CCM mpya ya JPM, yafyeka watu maarufu mikutano saba yafanyika ndani ya siku 11

Muktasari:

  • Miaka ya nyuma vikao vya taifa ya jumuiya za CCM, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ratiba za vikao vyao zilitofautiana kwa takriban mwezi mzima, lakini kwa mara kwanza vikao hivyo vimefuatana mfululizo na vikao vya chama Taifa kwa kufanyika ndani ya siku 11.

Wakati CCM ikielekea kuadhimisha miaka 40 tangu ilipozaliwa Februari 5, 1977, Mwenyekiti wake wa Taifa wa tano, John Magufuli ameweka rekodi kwa kuwezesha vikao vya jumuiya zake na vikao vya chama Taifa kufanyika kwa kufuata mfululizo ndani ya siku 11 huku wagombea wa nafasi mbalimbali kutojulikana na wengi ni wapya ambao hawana umaarufu wa kisiasa.

Miaka ya nyuma vikao vya taifa ya jumuiya za CCM, Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Jumuiya ya Wazazi na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ratiba za vikao vyao zilitofautiana kwa takriban mwezi mzima, lakini kwa mara kwanza vikao hivyo vimefuatana mfululizo na vikao vya chama Taifa kwa kufanyika ndani ya siku 11.

Pia, miaka ya nyuma wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho walikuwa watu maarufu katika jamii, walijitangaza sana wakati wa kuchukua fomu za kugombea, kampeni na hata wakati wa uchaguzi. CCM iliyopita nafasi za ujumbe wa mikutano ya ngazi mbalimbali ziligombewa na mawaziri, madiwani, wabunge, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya,wake za viongozi na watoto wao.

Mbwembwe zilizo zoeleka Dodoma hazijaonekana tangu kuanza vikao vya kitaifa vya jumuiya ambapo Desemba 8-9 ulifanyika mkutano wa UWT, Desemba 10-11 mkutano wa UVCCM na Wazazi walianza mkutano wao jana na unamalizika leo. Vikao vya chama Taifa vitaanza Desemba 14 na kumalizika Desemba 19 kwa kikao cha siku mbili cha mkutano mkuu wa CCM Taifa.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) kilichofanyika Desemba 2016 jijini Dar es Salaam ndicho kilichoifumua CCM kwa kufanya mabadiliko ya 16 ya Katiba yake ya mwaka 1977 iliyopitishwa na mkutano mkuu uliofanyika Machi 12, 2017 mjini Dodoma.

Katika Mabadiliko hayo, kuanzia sasa, idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho itapungua kutoka idadi ya wajumbe 388 hadi wajumbe 158, huku idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu, (CC), wamepungua kutoka idadi ya wajumbe 34 hadi 24.

Aidha katika mabadiliko hayo, kiongozi wa CCM hataruhusiwa kuwa na vyeo zaidi ya kimoja vya utendaji wa siku hadi siku. Hivyo, CCM itakayoanza baada ya Desemba 20 itakuwa imekamilisha mabadiliko ya 16 ya Katiba yake.

Dodoma iliyokuwa ikitamba kwa wingi wa wageni wakati wa vikao vya CCM hadi wageni wengine kukosa nafasi kwenye nyumba za kulala wageni, safar hii imekuwa tofauti tangu kuanza kwa kikao cha UWT kikafuatiwa na kile cha UVCCM na cha Wazazi kinachomalizika leo.

Huku viongozi wote wakuu wakiwa mjini Dodoma wakiwamo wastaafu, mkutano wa UWT ulimalizika kwa kumchagua Gaudentia Kabaka kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo, wakati UVCCM mwenyekiti alichaguliwa Kheri James.

Lakini, chaguzi hizi zimekuwa tofauti na chaguzi zilizotangulia ambazo zilifanya mji wa Dodoma kujaa wapambe ambao ni wapiga kampeni wa wagombea kutoka katika mitandao ambayo wagombea wanakuwa wamejitengenezea miaka mitano iliyopita.

Hatua hii ilifanya mji wa Dodoma kufurika na hata wakati mwingine wageni kukosa vyumba vya kulala kutokana na wingi wa wapambe wanaofika kuwapigia wagombea wake.

Hata shamrashamra za uchaguzi na upokeaji wa matokeo yake zimekuwa tofauti na chaguzi nyingine ndani ya chama hicho tawala, badala yake watu kutumia mitandao ya jamii kwa kiasi kikubwa kuwauza wagombea wao.

