CCM imeamua kuvunja misingi ilioyoipa thamani

Muktasari:

Katika kipengele hicho, Dk Johnson anaeleza jinsi ambavyo wanasiasa waliopo madarakani wanavyoweza kuandaa matukio na mazingira ya muda mfupi kuupamba uchumi kupitia sera ya udhibiti wa mzunguko wa fedha, vilevile makusanyo ya kodi za Serikali na matumizi yake. Kuonyesha kuwa vitu vipo sawa au vinakwenda vizuri.

Dk Paul Johnson wa Chuo Kikuu cha Auburn, Marekani, kupitia mafundisho yake aliyoyapa jina, A Glossary of Political Economy Terms, ndani yake kuna kipengele alichokiita Mzunguko wa Biashara za Siasa, unafuu wa maonyesho ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya mtaji wa kisiasa.

Katika kipengele hicho, Dk Johnson anaeleza jinsi ambavyo wanasiasa waliopo madarakani wanavyoweza kuandaa matukio na mazingira ya muda mfupi kuupamba uchumi kupitia sera ya udhibiti wa mzunguko wa fedha, vilevile makusanyo ya kodi za Serikali na matumizi yake. Kuonyesha kuwa vitu vipo sawa au vinakwenda vizuri.

Naomba ninukuu aya hii ya Dk Johnson kama alivyoiandika kwa Kiingereza: “Politicians tend to ‘bite the bullet’ and reverse course by raising taxes, cutting spending, slowing the growth of the money supply, allowing interest rates to rise.”

Kwa tafsiri yangu, anasema, “Wanasiasa huweza kuyapamba mambo kinyume na ukweli na kupindisha sababu halisi kwa kuongeza kodi, kukata matumizi, kupunguza kasi ya ukuaji wa fedha na kuruhusu viwango vya riba kuongezeka.

Kwa maneno “bite the bullet”, Dk Johnson anamaanisha kuficha maumivu au hali isiyopendeza ambayo inaonekana haiepukiki. Mwandishi Rudyard Kipling katika kitabu chake cha riwaya, The Light that Failed cha mwaka 1891, ndiye alikuwa wa kwanza kutumia maneno hayo.

Mwaka 1975, ilichezwa sinema yenye jina ‘Bite the Bullet’ ambayo ilifikisha tafsiri ya kufanya jambo kwa kufichaficha ukweli kwa muda mfupi. Mathalan, una kovu, lakini unapaka ‘make-up’ ili lisionekane kwenye macho ya watu, ingawa kiuhalisia kovu linabaki palepale. Jino limeoza, linauma na ile sehemu iliyooza inajazwa. Baadaye maumivu hurejea yakiwa makali zaidi.

Huo utaratibu wa kuficha tatizo kwa kuweka pambo la muda mfupi, ni janga linaloinyemelea CCM kwa sasa. Kufanya maonesho ya wanasiasa wanaohama kutoka vyama vya upinzani. Kuwapa upendeleo wageni kuliko wenyeji.

Misingi inayovunjwa

CCM imekuwa chama cha kupokea mgeni kutoka upinzani kisha kinamsimamisha kugombea nafasi ya uongozi bila hata kumpima kwa kura za maoni. Mtindo ambao vyama vya upinzani vimekuwa vikiutumia muda mrefu kuvizia wana-CCM wanaokosa nafasi au wanaojiondoa kwa sababu mbalimbali, eti nacho kimeuiga.

Vyama vya upinzani ndivyo ambavyo vimekuwa vikisimamisha wagombea urais na wabunge ambao wamenyimwa nafasi au waliohama CCM. Chadema kinaye Edward Lowassa, bila kupepesa macho ni wazi alikosa nafasi CCM ndiyo maana akahamia upinzani ili kutafuta fursa ya kugombea urais na akaipata.

Augustine Mrema alikuwa mgombea mwenye nguvu zaidi mwaka 1995. Aligombea kupitia NCCR-Mageuzi baada ya kutoka CCM. Rekodi zinaonesha wapinzani hupata kura zaidi wanaposimamisha wagombea wanaotoka CCM.

Mwaka 1995, Mrema alipata kura asilimia 28 na mwaka 2015, Lowassa aliupandisha hadhi upinzani kwenye mbio za urais alipopata asilimia 39.97. Mgombea pekee ambaye alikuwa upinzani kwa muda mrefu na kupata matokeo mazuri ni Dk Willibrod Slaa aliyegombea kupitia Chadema mwaka 2010 na kupata asilimia 27.

Ni wazi tafsiri ya upinzani inajipambanua dhahiri kwamba wanasiasa wa CCM wana nguvu zaidi, ndiyo maana huwapokea kwa mikono miwili na kuwapa nafasi ya kugombea kwa matumaini na mbwembwe nyingi. Hili CCM walitakiwa kulipokea kwa heshima, hivyo kuendelea kujiheshimu.

Said Arfi alikuwa mbunge wa Mpanda kuanzia mwaka 2005 mpaka 2010. Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, jimbo hilo liligawanywa mara mbili na Arfi aligombea na kushinda Mpanda Mjini. Mwaka 2015, Arfi alihamia CCM, lakini aliposhiriki kura za maoni ili agombee kulitetea jimbo hilo alishindwa.

