Comoro na migogoro ya kisiasa isiyoisha

Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete akimkaribisha ikulu jijini Dar es Salaam Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ahmed Abdallah Sambi. Hiyo ilikuwa mwaka 2010 wakati kiongozi huyo alipotembelea nchini. Picha na maktaba

Muktasari:

Si hilo tu, Kikwete alikuwa msuluhishi wa migogoro ya Comoro ambayo imepitia kwenye historia ya kuwa na idadi ya serikali 21 zilizoondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi.

Ilikuwa Machi, 2009 wakati Rais wa Comoro kwa wakati huo, Ahmed Abdallah Sambi alipokabidhi medali maalumu kwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete kutokana na mchango wa Tanzania katika kukikomboa kisiwa cha Anjouan.

Si hilo tu, Kikwete alikuwa msuluhishi wa migogoro ya Comoro ambayo imepitia kwenye historia ya kuwa na idadi ya serikali 21 zilizoondolewa madarakani kwa njia ya mapinduzi.

Lakini, tangu juhudi za Tanzania katika kuleta amani kwenye visiwa hivyo kufanikiwa, ikiwamo kusaidia kukikomboa kisiwa cha Anjouan, chokochoko za kisiasa zimeanza tena baada ya kutokea madai kwamba kiongozi wa sasa, Azali Assoumani anataka kubadili Katiba ‘kibabe’ ili asalie madarakani hadi mwaka 2030.

Kitendo chake hicho kimeonekana kupata kikwazo toka kwa Rais mstaafu, Ahmed Abdallah Sambi ambaye amekuwa akihubiri waziwazi akipinga uvunjaji wa Katiba ya nchi. Kelele hizo za Sambi zimemfikisha kwenye uamuzi wa kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani ikiwamo kunyang’anywa walinzi.

Ni Tanzania pekee ndiyo inayoweza kujivunia kwamba imewasaidia Wacomoro na tangu wakati huo kumekuwa na utulivu, japo kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 kulikuwa na viashiria vya vurugu hasa baada ya uchaguzi wa rais kulazimika kurudiwa katika baadhi ya maeneo.

Rais Sambi ambaye aliongoza visiwani hivyo kuanzia mwaka 2006 hadi 2011, uongozi wake uliimarisha ushirikiano na Tanzania kiasi cha kurejeshwa safari za anga kwa ndege za Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania au kwa sasa ATCL), vyama vya wafanyabiashara wa nchi hizi walianzisha ushirikiano na kuna wakati Rais Sambi alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma.

Medali maalumu ambazo ni ya ushujaa na heshima ya juu kwa wananchi wa Comoro zilikabidhiwa kwenye sherehe zilizofanyika uwanja wa Missiri kisiwani Anjouan Machi 2009. Ni sherehe zilizoongeza mshikamano kati ya Tanzania na Comoro kwani mbali na Kikwete, wengine waliotunukiwa ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa wakati huo, Bernard Membe na aliyekuwa Mkuu wa Majeshi Jenerali Davis Mwamunyange.

Tofauti na hali ilivyokuwa huko nyuma, hivi sasa siasa za Muungano wa visiwa hivyo imebadilika, Sambi ambaye ni Rais mstaafu hivi sasa yuko kwenye kizuizi cha nyumbani na ameandika barua kwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahama na kwa Serikali ya Tanzania kuomba msaada akiomba msaada.

Barua kwenda AU

“Ninaandika nikiwa ndani ya nyumba yangu baada ya serikali kuniweka kwenye kizuizi cha nyumbani kwa tuhuma za rushwa na wamenizuia kusafiri nje ya Comoro.” Ndivyo ilivyoanza barua ya Sambi kwa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika.

Kiongozi huyo ambaye baada ya kustaafu ameamua kujishughulisha na masuala ya dini kwa kutoa mahubiri msikitiini, kwenye barua yake anasema tuhuma dhidi yake ziko kisiasa zaidi na hasa baada ya kupinga uamuzi wa kusimamisha Mahakama ya Katiba na hoja kubadili katiba.

