Dar es Salaam inavyojipanga kukuza utalii wa malikale, miundombinu yake

Moja ya mabasi maalumu kwa ajili ya watalii watakaokuwa wanatembelea vivutio mbalimbali vilivyopo jijini Dar es Salaam. Picha na Nasra Abdallah.

Muktasari:

  • Pamoja na hilo haiifanyi Dar es Salaam kuwa nyuma katika utalii ambao ni chanzo cha mapato katika maeneo mengi duniani kutokana na kuwa na majengo ya zamani yaliyotumika enzi za ukoloni yanayoweza kuwa kivutio kwa wengi.

Dar es Salaam ni moja ya mikoa ambayo haijabarikiwa kuwa na mbuga za wanyama kama ilivyo Jiji la Arusha ambao uchumi wake kwa kiasi kikubwa unategemea utalii.

Pamoja na hilo haiifanyi Dar es Salaam kuwa nyuma katika utalii ambao ni chanzo cha mapato katika maeneo mengi duniani kutokana na kuwa na majengo ya zamani yaliyotumika enzi za ukoloni yanayoweza kuwa kivutio kwa wengi.

Dar es Salaam ambayo kwa sehemu kubwa imezungukwa na fukwe zenye mchanga mweupe (whitesand beach) maarufu kibiashara, ina majengo marefu yanayoipamba.

Vilevile, kuna visiwa vidogo kama Bongoyo na Mbudya ambavyo vimekuwa vikiwavutia Watanzania na wageni kuogelea na kubarizi au kukaa huko kwa siku kadhaa, ingawa bado hayajawa maeneo rasmi ya utalii.

Uwepo wa bandari kongwe ya Dar es Salaam, majengo na nyumba za ibada yaliyojengwa miongo kadhaa kabla ya uhuru yawezekana ni vivutio kwa wengi kutokana na mtindo wa zamani wa jengo kuandikwa mwaka lilipo.

Bahati nyingine iliyopo ni kuwa jiji hilo ndilo lango kuu kwa wageni kuingia Tanzania lenye miundombinu muhimu kuliko maeneo mengine. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kituo kikubwa zaidi cha mabasi yaendayo mikoani, reli na daraja la Kigamboni ambalo ni refu zaidi Afrika Mashariki na Kati likiwa na urefu wa zaidi ya mita 600.

Vivutio vilivyopo ni sawa na vile vya majiji ya London nchini Uingereza au New York, Marekani yanayotegemea utalii wa namna hiyo. Huko, sehemu kubwa ya vivutio vyao ni madaraja, majengo ya kale, nyumba za makumbusho na, miundombinu na mandhari ya jiji hilo kongwe na maarufu duniani.

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana anasema ofisi yake ina dawati la utalii tangu mwaka 2008, shughuli zilizoingizwa rasmi kwenye bajeti kuanzia kipindi hicho.

Liana ambaye alizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa kukuza utalii uliofanyika hivi karibuni, anasema jiji lilizingatia maoni na ushauri uliotolewa na wadau mbalimbali kupitia mikutano iliyobainisha fursa ambazo linazo na umuhimu wa kulifanya kuwa kitovu cha utalii na kuongeza mapato.

“Mradi huu wa utalii unalenga kubadili sura ya jiji kutoka kuwa njia ya kupita wageni kuelekea katika vivutio na kuwa kituo cha utalii,” anasema.

Imezoeleka kuwa idadi kubwa ya wageni wafikao nchini hutumia Bandari ya Dar es Salaam na JNIA kwenda kwenye vituo vingine vya utalii kzikiwamo hifadhi za taifa na sehemu nyingine za nchi.

“Watalii wamekuwa wakifanya hivi na kushindwa kujua kama Dar es Salaam ina sehemu ambazo wanaweza kukaa kabla ya kuendelea na safari zao na hiyo ni moja ya sababu iliyoifanya halmashauri (ya jiji) kuamua kuvitangaza vituo vyake vya utalii kwa kasi,” anasema.

Maandalizi yakoje?

Katika kutekeleza mikakati hiyo, Liana ambaye aliwahi kuwa mkurugenzi mtendaji wa Jiji la Arusha, anasema shughuli mbalimbali zimeshaanza kufanyika.

Anasema kuna uhifadhi wa majengo ya kihistoria ambayo ni moja ya kivutio vya wageni.

Anayataja majengo hayo kuwa ni pamoja na lile la Halmashauri ya Jiji (City Hall), Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, Kanisa la Azania Front, Ukumbi wa Karimjee na Old Boma.

Kadhalika, kumeanzishwa kitabu cha utalii kinachotoa taarifa za vivutio mbalimbali vilivyopo jijini humo, mahali pa kwenda , vitu muhimu vya kuangalia na taarifa za kiusalama kumuongoza mgeni yeyote wa ndani au nje ya nchi.

Kitabu hicho kinapatikana katika hoteli mbalimbali na dawati la utalii la jiji lililoanzishwa JNIA na baadhi ya maeneo ya utalii.