Pia, katika uchaguzi UVCCM kumekuwa na idadi kubwa ya wanachama waliojitokeza katika kuwania nafasi za uongozi tofauti na miaka ya nyuma, ambapo katika nafasi ya uenyekiti watu waliomba nafasi hiyo walikuwa 113 na saba ndio waliopitishwa na Nec kugombea nafasi hiyo.

Hata hivyo, hotuba za Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli alizozitoa kwa nyakato tofauti wakati wa vikao vya jumuiya hizo zinaonyesha kuchangia kuwabadilisha wajumbe wa mikutano hiyo wanaoishi kwa mazoea kwa kuanika udhaifu wao hadharani kinagaubaga.

Mfano halisi ni pale alipokuwa akifungua mkutano wa uchaguzi wa UWT, Rais Magufuli anasema kama kutakuwepo na ikadhihirika kuwa amepita kwa mchezo mchafu Kamati Kuu ya chama hicho itakaa na wataamua kufuta matokeo ya uchaguzi na kuchukua hatua za nidhamu.

Anasisitiza kuwa anataka viongozi watakaomsaidia katika chama chao ambao hawajapita kwa rushwa ili wamsaidie kuchagua viongozi wasiotokana na rushwa.

INAENDELEA UK 20

INATOKA UK 17

“UWT iliyokuwa ya kina Sofia Kawawa sio UWT tuliyonayo sasa. Na mimi siwezi kuwaficha lazima nilipasue jipu moja kwa moja hapa,”anasema na kuongeza kuwa mwanachama aliyekuwa anataka uongozi ndani ya jumuiya hiyo ni lazima atafute kiongozi wa kumbeba.

Maneno kama hayo aliyarudia tena wakati wa ufunguzi wa uchaguzi wa UVCCM kwamba jumuiya hiyo imegubikwa na vitendo vya rushwa na ndio maana hawakupendekeza majina yanayomfanya kufanya uteuzi.

“Nitashangaa kama mkiniletea mwenyekiti aliyewahonga. Kuwahonga ni kuwamaliza thamani yenu. Kukupa hela ili umchague amekudharau na hii ni dalili ya mwanzo kuwa huyu mtu hatakuwa kiongozi mzuri,”anasema.

Wana CCM wazungumza

Katibu wa Mwenezi wa CCM Mkoa wa Dodoma aliyemaliza muda wake, Donald Mejitii, anasema tofauti anayoiona ni nyakati za nyuma kulikuwa na hekaheka za makundi makubwa ambayo yalikuwa yakipingana.

“Makundi haya yalikuwa yakianza kutengeneza mtandao kabla ya uchaguzi na hapo kulikuwa na matumizi makubwa ya fedha katika hilo,”anasema.

Hata hivyo, anasema katika uchaguzi wa mwaka huu ndani ya chama kumekuwa na ukemeaji mkubwa wa masuala ya rushwa kulikofanywa na Mwenyekiti wa chama Taifa, jambo ambalo limefanya hakuna aliyeteuliwa ambaye amevuma bali wengi wao waliibukia baada ya kuteuliwa na vikao vya chama.

“Zamani nguvu za pesa ilikuwa inatumika kwa muda mrefu wazi lakini sasa hivi wamechaguliwa watu ambao hatukuwa tumewasikia kwamba wanajiandaa. Tumeona wanaibukia badaa ya kuteuliwa na vikao vya chama,”anasema.

Anasema uchaguzi wa mwaka huu umefanyika bila wengi wao kutumia nguvu za fedha wenye fedha na jambo kubwa lililokuwa likiangaliwa ni watu wenye sifa.

Mejitii anasema suala hilo limefanya kuleta sura mpya katika uongozi ambazo hazijulika kabisa ili mradi tu walikidhi kanuni tofauti na chaguzi zilizotangulia ambazo ni lazima uwe unafahamika.

“Aina hii inatoa fursa kwa wengi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.Mazingira ya rushwa yamepungua, watu hawatoi rushwa hadharani, hata kama yapo ni mmoja mmoja tena kwa kificho. Mwenyekiti wa Taifa (Dk Magufuli) ameonyesha ukali sana kwenye rushwa na wasaidizi wake wamemfuata,”anasema.

Mejitii anasema mfumo huo utasaidia chama kukua ingawa hofu yake ni matokeo ya mfumo huu kwasababu chama hakina uhakika na shughuli ambazo waliochaguliwa wanazifanya.

“Zamani waliokuwa wanachaguliwa ni wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji sasa jinsi ya kujihakikishia kile ambacho mgombea anakifanya chama hakina uhakika nacho sana,”anasema.

