MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Changamoto za waandishi chipukizi wa Kiswahili

Muktasari:

  • Katika lugha ya Kiswahili, kuna machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kukidhi matakwa ya watumiaji wa lugha katika viwango mbalimbali.
  • Hata hivyo, bado machapisho zaidi yanahitajika kwa kuwa lugha ni chombo kinachokua na kukumbana na mabadiliko mbalimbali. Mabadiliko hayo huiathiri lugha na watumiaji wake.

Ili lugha iweze kuendelea haina budi kuwa na machapisho mbalimbali. Machapisho hayo ni pamoja na majarida na vitabu vinavyojadili mada anuwai za lugha husika katika isimu, fasihi na maeneo mengine muhimu ya lugha hiyo.

Katika lugha ya Kiswahili, kuna machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kukidhi matakwa ya watumiaji wa lugha katika viwango mbalimbali.

Hata hivyo, bado machapisho zaidi yanahitajika kwa kuwa lugha ni chombo kinachokua na kukumbana na mabadiliko mbalimbali. Mabadiliko hayo huiathiri lugha na watumiaji wake.

Mabadiliko yatokeapo, hapana budi waandishi kufanya tafiti na kuandika ili kupata machapisho yatakayokidhi mahitaji ya watumiaji wa lugha husika kuendana na wakati na mazingira husika.

Tukiachana na waandishi wakongwe waliokwishafanya kazi kubwa katika Kiswahili, na ambao pengine bado wanaendelea kufanya kazi hiyo, ili maarifa hayo ya Kiswahili yaweze kuendelea katika lugha, tunahitaji waandishi chipukizi kujitokeza na kuandikia nyanja mbalimbali za Kiswahili.

Wapo waandishi chipukizi wanaojitahidi kuandaa miswada inayohusiana na Kiswahili. Jitihada za waandishi wengi chipukizi hukwamishwa na changamoto kubwa ya gharama za kutoa machapisho wanayokusudia.

Hii hutokana na shughuli za uchapishaji kuwa na gharama kubwa. Kwa sababu hiyo, nia na ndoto za waandishi hao hupotea wakibaki na miswada yao kibindoni.

William Himu ni miongoni mwa waandishi chipukizi wa kazi za kifasihi. Ndoto yake ni kuisaidia jamii kwa kuandika kazi mbalimbali za kifasihi kama vile tamthiliya, riwaya na kazi za ushairi. Himu anaona kuwa, jamii inakabiliwa na matatizo mengi.

Anaamini kuwa kupitia kazi za kifasihi jamii huzinduliwa na kufanywa ifahamu matatizo inayokabiliwa nayo ili ichukue hatua mbalimbali za kujiletea ukombozi kutoka katika matatizo ambayo jamii inakabiliana nayo.

Himu ameandika tamthiliya mbili ambazo ni “Chanzo ni Wewe” (2015) na “Wakilia Tutacheka” (2017). Mwandishi huyu chipukizi anaeleza kwamba, tasnia ya uandishi inakabiliwa na changamoto kubwa ya gharama za uchapishaji ambazo zinamfanya ashindwe kumudu kutoa kazi zake.

Analaumu mfumo uliopo katika jamii wa kutowafikiria waandishi hasa chipukizi wenye mapenzi na uandishi. Anasema: “Katika jamii yetu hakuna chombo maalumu cha kusimamia na kuibua vipaji vya waandishi chipukizi kama zilivyo sanaa nyingine ambazo zinaibuliwa kuanzia ngazi za shule ya msingi na sekondari.

‘’Pia, ninaona jambo la ajabu kwa baadhi ya vyuo vikuu nchini, badala ya kuhamasisha taaluma kwa kuwaibua waandishi na wasomi kupitia uandishi, baadhi ya vyuo hutumia pesa nyingi kuratibu mashindano ya ulimbwende badala ya kuhamasisha taaluma.”

Mwandishi huyu anaona kwamba ulimwengu umefika ulipo kwa sababu ya maandiko. Anaitaka jamii kuelekeza jicho na moyo wake katika maandishi kwa kuwa maandishi hayo ni hazina yenye thamani isiyomithilika.

Anawaomba wachapishaji kuwafikiria waandishi chipukizi ili waweze kuwadhamini katika kazi kwa lengo la kukuza vipaji vyao lakini pia ili waweze kufikisha ujumbe wao katika jamii.

Mintarafu suala la mrabaha, Himu anaeleza kuwa bado waandishi wanaminywa na wachapishaji kwa kupewa kiasi kidogo cha pesa pindi machapisho yao yanapouzwa.

Himu anaiomba jamii hasa wachapishaji kutambua mchango wa waandishi chipukizi ili kuwawezesha kukuza vipaji vyao.