“Tunaendelea kutangaza vivutio vya utalii vya jiji letu ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi na Bodi ya Utalii (TTB) na kutoa mafunzo kwa waongoza watalii ili watoe taarifa sahihi watakapotakiwa kufanya hivyo,” anasema Liana.

Kwa kushirikiana na Jumuiya ya Wasanifu Majengo (Taa), jiji limekarabati jengo la kihistoria la Old Boma lililojengwa mwaka 1860 na kuanzisha kituo maalumu cha utalii ikiwemo mgahawa wa kitalii, maduka na ukumbi mdogo wa mikutano.

Meya wa Dar es Salaam, Isaya Mwita anasema katika kutekeleza mpango huo halmashauri inashirikiana na sekta binafsi na tayari imeanza kutoa elimu ya kuwahudumia wageni kwa madereva teksi na mamalishe.

Kwenye mpango huo, madereva 25 wanaoegesha magari yao karibu na bandari ya boti zitokazo Zanzibar, JNIA na mamalishe 25 wameshanufaika na maarifa hayo yatakayowawezesha kutoa huduma za kiwango cha kimataifa ili kukidhi matarajio ya wageni.

Mwita anasema jiji limeanza kukamilisha hatua za ununuzi wa mabasi maalum kwa ajili ya kuwatembeza watalii ndani ya jiji.

“Pamoja na mipango yote hiyo ni lazima tutengeneze mazingira mazuri ya kuwafanya watalii wabaki katika jiji letu. Tumeshaanza kutengeneza na kuboresha bustani zetu, sehemu za kupumzikia na kucheza ngoma za jadi na kuboresha huduma kwa watalii,” anasema Mwita.

Pia yataanzishwa matamasha ya kitaifa yatakayosaidia kutangaza jiji na kuleta idadi kubwa ya watalii kama ilivyo sauti za Busara Zanzibar na kuamsha uelewa wa wananchi juu ya vivutio vilivyopo na kuwa na siku ya kusafisha fukwe.

Mafunzo ya ukarimu yanatolewa na Chuo cha Taifa cha Utalii. Ofisa habari wa chuo hicho, Consolatha Shoo anasema wamelenga kundi hilo kwa wasababu ndio watu wa kwanza kuwapokea wageni wanaoingia jijini hapa iwe kutoka nje au mikoani.

“Mgeni yeyote kutoka nje ya nchi akifika uwanja wa ndege anakutana na dereva teksi na mtaani anakula kwenye migahawa hivyo ukarimu unatakiwa uanze kwao,” anasema Consolatha.

Anasema chuo kinatoa mafunzo ya siku tano kwa makundi hayo ya wadau muhimu wa sekta na huduma za utalii.

Anasema mafunzo hayo yanalenga kuwahamasisha mamalishe kufanya biashara zao katika hali ya usafi ili kulinda afya za wateja wao na jamii kwa ujumla.

“Hii itasaidia kuwanyanyua kiuchumi endapo mazingira ya biashara yatakuwa mazuri hata wateja watajitokeza kwa wingi. Hali kadhalika madereva wa teksi, wakitumia lugha nzuri na ya ukarimu abiria watawapenda,” anasisitiza.

Katibu wa umoja wa madereva teksi jijini Dar es Salaam, Ramadhani Ashiru anasema: “Nimegundua, ukarimu ni kitu muhimu sana kwenye biashara yetu. Wakati mwingine mgeni anakuwa na hasira lakini unapozungumza nae vizuri unamrudisha katika hali yake,” anasema.

Mmoja wa mamalishe aliyepata mafunzo ya ukarimu, Lucy Mwizarubi anasema huduma bora huanzia kwenye maandalizi ya chakula mpaka kinapofikishwa kwa mteja.

“Tunachokosea ni kufanya biashara kwa mazoea, tunadhani hata usipomuonyesha ukarimu mteja atakuja tu kumbe sivyo,” anasema.

Wanachosema wananchi

Hamida Semdoe ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo katika eneo la kituo cha stesheni, anasema mpango huo umekuja wakati mzuri ambapo Rais kakataza wafanyabiashara wa aina yake kutobughudhiwa.

“Nina imani nitapata wateja wengi watakaopita hapa ukizingatia kuwa majengo yaliyotajwa kwa ajili ya utalii nipo karibu nayo, najua mtalii haweezi kupita bila kununua soda au maji ninayouza,” anasema Hamida.

Hassan Mwiru, mkazi wa Kariakoo, anasema mpango huo wa utalii kwa wakazi wa Dar es Salaam ni neema kwani utasaidia kuzalisha ajira na fursa mpya za biashara.

Wizara kuibeba Dar

Akizungumza katika siku ya ufunguzi wa onyesho la chimbuko la binadamu Afrika, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla alisema mojawapo wa mikakati yao ni pamoja na kulifanya Jiji la Dar es Salaam kama moja ya majiji yenye ushawishi mkubwa wa utalii.

Kigwangalla anaitaja Makumbusho ya Taifa palipohifadhiwa vitu mbalimbali ikiwemo fuvu la binadamu wa kale kama mojawapo wa vivutio muhimu jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa TTB, Devota Mdachi anasema watajitahidi kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika jiji hilo katika sehemu mbalimbali duniani.