Dhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii ili uongeze ufanisi kazini

Muktasari:

  • Pamoja na umuhimu wa teknolojia hii, matumizi mabaya au yaliyopitiliza yamekuwa na athari kubwa katika utendaji kazi wa watumiaji.

Mitandao kijamii imekuwa sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Teknolojia imetusaidia sana kuwaweka karibu wale walio mbali huku tukipata taarifa na kuburudika kupitia mitandao ya kijamii inayowezeshwa na simu zetu za mkononi na vifaa vingine vya kielektroniki.

Pamoja na umuhimu wa teknolojia hii, matumizi mabaya au yaliyopitiliza yamekuwa na athari kubwa katika utendaji kazi wa watumiaji.

Kwa watu wengi, mitandao ya kijamii imeendelea kuwatawala badala ya kuitawala na kuathiri utendaji katika shughuli nyingine.

Mutumizi ya mitandao ya kijamii yaliyopitiliza hukera watu wengi sana hasa wale unaowahudumia. Umeshawahi kwenda benki, umechoka upo kwenye foleni ndefu halafu muhudumu kasitisha kutoa huduma huku macho yake yakiwa kwenye simu yake? Basi hapo ndipo utajua namna hali hiyo inavyokera wateja.

Utajuaje kama una matumizi yaliyopitiliza ya mitandao ya kijamii

Wengi ni waathirika wa matumizi ya mitandao ya kijamii, lakini hawajajua kuwa wameshakuwa ‘mateja’ wa teknolojia hiyo. Moja ya namna ya kujua kuwa matumizi yako siyo ya kawaida ni kuangalia kama matumizi ya mitandao ya kijamii ni kitu cha kwanza siku yako inapoanza.

Ukiamka hakuna kingine unachowaza kufanya zaidi ya kufungua WhatsApp, Instagram, facebook au mtandao wowote kuperuzi.

Kitu kingine ni kuwaza kinachoendelea katika mitandao ya kijamii hata kama unashughuli nyingine tofauti.

Ukiona mara kwa mara unapokuwa unafanya shughuli zako mawazo yako yanakuwa kwenye yale yanayoendelea kwenye mitandao, jua hiyo ni dalili kuwa umeshakuwa mtumwa wa teknolojia hiyo.

Dalili nyingine ni kushindwa kujizuia kuingia kwenye mitandao hiyo hata kama unashughuli nyingine za kufanya.

INAENDELEA UK 26

INATOKA UK 25

Kwa kifupi, mitandao ya kijamii inakuwa sehemu ya kila kitu unachokifanya. Wakati ukiendelea kutoa huduma au ukifanya shughuli fulani haiwezi kukamilika bila kuingiliwa na matumizi ya mitandao.

Madhara

Madhara ya matumizi yaliyokithiri ni mengi. Kwanza, ni kupoteza muda ambao ungeutumia katika kazi au shughuli unayoifanya.

Hebu tafakari ni muda kiasi gani unautumia katika mitandao ya kijamii kwa siku halafu tafakari ingekuwa vipi kama muda huo ungeutumia katika kazi au shughuli unazofanya.

Ifamike kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii si kitu kibaya lakini matumizi yaliyo pitiliza ndiyo yanaathari.

Kukosekana kwa umakini katika kazi ni athari nyingine ya utumiaji uliokithiri wa mitandao hii.

Ili kazi ifanywe kwa ufanisi na ufasaha inahitaji mtu anayeifanya azingatie umakini huku akili yake ikiwa tulivu.

Kwa watu wenye matumizi ya mitandao ya kijamii yaliyopitiliza, hili suala ni gumu kwao kwani wakati wanafanya shughuli zao akili yao inawaza yale yanayoendelea kwenye mitandao hiyo.

Matumizi ya aina hii pia huathiri uhusiano katika maeneo ya kazi na wale anaofanya nao kazi.

Kitu ambacho wengi huwa hawakigundui ni ukweli kwamba mara nyingi matumizi ya mitandao ya kijamii huwaleta karibu wale walio mbali na kuwaweka mbali wale walio karibu.

Watu wenye matumizi yaliyopitiliza ya mitandao ya kijamii wapo kwenye hatari ya kuathiri uhusiano mzuri na wale wanaofanya nao kazi.

Ni kitu kinachokera sana ukiwa unazungumza na mwenzako lakini yeye anajishughulisha na simu yake.

Namna ya kukabiliana na matumizi yaliyokithiri

Kwanza, kabla ya kuanza kulishughulikia tatizo hilo, muathirika wa tatizo anatakiwa akubali ukweli kuwa kuna tatizo.

Ni vigumu kukabiliana na tatizo ambalo haujakubali kwamba lipo.

Ukweli huu unatoa wito kwa mtu binafsi kujitathmini na kuangalia mwenendo wake katika matumizi ya mitandao ya kijamii na kuona kama si ya kawaida.

Waweza pia kuwauliza wale walio karibu yako kusikia wanasemaje juu ya matumizi yako.

Endapo unaona au utaona matumizi yako yamezidi kiasi, ni vyema kuchukua hatua mapema kwa kuwa na nidhamu ya matumizi.

Si muda wote lazima ushike simu yako au kifaa chochote cha kielektroiniki kinachoweza kurahisisha matumizi ya mitandao ya kijamii.

Anza kwa kupunguza muda unaoutumia katika mitandao kidogo kidogo; mara nyingi siyo rahisi kuacha ghafla.

Jizoeshe kushika simu yako unapokamilisha shughuli fulani au kipindi cha mapumziko ili upate muda wa kufanya kazi yako kwa umakini na kuondoa muingiliano unaosababishawa na mitandao ya kijamii.

Vifaa vya kielektroniki vinavyotumika vinauwezo wa kudhibiti mtandao unaowezesha matumizi ya mitandao ya kijamii.

Pale unapokuwa unashughuli zako ni vyema kudhibiti au kuzuia mtandao wa intaneti ili jumbe zisiingie kwa wakati fulani.

Njia nyingine ni kujiondoa kwenye makundi yasiyo na tija mtandaoni.

Teknolojia katika mitandao ya kijamii inawezesha watu kuunda makundi yenye malengo mbalimbali.

Ukweli ni kwamba siyo makundi yote huwa na tija na kukujenga kwa namna yoyote ile zaidi ya kupiga soga na kujadili mambo yasiyo na maana na pengine maadili.

Kwa kawaida, akili ya mwanadamu ni ya kidadisi; hata kama kundi halina mambo ya maana ni dhahiri utasukumwa kutaka kujua nini kinaendelea kwenye kundi fulani.

Suala hili husababisha kuwa mtu wa kuzunguka kundi baada ya kundi na kujikuta ukipoteza muda mwingi mtandaoni.

Hakikisha makundi uliyopo una sababu za msingi za kuwa humo na kama kundi halina nidhamu ya kuongoza mijadala si lazima uendelee kuwapo humo.

Jambo jingine la msingi na la kuzingatia; siyo lazima kila ufanyacho, uwazacho au uonacho ni lazima ukiweke mtandaoni.

Jifunze kuyaacha mengine yapite tu.

Kitu kinachowaponza watu wengi mara nyingi ni kuweka picha zao kwenye mitandao ya kijamii kila wanapojisikia kufanya hivyo.

Madhara yake ni kutaka kujua mrejesho wa hicho unachokifanya na mwisho hujikuta walevi wa mitandao kiasi cha kuwapotezea umakini na ufanisi kwenye kazi wazifanyazo.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapakikana kwa 0659 08 18 38, [email protected], www.kelvinmwita.com.