Anataka wanachama kutoa muda kwa mfumo huo ili kuona kwa matokeo hayo kwasababu kilichofanyika hivi sasa kitu kipya.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Losolutie anasema Rais Magufuli amejaribu kwa kiasi kikubwa kusimamia nidhamu katika chama.

“Yeye (Rais) anachoamini kuwa rushwa ni adui wa haki, rushwa ni rushwa iwe kwenye Serikali ama kwenye chama, ameweza kudhibiti hata kama ipo hatua inachukuliwa bila kigugumizi. Badaa ya kuthibiti nidhamu katika chama inawezesha watu mbalimbali wenye uwezo kugombea nafasi mbalimbali,”anasema.

Anasema hatua hiyo imefungua uwanja kwa watu wengi kushiriki katika siasa za chama hicho bila kujali kama wanauwezo wa kifedha ama wanarefarii ndani chama ili mradi wanajijua kuwa wanaouwezo wa kuongoza.

“Pongezi zimwendee mwenyekiti wa chama wa Taifa kwa kutengeza fursa za watu kugombea kwa wingi. Jambo jingine watu wanakiona chama cha CCM bado kina mvuto mkubwa sana katika nchi kwasababu ndicho kinaongoza Serikali,”anasema.

Anasema hivi sasa watu wanaoona kuwa ili kuingia katika Serikali lazima uwe mwanachama wa CCM huko nako kunavutia watu wengi kuingia katika chama hicho.

Losolutie anasema pia aina ya siasa iliyopo nchini hivi sasa imeegemea upande mmoja na imefanya siasa ya upinzani kuwa ngumu kwawsababu imebana.

“Hali hii inafanya sehemu pekee ni CCM, Watanzania wengi hawawezi mikiki hivyo wanaona sehemu pekee haina mikiki ni CCM. Pia, watu wanaimani CCM na wanaimani kuwa bado kina nguvu kitaendelea kuongoza,”anasema.

Anasema pia wengine wanajitokeza kuwania nafasi katika chama hicho kwasababu wanajua hata kama watashindwa katika uchaguzi basi siku za baadaye watafikiriwa katika nafasi nyingine.

“Watu wengine wanagombea ili waonekane, wanafikiri hata wakikosa nafasi kesho keshokutwa watafikiriwa katika uongozi wa ndani ya chama ama serikalini,”anasema.

Mkazi wa Nkhungu mjini hapa, Salim Abdalah anasema kuwa tofauti na miaka mingine hamasa sasa juu ya uchaguzi ndani ya CCM imehamia kwa wananchi wasio wanachama wa CCM na hata vijiweni ndicho kinachozungumza.

“Mapigano juu ya rushwa nchini yako kwenye dhamira ya kweli ndani Rais Magufuli, jambo hili limewafanya wananchi wa kawaida kuongeza dhamana. Lakini, miongoni mwao (wanachama) bado wana harufu ya rushwa. Hii inawafanya kulazimika kubadilika,”anasema.

Abdallah anasema mabadiliko ya chaguzi za ndani ya CCM, yanawasukuma vijana wa Dodoma kuhamasika kufuatilia siasa hizo.

Anasema hamasa hiyo inachagizwa pia na Serikali kuhamia Dodoma jambo ambalo limeshindwa kufanyika kivitendo kwa zaidi ya miaka 40 tangu tamko hilo litolewe.

“Ukweli kitendo cha Serikali kuhamia Dodoma nacho kimeongeza hamasa wananchi kufuatilia chaguzi za CCM ingawa wao sio wanachama,”anasema.

Hata hivyo, mmoja wa wagombea wa Uchaguzi wa UVCCM, Thobias Mwesiga anasema bado kuna kazi ya kufanya katika kuhakikisha kuwa rushwa ndani ya chaguzi na mali za UVCCM ili zitumike katika kuwanufaisha wanachama wote.

“Ajitahidi kuhakikisha kuwa anapambana na rushwa. Namimi katika hili niseme niko tayari muda na wakati wowote kushirikiana naye kuhakikisha tunamtokomeza huyu mdudu anayeitwa rushwa. Watanzania wengi ni masikini, watanzania wengi wanaimani na CCM.”anasema.

Anasema anaamini kuwa viongozi waliopata nafasi watayafanya hayo kwasababu ndio mwelekeo wa UVCCM wa kulijenga Taifa lipo kinyume na masuala ya rushwa na yanayowakandamiza wanyonge,”anasema.