TUONGEE UJANA: Dhibiti hasira yako “Hasira Hasara”

Muktasari:

Inawezekana ukakwazika kiasi cha kupata hasira ukiwa nyumbani, njiani na hata ofisini.

Kukasirika ni sehemu ya binadamu, na inafahamika kila mmoja wetu anakasirika pale tu anapoamini isivyo jambo tofauti na kawaida.

Inawezekana ukakwazika kiasi cha kupata hasira ukiwa nyumbani, njiani na hata ofisini.

Hivyo kushikwa na hasara ni maumbile ya binaadamu ambayo hayakwepi, ila kuchukua hatua mbaya dhidi ya aliyesababisha hasira ni jambo linaloweza kuepukika.

Unachotakiwa kufanya kwanza kuhakikisha aliyekukwaza anafahamu kama amefanya hivyo.

Jambo la kuzingatia wakati wa kumueleza kuwa amekuudhi ni kutumia lugha ya busara na ukiwa umetulia ili usije kukasirisha unayemueleza kwa sababu inawezekana hafahamu kama amekukwaza.

Ili usiwe na hasira wakati unamueleza kuwa alikuudhi na kukukasirisha kama upo ofisini au nyumbani ondoka kwa muda eneo hilo.

Ukikaa mbali na aliyekuudhi kwa dakika chache utakaporudi munkari utakuwa umepoa na unaweza kumuelewesha bila kuleta madhara.

Kuzungumza ukiwa na hasira kali kunaweza kukusababishia matatizo ikiwa kushusha hadhi yako.

Wengi wakiwa na hasira wanazungumza maneno ambayo wakiyasikia baadaye hutamani kukataa kama waliyasema wao.

Ili usifike huko chukua hatua hizo muhimu kabla ya kumkabili aliyekuudhi, kukaa kimya kutakufanya uendelee kuwa na hasira naye na usimsamehe.

Ukimueleza kwa busara na ukatumia dakika chache kutafakari maneno ya kutumia ambayo hayatakuwa na madhara kwake wala kwako itakusaidia kumsamehe na kuanza upya.

Licha ya kumueleza fikiria namna bora ya kupata suluhisho kati yenu na utafakari kulimaliza kama siyo kulikomesha kabisa jambo lililowafanya mkafikia kuudhiana.

Inawezekana unachelewa kufika kazini kutokana na foleni, mkeo hakuelewi kutokana na kuchelewa kurudi nyumbani, hawa wote kila mmoja kwa wakati wake akikulaumu utapatwa na hasira kwa sababu hukudhamiria hayo yatokee.

Hivyo ukikasirika na kuwaeleza kinagaubaga jinsi wanavyokuudhi kwa kukulaumu kwa jambo usilolipanga, fikiria mara mbili utafanya nini kutatua kadhia hiyo.

Kuendelea kufanya jambo ambalo ukisemwa unachukia inaweza kuwa na madhara zaidi kwa sababu ipo siku utashindwa kuzuia hasira zako.

Inajulikana kuzuia hasira ni changamoto, lakini kila mara zinapokupata kumbuka usemi wa Wahenga usemao “Hasira Hasara”, kwa maana ukiziendekeza zinaweza kuleta madhara kwako na kwa jamii yako pia.

Wapo watu katika umri wa ujana kama ulionao wamefungwa au wapo mahabusu kwa sababu ya hasira, walichukia wakashindwa kujidhibiti na kufanya mambo mabaya ikiwamo kuua na sasa wanasota rumande au gerezani.

Busara zaidi kuwa na mtu au watu utakaokuwa unakwenda kuwaomba ushauri unapoona hasira zimekuzidi na unashindwa kujiuzia au kumsamehe aliyekuudhi.

Wakati wa ujana vikwazo ni vingi na ukikaa kimya, ukizungumza kwa upole kwa aliyekuudhi unaonekana unamuogopa, hivyo kama huwezi kujiuzia unapoudhiwa tafuta ushauri kwanza kabla ya kuzungumza na aliyekuudhi.

Yale yote yaliyo ndani ya uwezo wako ambayo mara kadhaa yamekuwa sababu ya wewe kukwazika na unaweza kuyazuia, fanya hima kuyadhibiti ili uwe salama.

Narudia tena “Hasira Hasara”.

Imeandaliwa na Kalunde Jamal