madaraka.

Uchaguzi huo ulifutwa na mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha Oktoba 28 siku ambayo alipaswa kutangaza matokeo ya urais na kulazimika kufanyika kwa uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 mwaka huu na kususiwa na CUF na kuipa ushindi CCM.

Katika mazingira hayo CCM ingepata mtu tofauti wa kuisimamia ili ikasahihisha mambo yake badala ya Rais ambaye ana mambo mengi ya kusimamia Serikali na kutekeleza azma yake ya kujenga Tanzania ya viwanda.

Mkutano wa CCM ubadili ajenda

Ili kutoa uamuzi wa kuzitenganisha kofia mbili za urais na uenyekiti wa CCM, mkutano mkuu maalumu unalazimika kubadili ajenda ya kumkabidhi uenyekiti wa chama hicho Rais Magufuli.

Wajumbe wa mkutano huo wanapaswa kujadili muelekeo mpya wa kuzitenganisha kofia hizo na kumruhusu mwenyekiti wa sasa, Kikwete aendelee kushika wadhifa huo hadi muda wake wa miaka mitano utakapomalizika.

Baada ya hapo wajumbe wa mkutano ndiyo wanaweza kuamua kama Kikwete aendelee kuwa mwenyekiti wa chama hicho au achaguliwe mwenyekiti mpya ambaye kwa namna yoyote ile hatakuwa Rais Magufuli.

Kwa sababu ya mazoea jambo hili linaweza kuonekana kuwa gumu, lakini kama litafanywa lina nafasi ya kuleta changamoto mpya zenye mwelekeo wa kuleta mafanikio katika Tanzania.

Ni dhahiri kwamba wanachama wa CCM watakaokutana mkutanoni wanatakiwa kujikita katika kufikiria kuzitenganisha kofia mbili na kuanzisha utaratibu mpya kwa kuiongoza Tanzania.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatikana kwa barua pepe: [email protected]