Dira ya maendeleo ya taifa inahusu wananchi pia

Muktasari:

  • Inaaminika kila mwanadamu ana kazi ya kufanya katika kipindi cha kuishi kwake duniani. Mwanadamu asiye na dira na maono anaweza kuondoka duniani bila kujua aliletwa kufanya nini.

Kati ya watu zaidi ya bilioni saba waliopo duniani hivi sasa, hakuna yeyote anayeweza kuwa mbadala wa mwingine. Kila mmoja yupo kwa lengo maalumu.

Inaaminika kila mwanadamu ana kazi ya kufanya katika kipindi cha kuishi kwake duniani. Mwanadamu asiye na dira na maono anaweza kuondoka duniani bila kujua aliletwa kufanya nini.

Kama ilivyo kwa mwanadamu, hakuna nchi inayoweza kuwa mbadala wa nyingine. Nchi isiyokuwa na maono na dira imepoteza mwelekeo. Tanzania ina Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 inayotekelezwa kuelekea uchumi wa kati na viwanda.

Mchakato wa kuiandaa dira hii ulianza mwaka 1994 na kupitishwa rasmi mwaka 1999. Katika uandaaji wake, inaelezwa kuwa uliyashirikisha makundi yote wakiwamo wabunge, vijana, wanawake na wazee ili kuhakikisha inapata ridhaa ya umma.

Hii ni dira ya maendeleo kwa kila Mtanzania si Serikali pekee. Kila mwananchi ana sehemu yake ya kutenda kuhakikisha dira hii inatimia kabla au ifikapo mwaka 2025. Kutokuilewa ni kuibebesha Serikali mzigo mzito ambao kwa vyovyote haitouweza.

Dira ina malengo makuu matano. Mosi ni maisha bora kwa wote. Watanzania wengi wakati huo walipanga ifikapo 2025 kila Mtanzania awe na maisha bora. Pasiwepo umaskini miongoni mwao bali uchumi imara unaomilikiwa na kila Mtanzania kwa sehemu yake.

Pawepo na huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu, umeme, skimu za umwagiliaji na huduma nyinginezo za kiuchumi na kijamii ili kuhakikisha kila Mtanzania anafurahia kuzaliwa na kuishi nchini humu.

Lengo la pili ni kuhakikisha uwapo wa amani, utulivu na umoja. Kabla ya mwaka 1994, Tanzania ilikuwa na vitu vyote hivyo. Walio wengi waliona ni vyema tunu hizi za taifa zikatiliwa mkazo na kuendelezwa.

Ili kuifikia dira hii ndani ya muda ulioainishwa ni lazima pawepo na utulivu wa kisiasa, umoja wa kitaifa na kuvumiliana katika jamii.

Lengo la tatu ni utawala bora. Kuhakikisha kuelekea 2025 panakuwepo na uwajibikaji kwa viongozi wa kisiasa na kiutendaji. Kuendeleza dhana ya uwajibikaji, kupongeza na kuwazawadia wanaotenda vyema, kutokomeza rushwa na maonevu yote katika jamii.

Lengo la nne ni kuhakikisha uwepo wa jamii iliyoelimika na yenye kujifunza. Kila mwanadamu ana fikra hasi na chanya, ila kuweza kupata maendeleo fikra chanya zinatakiwa kuongoza na kumtawala mwanadamu. Pia maendeleo huenda kwa mwanadamu mwenye roho au tamaa ya kutafuta maendeleo.

Jamii iliyoelimika ni ile yenye ustaarabu, kuheshimiana, maadili, uadilifu, uvumilivu, kusamehe, wajibikaji, bunifu, jasiriamali na inayofanya kazi. Kwa kuwa kujifunza hakuna mwisho kila mtanzania anapaswa kujifunza kwa hari ili kutumia matokeo ya kujifunza kwake kuendeleza nchi yake.

Lengo la tano na la mwisho ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi imara na shindani kwa mataifa mengine. Hii ndio nchi ya viwanda anayoihubiri na kuisimamia Rais John Magufuli.

Kabla ya uanzishwaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Tanzania ilikuwa na Dira nyingine mbili. Mosi kupata uhuru, hii ndio ilikuwa ndoto ya kila mtanzania wa kabla ya uhuru. Pili, Dira ya Taifa iliyotokana na Azimio la Arusha mwaka 1967.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ni Dira ya tatu ya Tanzania. Kwa msingi huu Tanzania haijawahi kukosa Dira ya Taifa tangu uwepo wake. Ili kufikia uchumi wa kati na wa viwanda na kuachana na kilimo kisicho cha uhakika ni lazima kila mtanzania awajibike kwenye eneo lake.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 siyo ya Serikali, ni ya watanzania. Ikifikiwa ni watanzania wamefikia, si Serikali. Ikifeli ni watanzania wamefeli. Rais John Magufuli ameonesha mfano wa kuigwa kwa kutekeleza yale yaliyopo kwenye Dira kwa vitendo.

Njia pekee kwa Mwananchi wa kawaida kuielekea Dira ya Taifa 2025 ni kufanya kazi kwa bidii na kulipa kodi. Kwa serikali ni kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara, uwekezaji na utawala wa sheria.

Mwandishi ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.