Dakika mbili zampa Jakline ajira, nyumba mbili

Jackline Sakalu

Alipomaliza darasa la saba, Jackline Juma Sakilu alitoka kijijini kwao mkoani Singida na kwenda Arusha kutafuta namna ya kutoka kimaisha kupitia riadha.

“Nilikwenda kwa kocha Zacharia Gwandu, nilikaa kwa miaka mitano hadi 2007 na katika kipindi hicho, nilifanya sana mazoezi.

“Si unajua tena, nikakutana na mwenzangu, tukaanza uhusiano na nikaondoka kwa kocha.

“Niliendelea kufanya mazoezi huku mwenzangu akinisapoti, baada ya miaka miwili zilitokea nafasi za kuajiriwa jeshini, nakumbuka mwanzo walisema wanahitaji wanariadha chipukizi.

“Juma Ikangaa akashauri wachukue wanariadha wa viwango, wakaandaa mbio za kitaifa ambazo tulianza kuchuana Arusha na fainali Dar es Salaam.

“Nilishiriki mbio za mita 800 nikatumia dakika 2:00:10 na moja kwa moja kufuzu mchujo wa kupata ajira jeshini kwani nilikuwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu wanapata ajira,” anasimulia Sakilu.

Mafanikio kupitia riadha

“Achilia mbali kupata ajira jeshini, kupitia riadha nimejenga nyumba Arusha, Singida  na nina mafanikio mengine ambayo ni ya binafsi,” anasema Sakilu.

Anasema amefahamiana na watu wa mataifa mbalimbali kama Brazil, China na Ufaransa ambako amekimbia mbio nyingi binafsi huku akiwa ameiwakilisha nchi katika mbio za dunia za nyika na za majeshi mara kadhaa.

Aligomea timu ya Madola 2014

Kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2014, Jackline Sakilu alikuwa miongoni mwa wachezaji walioitwa, lakini hakujiunga na wenzake katika kambi iliyoandaliwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe.

“Hili suala kila mtu alizungumza lake, ukweli nilikuwa nauguliwa na mama yangu mzazi na mimi ndiye niliyekuwa nikimuuguza, niliandika barua RT kuomba nisijiunge na timu nikakubaliwa.

“Nyuma akatokea mtu na kuzusha nimekataa kwa makusudi, ilikuwa vurugu hadi kunyang’anywa pasipoti yangu,” anasema.