Sambi ameandika kwenye barua hiyo kwamba pia Serikali imemuondolea ulinzi hali inayomfanya ahisi maisha yake yako hatarini, hasa kutokana na madai kwamba Rais wa sasa wa Comoro, Azali Assoumani amedhamiria kubadili Katiba kwa lengo la kuongeza kipindi kingine cha uongozi.

Katika barua nyingine aliyomwandikia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania, alibainisha kuwa. “aliporejea Comoro Mei 12, 2018 akitokea Ufaransa Serikali imekuwa ikimnyanyasa.” Anasema Mei 15 alihojiwa na askari kuhusu sheria iliyopitishwa na Bunge mwaka 2008 (wakati akiwa Rais) inayohusu masuala ya uchumi na baada ya kuhojiwa aliamuliwa kutosafiri nje ya Moroni.

Anasema pia alizuiwa kuhutubia miskitini bila kujali yeye ni imam na Mei 19 aliwekwa chini ya ulinzi nyumbani kwake, hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka wala kuingia, na watu 11 wa chama chake aliokuwa nao nyumbani kwake wakati akiwekwa kizuizini nao wamezuiwa kutoka.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Profesa Adolf Mkenda alipoulizwa kuhusu suala hilo kwa njia ya simu alisema “Nisingependa kusema chochote kwa sasa hivi. Wote tunaangalia kinachoendelea kule.”

Kiongozi huyo mstaafu ana historia ya urafiki na Tanzania enzi za utawala wake ikiwamo kuimarisha njia za biashara kati ya mataifa haya mawili.

Sambi ndiye aliyeleta ukaribu wa Tanzania na Comoro, tangu astaafu uongozi wa nchi ameendelea kuwa kiongozi wa kisiasa anayekubalika katika visiwani hivyo na kukubalika kwake huko ndiko kulikomuwezesha Azali Assoumani kuingia madarakani.

Sambi aliweza kumaliza kipindi chake cha uongozi madarakani bila kuwa na vurugu za kisiasa, na pengine kwa kuwa hakuwa na pilikapilika za kutaka kuongeza muda wa kusalia madarakani. Hali hiyo kwa sasa imekuwa tofauti kwa aliyempigia debe wakati wa kampeni na kumkabidhi madaraka ya nchi. Sambi sasa anatuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Kiongozi wa sasa visiwani humo, Assoumani amekuja na mipango inayoweza kuirudisha Comoro kwenye historia ya migogoro ya kisiasa iliyosababisha mapinduzi ya mara kwa mara.

Assoumani amevunja Mahakama ya Katiba na ameelezwa kutaka kufanya mabadiliko ya katiba lenye lengo la kuongeza muda wa kuendelea kukaa madarakani hadi mwaka 2030.

Kinachoonekana kutokea Comoro hivi sasa ni kwamba Rais Assoumani ameamua kufanya hila kumzima Sambi anayeoonekana kutaka kukwamisha jitihada zake za kubadili katiba ili ajiongezee muda wa kukaa madarakani.

Hivyo ni juu ya viongozi wa Afrika kuona namna gani wanaweza kuingilia mgogoro visiwa humo kama walivyowahi kufanya siku za nyuma wakati wa mzozo wa kisiwa cha Anjouan kilichokuwa kikikaliwa kimabavu na Kanali Mohamed Bacar.

Siasa za Comoro

Kuna wakati wapinzani wa Comoro wakiongozwa na Ali Houmadi Msaidie, walipinga Bunge la nchi hiyo ambalo mwaka 2010 lilikuwa limeitisha Uchaguzi Mkuu kwamba ufanyike Novemba 2011, wakati huo Sambi ndiye alikuwa Rais. Lakini, wapinzani hao walidai kufanya hivyo ni sawa na mapinduzi ya Katiba yatakayomwezesha Rais wa Visiwa hivyo Sambi kuendelea kuwa madarakani kwa miezi18 zaidi.

Madai mengine yaliyotolewa na wapinzani hao ambao malalamiko yao waliyafikisha hadi Makao Makuu ya Umoja wa Afrika, Addis Ababa nchini Ethiopia , wakimtuhumu Sambi kuwa na ukaribu na Azali Assoumani ambaye alikuwa akigombea urais kwa wakati huo, wakidai atamsaidia kupata ushindi kwa njia za hila.