Kushindwa kwa Arfi katika kura za maoni CCM kulionyesha tofauti kati ya chama hicho na vyama vya upinzani. Asilimia kubwa ya wana-CCM waliohamia upinzani walipata fursa ya kugombea ubunge, wakati Arfi ambaye alikuwa kigogo wa upinzani, aliyetoka kuwa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara Chadema aliangushwa.

CCM wameamua kuipoteza heshima hii ya kujipambanua kuwa chama cha wanachama. Chama ambacho kila mwanachama anajiona yupo huru kushiriki uchaguzi. CCM haikuwa chama cha kupendelea wageni wala kuwapapatikia. Hata hivyo, haikuwa ikiwanyima fursa wageni. Hii ndiyo misingi yake.

CCM ni chama ambacho msingi wa wagombea nafasi za uongozi upo kwenye kura za maoni. Wanachama katika kata au jimbo hawapangiwi mgombea, isipokuwa hupiga kura za maoni, kisha mamlaka za juu huketi kupitia mchakato wa kura za maoni kama ulikuwa huru na haki.

Upigaji kura za maoni CCM, umefungwa kama haki ya kikatiba. Katiba ya chama hicho ibara ya 14 inazungumzia haki za mwanachama, ibara ndogo inasema ni haki kwa mwanachama kupiga kura ya maoni.

Ibara hiyo kwa ukamilifu wake kama ilivyoandikwa, inasema: “Mwanachama yeyote wa CCM atakuwa na haki ya kupiga kura yake ya maoni kwa wagombea wa CCM wa nafasi za udiwani wa kata/wadi, ubunge na uwakilishi wa jimbo kwa kufuata masharti ya Kanuni za CCM.”

Ieleweke kuwa jambo lolote likishatamkwa ni haki ya mtu, likiondolewa au kunyimwa, maana yake mtu husika amenyimwa haki yake. Ikishaitwa haki, maana yake ni stahili ya mtu. Sasa Katiba ya CCM imeandikwa ni haki ya mwanachama kupiga kura ya maoni. Hivyo, akinyimwa haki hiyo, anakuwa hajatendewa haki. Na Katiba inakuwa imevunjwa.

Walichokosea CCM

Desemba mwaka jana, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Maulid Mtulia (CUF) na Dk Godwin Ole Mollel, Siha (Chadema), walijiuzulu ubunge kisha kutangaza kujiunga CCM kwa hoja kuwa walifanya hivyo ili kuunga mkono jitihada za Rais John Magufuli. Habari za kuhama kwao ziliibua mjadala mkubwa.

Chadema na CUF walidai, japo bila ushahidi, kuwa wabunge hao walishawishiwa kwa ahadi mbalimbali ikiwa kusimamishwa kugombea majimbo katika hayohayo kupitia CCM, na chama kingefanya juu chini kuwarejesha bungeni. Hili pia halikuwa na ushahidi lakini limetokea.

Kitendo cha Mtulia na Dk Mollel kuteuliwa na Kamati Kuu (CC) CCM, kugombea tena majimbo hayo katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 17, mwaka huu, kinaleta tafakuri ya aina tatu; mosi ni wana-CCM wa Kinondoni na Siha wamenyimwa haki ya kupiga kura za maoni.

Pili ni CCM imeanza kupokea wageni na kuwasimamisha kugombea nafasi za uongozi bila kuwapima na wanachama wengine ili kujiridhisha kukubalika kwao kwa wana-CCM wa majimbo husika. Tatu ni kukaribisha hali ya kuamini yaliyovumishwa na wapinzani, japo hawakuwa na ushahidi.

Mazingira ya uteuzi, kujivua kwao ubunge na jinsi wanachama wa CCM walivyonyimwa fursa za kujipima nao ubavu na kuondolewa haki ya kupiga kura za maoni, yanaleta uhai wa kimazingira kuhusiana na hoja ya wapinzani. Si bure mbunge kuacha ubunge hivihivi, kwa hoja ya kutaka kumshabikia Rais Magufuli anavyofanya kazi.

Kwa nini wana-CCM wa Siha na Kinondoni wanyimwe haki ya kupiga kura za maoni ili wamchague wanayedhani anawafaa? Kwa nini Mtulia na Dk Mollel wapendelewe? Ni kwa nini wanachama wengine waliokuwa na nia ya kugombea majimbo hayo, wamenyimwa haki kisha Kamati Kuu kuchukua uamuzi wa jumla?

Tukumbuke tukio la mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari, alipotoa video alizorekodi kuonyesha kile alichokiita ni madiwani wa Chadema walivyonunuliwa Arusha na jinsi Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilivyoshughulikia ushahidi huo.

Hata hivyo, haisahauliki kwamba miongoni mwa yaliyozungumzwa ni kwamba madiwani husika waliahidiwa kurejeshwa kwenye kata zao kupitia CCM. Na kilichotokea ni madiwani hao kutokeza kugombea kura za maoni CCM na kushindwa lakini waliteuliwa kuwa wagombea na sasa ni madiwani.

Matukio hayo ndiyo ambayo yanafanya ionekane CCM inaficha kovu kwa urembo wa juu. Kimeanza kuacha misingi yake. Kamati Kuu inachukua uamuzi kuteua wagombea bila kushirikisha wanachama wa majimbo husika. Wageni wameanza kupendelewa na kupapatikiwa kuliko wenyeji. Chama kinafanya uamuzi unaoshabihiana na tuhuma za wapinzani.