Dawa ya elimu Tanzania ni zaidi ya kuwa na chombo cha kusimamia elimu

Mwalimu akiwajibika shuleni. Walimu ndio nguzo kuu ya mafanikio ya elimu. Picha ya Maktaba

Muktasari:

Katika jitihada za kufanya tukio hilo lipate watu na hadhi, waandaaji waliamua lifanyikie katika ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

       Hivi karibuni, asasi isiyo ya kiserikali ya HakiElimu, iliandaa kongamano la kujadili hali ya elimu ya Tanzania Bara kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali.

Katika jitihada za kufanya tukio hilo lipate watu na hadhi, waandaaji waliamua lifanyikie katika ukumbi wa Nkrumah uliopo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Huu ni ukumbi wa mapinduzi ya mawazo ya Kwame Nkurmah, aliyekuwa rais wa kwanza wa Ghana.

Katika Kongamano hilo ambalo nilitegemea wasomi wangezungumzia kwa mapana yake, dhana ya uboreshaji wa elimu katika nchi kwa kubeba dhana aliyokuwa nayo Nkurumah, wajumbe walijikita bila ya kujua katika koti la kubariki mtazamo wa siku nyingi wa HakiElimu.

Mtazamo huo ni ule utokanao na dhana kuwa ili elimu ya Tanzania iwe bora zaidi, kunatakiwa kuwapo kwa chombo cha kusimamia elimu pekee kama vile Kamishna wa Magereza anavyosimamia magereza nchini ndani ya Wizara ya mambo ya Ndani.

Makala haya yanajaribu kupitia kwa kifupi elimu ya Tanzania kwa sasa, changamoto zake na namna ya kukabiliana na changamoto hizo

Dhamira yangu ni kushauri mamlaka husika kuchukua hatua katika kurekebisha kasoro zilizopo ili kuifikisha elimu ya Tanzania mahali inapostahili.

Elimu ya Tanzania

Elimu ya Tanzania kama nchi ni elimu ambayo imesukwa vizuri katika kuandaa nini cha kuwafundisha watoto wetu. Ni elimu inayoheshimika ndani na nje ya Afrika.

Silabasi inayofundishwa hapa Tanzania kwa sehemu kubwa inakidhi mahitaji ya nchi isipokuwa kinachotakiwa ni kuboresha mbinu za ufundishaji, ili watoa elimu waweze kuwapa wanafunzi elimu inayowasaidia katika kukabiliana na changamoto zilizopo.

Silabasi ya Tanzania inaheshimiwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Hata mhitimu wa shahada ya kwanza nchini anapohitaji kusoma shahada ya uzamili katika vyuo katika baadhi ya nchi za Ulaya, haihitaji kufanyiwa usaili kama inavyofanyika kwa wanafunzi wa baadhi ya nchi barani Afrika.

Tunahitaji maboresho madogo madogo katika silabasi yetu, ili kukidhi mahitaji ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na kuwanoa vizuri walimu wetu mara kwa mara ili wapate mbinu mpya.

Changamoto za elimu Tanzania

Changamoto kubwa kuliko zote katika elimu ya Tanzania, ni maslahi duni ya walimu katia ngazi zote. Wataalamu wanakubaliana kuwa ubora wa nchi hautegemei barabara, demokrasia iliyopo wala uchumi wa nchi hiyo.

Ubora wa nchi hupimwa kwa kuangalia ubora wa walimu wanaowafundisha watoto. Ili uwapate walimu bora lazima upitie hatua zifuatazo.

Kwanza, nchi ikubali kwamba utoaji wa elimu bora ni gharama kubwa na matokeo yake hayawezi kupimwa kwa Dola za Marekani. Watanzania watakapokubaliana kuwekeza kwenye elimu, watawasukuma wanasiasa kuhakikisha kuwa nchi inawekeza katika elimu kwa viwango vinavyokubalika.

Pili, nchi ikishawekeza kwenye elimu, walimu walipwe vizuri ili watekeleze majukumu yao kwa kuruhusu akili zao kumwaga ujuzi wote kwa watoto na kuweka mawazo yao yote kwa maendeleo ya watoto.

