Dhibiti magonjwa na wadudu kwa njia za asili

Vitunguu saumu na pilipili. Hizi zote ni aina mbalimbali za vitu vya asili vinavyoweza kutumika kudhibiti magonjwa na wadudu shambani. Picha na mtandao wa motherearthliving

Muktasari:

Mwarobaini

  • Mwarobaini ni mti unaostahimili ukame, unaotoa kivuli na pia umeonekana kuwa na manufaa makubwa kama tiba kwa binadamu na mafuta yake hutumika kutengeneza sabuni.
  • Kati ya dawa zote za asili, mwarobaini umethibitika kufanya vizuri zaidi kutokana na uwezo wake maradufu ya dawa nyingine zaidi hata ya zile za viwandani
  • Ili  kutengeneza dawa kutokana na unga wa mbegu za mwarobaini, twanga mbegu kiasi zilizokomaa na kukaushwa ili kupata unga. Changanya na maji lita moja kisha nyunyiza bustanini ili kuzuia wadudu.

Kuna madhara mengi yatokanyo na matumizi ya dawa za viwandani zenye sumu. Madhara hayo ni pamoja na athari za afya kwa binadamu, wanyama, mimea, na uharibifu wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Kama wakulima na wafugaji watazingatia matumizi sahihi ya dawa za asili pamoja na mbolea za asili, ni dhahiri kuwa tutakuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na afya zetu. Katika makala haya tutaangazia kwa undani jinsi ya kudhibiti magonjwa na wadudu kwa kutumia dawa za asili shambani.

Madawa haya yasipotengenezwa vizuri na kutumiwa ipasavyo, yanaweza yasifanye kazi ipasavyo. Ni muhimu kuhakikisha kuwa wakulima wanatumia vipimo sahihi na mahitaji sahihi katika utengenezaji.

Inashauriwa kutumia dawa  hizi kama kinga kabla mashambulizi hayajashamiri, kwani ufanyaji kazi wake ni wa taratibu, hivyo ni vizuri kuzitumia kama kinga kuliko tiba.

Sifa za dawa za asili

Upatikanaji wake ni rahisi na hazina  ushindani wa virutubishi na mazao; ni  rahisi kutengeneza na hazihitaji maandalizi ya kiteknolojia,kwa kuwa hazichukui muda mrefu kutengeneza.  Mara nyingi dawa hizi hufukuza wadudu waharibifu zaidi kuliko kuua.

Sifa nyingine ni unafuu wa gharama. Dawa hizi hupatikana bure katika maeneo yanayomzunguka mkulima, ila utengenezaji wa dawa hizi ni lazima upimwe kulingana na gharama zinazojitokeza, pamoja na mgongano wa mazingira, ukilinganishwa na madawa yaliyokiwisha tengenezwa la sivyo wakulima wataendelea kutumia sumu.   Yawe na uwezo wa kuua wadudu walengwa tu bila kudhuru viumbe hai rafiki.

Baadhi ya dawa za asili na jinsi ya kuzitengeneza

Majivu

Weka majivu moja kwa moja kwenye mashina ya mimea michanga baada ya kuotesha ili kuzuia wadudu wakatao mimea michanga.  Majivu huonyesha matokeo mazuri endapo yatachanganywa na mafuta ya taa kidogo.

Pilipili kali

Hii ni moja ya dawa za asili ambazo zimekuwa zikitumika na kwa ufanisi mkubwa. Dawa hii inapotengenezwa na kutumika kwa umakini huwa na ufanisi mkubwa zaidi katika udhibiti wa wadudu na magonjwa.

Chukua gramu 55 za pilipili.  katakata vipande vidogo vidogo kisha chemsha kwa dakika 20 kwenye

maji ya lita tano. Chuja kisha ongeza maji lita 5 Dawa hii huua wadudu wenye ngozi ngumu (mbawa kavu) na laini kama  vidukari, wadudu wa kabichi na wengineo.

Vitunguu saumu

Dawa hii hutumika kufukuza wadudu kutokana na harufu yake.  Chukua gramu 100 za vitunguu, twanga vilainike, changanya na maji lita mbili. Chuja kisha nyunyiza kwenye mimea. Dawa hii pia inaweza kuchanganywa na mojawapo ya dawa za asili, ili kutoa harufu kali itakayofukuza wadudu.

 Tumbaku

Tumia ugoro au chemsha miche 20 ya tumbaku. Dawa hii inazuia wadudu wanaoshambulia mahindi shambani,  wadudu wanaokata miche, kupe, vidukari, viwavi na wengineo. Chukua gramu 500 za tumbaku, changanya maji lita nane  na uchemshe. Chuja baada ya kupoa, ongeza maji lita nane tena na gramu 60 za sabuni ili kuongeza ubora.

Ni muhimu kuwa na tahadhari kwa kuwa   tumbaku ni sumu kwa binadamu na wanyama, hivyo weka mbali

na wanyama wafugwao. Inashauriwa kuvuna mazao siku 4-5 baada ya kunyunyiza aina hii ya dawa.

 Ndulele/ ndula

Chukua matunda ya ndulele 30 au 40 haijalishi yameiva au mabichi. Katakata na uyakamue ili kupata juisi. Ongeza lita moja ya maji, koroga sawa sawa kisha chuja. Ongeza maji lita mbili. Tumia lita moja  ya dawa kwa lita 15 za

Maji kisha  nyunyiza mimea mara mbili  kwa wiki.

Mchicha (kwa ajili ya ukungu)

 Chukua kilo 1 ya mchicha, twanga kisha loweka kwenye maji

Lita moja. Acha ikae kwa saa 12, ongeza sabuni gramu 20, koroga ili sabuni iyeyuke, kisha ongeza maji lita 2 na uchuje. Tumia kwa uwiano wa 1:10 yaani

lita 1 ya dawa kwa lita 10 za maji.

Makala haya kwa  hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu. Mawasiliano na mtaalamu 0765 428877