MAONI YA MHARIRI: Dawa ya ufaulu bora ni kuwekeza katika elimu

Muktasari:

Baada ya matokeo hayo kutangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) wiki hii na kuonyesha shule sita za mkoa wa Dar es Salaam zikishika mkia kitaifa, tayari walimu wakuu wa shule mbili wameingia matatani, baada ya uongozi wa Wilaya ya Kigamboni kuagiza wavuliwe madaraka kwa madai ya shule zao kufanya vibaya.

Kama ilivyo ada kila yanapotoka matokeo ya mitihani ya taifa hasa wa kidato cha nne, hapakosekani matukio ya watu ‘kushikana uchawi’.

Baada ya matokeo hayo kutangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) wiki hii na kuonyesha shule sita za mkoa wa Dar es Salaam zikishika mkia kitaifa, tayari walimu wakuu wa shule mbili wameingia matatani, baada ya uongozi wa Wilaya ya Kigamboni kuagiza wavuliwe madaraka kwa madai ya shule zao kufanya vibaya.

Shule hizo ni Somangira na Kidete zilizomo katika orodha ya shule 10 zilizofanya vibaya kitaifa.

Zipo sababu zilizoisukuma mamlaka hiyo kufanya uamuzi huo na inawezekana sababu hizo zikawa na mashiko, lakini tumejiuliza ikiwa walimu hao ndiyo sababu kuu iliyochangia shule hizo kufanya vibaya.

Kwa jumla, yako matatizo ama changamoto nyingi zinazochangia kwa namna moja au nyingine kuwapo kwa matokeo mabaya katika shule za umma.

Baadhi ya changamoto hizo ni miundombinu duni ya kujifunzia inayotokana na uwekezaji mdogo unaofanywa katika sekta ya elimu, uhaba na katika baadhi ya maeneo ukosefu kabisa wa walimu, ukosefu wa ushirikiano wa wadau wa elimu, yaani, walimu, wazazi, wanafunzi na viongozi wa kisiasa.

Changamoto nyingine ni uhaba wa vitabu, huduma duni kwa wanafunzi wa kike wawapo shuleni, walimu kukosa morali ya kufundisha hali inayotokana na kukosa maslahi mazuri na hata kada hiyo kutothaminiwa.

Japo udhaifu wa uongozi wa shule nao unaweza kuwa moja ya sababu, lakini katika mlolongo huu wa changamoto tulizotaja tena zikiwa ni baadhi tu, ni muhali kwa shule hizi kufanya vizuri kitaaluma hata kama kutakuwa na uboreshaji mkubwa katika uongozi wa shule.

Ndiyo maana tunaamini kuwa walimu hawa wametolewa tu kuwa mbuzi wa kafara, lakini bado mamlaka husika zimeshindwa kubaini kiini cha matatizo na kukitafutia ufumbuzi.

Aidha, kilichotokea kwa walimu wa Dar es Salaam siyo kitu kigeni, kimekuwa kikitokea mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Walimu wakuu na wakuu wa shule mara nyingi wanakuwa waathirika wa matokeo mabaya ya shule zao kwa kuvuliwa madaraka au kusimamishwa kazi.

Hatupingi hatua hiyo ila tunahoji mchakato wa kutekeleza uamuzi huo kama huwa unafuata taratibu na kanuni zinazosimamia elimu na hata uwajibikaji wa walimu kama watumishi wa umma. Na hata mchakato ukifuatwa, je, wahusika wanapata nafasi ya kusikilizwa au hatua zinachukuliwa mara moja kwa kuwa tu mamlaka za juu zimeshafanya uamuzi?

Rai yetu ni kuwa badala ya ‘kuwasulubu’ walimu pekee, mamlaka zijihimu kutafuta kiini cha sababu ya shule kufanya vibaya ambazo baadhi tumeshazitaja hapo awali.

Kuna mazingira hata uongozi wa shule ukiwa shupavu na mahiri, lakini kama uwiano wa walimu na wanafunzi haupo sawa, wanafunzi hawana nidhamu tangu nyumbani, utoro wa wanafunzi umetamalaki kwa sababu ya wanafunzi kuishi mbali, shule kukosa mazingira rafiki kwa ufundishaji na ujifunzaji; kuwavua madaraka wakuu wa shule ni sawa na kuwaonea. Katu hatua hiyo haiwezi kuwa dawa pekee ya kukuza ufaulu katika shule za umma.

Serikali iamke sasa na kuamua kuwa na dhamira ya dhati ya kuwekeza vilivyo katika shule zake, ili ziwe ni taasisi zenye ushindani wa kitaaluma na kuwa kimbilio la wengi kama ilivyokuwa zamani.