Tatu, usimamizi wa walimu haujawa mzuri kutokana na nchi kutokuwa na kanuni za kuwapata wasimamizi wa elimu. Viongozi wengi wa elimu katika ngazi zote huteuliwa kwa kujuana. Baadhi ya maofisa elimu wa wilaya wanawateua watu watakaowatii na kuwaweka kuwa walimu wakuu, wakuu wa shule na waratibu elimu kata

Kwa ngazi ya Wizara, hakuna utaratibu wa kuwapata maofisa elimu wa wilaya wenye ujuzi wa kusimamia elimu katika wilaya.

Usishangae kusikia kuwa hadi leo, kuna maofisa elimu wasio na shahada, lakini wanasimamia taaluma ambayo hutolewa na walimu wenye shahada.

Namna ya kukabiliana na changamoto hizi

Kwa kuwa Tanzania ina silabasi nzuri ya elimu katika ngazi zote, kipaumbele cha nchi kingeelekezwa katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza, mishahara ya walimu iwekwe kwa kiwango cha kuwavutia watu wenye ufaulu wa juu kupenda kazi ya ualimu. Kinachowavutia watu kujiunga na taaluma fulani ni maslahi watakayopata wakiwa kwenye taaluma hiyo.

Walimu wa Tanzania ni takribani asilimia 60 ya watumishi wote kwenye utumishi wa umma, lakini ukija kwenye mgawanyo wa mishahara, wanalipwa takribani asilimia 49 ya mishahara yote inayotengwa kwa ajili ya kuwalipa watumishi wa umma.

Kulipwa kwa mishahara ya walimu kuambatane na kulipwa kwa madeni yao, wapandishwe madaraja kwa wakati na kurekebishiwa mishahara kwa wakati na kupewa fedha za likizo.

Pili, Silabasi ya elimu yetu inapaswa kuangaliwa upya kwa kutoa uhuru kwa walimu kufundisha kulingana na sehemu husika. Kwa mfano, watoto wanaosoma kandokando ya Ziwa Tanganyika, wapewe elimu ya ziada juu ya uvuvi wa samaki.

Hii itakuwa kwa watu wote wanaokaa karibu na sehemu zenye uvuvi. Wanafunzi wanaoishi maeneo wanakolima ndizi wapate elimu zaidi juu ya utunzaji wa ndizi.

Walimu wakipewa uhuru huo wa kutoa elimu kulingana na sehemu walipo, mhitimu atakuwa na fursa nzuri ya kuchangia maendeleo kutokana na elimu aliyopata kutoka shuleni.

Tatu, usimamizi wa utoaji wa elimu uimarishwe kwa kuweka taasisi huru za kusimamia elimu kitaalamu bila ya kuingiliwa na wanasiasa. Elimu bora husimamiwa na taasisi tatu zilizo huru zinazoanzishwa kwa mujibu wa sheria za Bunge.

Taasisi hizo ni ile inayopima ubora wa elimu (Baraza la Mitihani), ya pili ni ile inayotunga silabasi ya kufundishwa na walimu ( kwa Tanzania kuna Taasisi ya Elimu Tanzania).

Taasisi ya tatu ambayo haipo ni taasisi ya kukagua jinsi elimu inavyotolewa kama inakidhi matakwa ya silabasi. Taasisi hii imekuwa ikijulikana kama ukaguzi wa shule ambao kwa sasa huitwa udhibiti ubora wa shule.

Kwa mfumo wetu, bado Udhibiti ubora wa shule wizarani. Kiini cha matatizo ya ubora wa elimu ni kutokuwapo kwa taasisi hii. Natoa wito idara hii iwe wakala rasmi wa Serikali.

Aidha, kuna taasisi ya nne ambayo ni

ni bodi ya kusimamia taaluma ya ualimu. Ualimu ni taaluma na taaluma zote duniani zina bodi zake. Mpaka sasa uanzishwaji wa bodi hii umekuwa ukipigwa danadana.

Sio ajabu kuona kuwa hoja ya kuundwa kwa chombo hicho si kipaumbele cha wanasiasa, kwa kuwa hawajaona umuhimu wa walimu kuwa na bodi yao kudhibiti taaluma ya ualimu.

Ni maoni yangu kwamba hayo yakirekebishwa, elimu yetu itaendelea kuwa bora zaidi. Hatuhitaji kuwa na chombo cha kuratibu elimu nchini kama ilivyo kwa TCRA, Sumatra na nyinginezo. Kinachotakiwa ni kutumia mfumo ulioko kwa kuufanya kuwa imara katika kutoa elimu iliyo bora.

Mwalimu Ezekiah Oluoch anapatikana kwa barua pepe: [email protected]