Monday, March 20, 2017

Duh! Hayatou madarakani tangu Lionel Messi mchanga

 

Mzee Jorge Messi na mke wake, Celia Cuccittini waliokuwa wakiishi kwenye mji wa Rosario kitongoji cha Santa Fe, Argentina, mnamo Juni 24, 1987 walipata mtoto wa tatu waliyempa jina Lionel.

Baba ana asili ya Uitaliano na Uhispania wakati mama ni Muitaliano.

Waliendelea kumlea Messi na alipofika miezi sita, alianza kukaa na kutambaa, si unajua hatua za watoto.

Ilipofika Machi mwaka 1988, Messi akatimiza miezi tisa tangu kuzaliwa.

Baba yake ambaye ndiye meneja wake kwa sasa, alikuwa mfanyakazi wa kiwanda cha kufua chuma cha sumaku.

Messi

Kakuzwa na alipofika miaka 13 akaenda akademi ya Barcelona ambayo ametumia muda mrefu wa maisha yake katika akademi hiyo kabla ya kuingia timu ya wakubwa, Barcelona inayoshiriki La Liga.

Sasa, Messi akiwa na miezi tisa tu tangu kuzaliwa, Machi 10, 1988, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika, CAF, Issa Hayatou akachaguliwa kuwa Rais.

Sasa, Messi kazaliwa, kakua, ana watoto jamaa yuko madarakani na hata juzi aligombea kutaka tena CAF kwa miaka mingine hadi 2021, lakini Ahmad Ahmad akachukua nafasi. Alimchapa kura 34 kwa 20.

Messi kawa staa, Hayatou yumo, Messi katwaa Tuzo za FIFA Ballon d’Or mara tano, Alikuwa mchezaji bora wa Fifa, Hayatou yumo na juzi alitaka tena kuwania muhula wa nane.

Ukiangalia, Messi kazaliwa, kalelewa, kakua na sasa mechezaji tegemeo, lakini Hayatou alitaka nafasi tena apige miaka mingine minne hadi 2021.

Hata hivyo, wajumbe wa CAF ambao ni marais wa vyama na mashirikisho ya soka Afrika, walimtengua Machi 16 ikiwa ni miaka 29 na siku sita.

Sasa Rais wa CAF ni Ahmad Ahmad, Rais wa Shirikisho la Soka, Madagascar, mchezaji na kocha wa zamani wa taifa hilo. Uchaguzi huo ulifanyika kwenye Ukumbi wa Nelson Mandela wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

 

Vilivyomaliza Hayatou

Kati ya vitu vilivyommaliza Hayatou ni baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa na wajumbe wakati wa mkutano Mkuu wa CAF uliofanyia marekebisho ya Katiba, mjini Libreville nchini Gabon wakati wa Fainali za Afrika, Afcon 2017.

Katiba ya sasa ya CAF ambayo awali ilionekana kumpa nafasi Hayatou ya kusonga mbele, imerekebishwa mengi ikiwemo

kuruhusu wagombea huru kutoka nje ya Kamati ya Utendaji kwani zamani ilikuwa tu wajumbe wa Kamati ya Utendaji ndiyo wanaoruhusiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Kigezo cha umri hakikuwa tatizo kwake, miaka 70 ilipitishwa kwa kigezo kwamba atawania lakini agombee kwa vipindi viwili vya miaka nane.

Baadhi ya mabadiliko yaliyofanyika, Kifungu cha 18(4) kuhusu masuala ya uchaguzi, waombaji uongozi na kura.

Kipengele cha 18:2(b); Mgombea Urais wa CAF atakubaliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro endapo tu, ataungwa mkono na vyama vitatu vya soka Afrika ambavyo ni wanachama wa CAF, kikiwemo chama ambacho mgombea anatoka.

Kipengele cha 18 (3), Mgombea Urais wa CAF anatakiwa awe mtu wa mpira moja kwa moja kama mchezaji, kiongozi katika chama cha soka katika taifa lake ambalo ni mwanachama wa CAF, au awe kiongozi Fifa au CAF kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo hadi kuomba urais wa CAF.

 

Mpango wa Ahmad

Ahmad anasema anataka kuleta mageuzi makubwa katika maendeleo ya soka na kurudisha Shirikisho kwa wanasoka wenyewe.

Katika mahojiano na AOIFootball.com amesema mpira unawatu wake na wanafahamika, hivyo atawatumia kuujenga mpira katika maeneo mbalimbali.

Anawataja baadhi ya wachezaji; George Opong Weah, Samuel Osei Kuffour, Kanu Nwankwo, Benni McCarthy, Jay Jay Okocha, Victor Ikpeba, Mark Fish, Lucas Radebe, Moustafa Hadji ambao walilitangaza vizuri bara la Afrika hivyo ni lazima heshima yao ionekane.

“Tatizo lililopo, wachezaji kama hawa na wengine, kazi yao ni kwenda tu uwanjani, jambo ambalo si sawa. Hawa waliliuza bara la Afrika Ulaya likasikika, sasa wakongwe hawa nitawatumia kwa maendeleo ya soka Afrika.”

Bosi huyo wa Chama cha Soka Madagascar alisema CAF ina fedha nyingi kwa maendeleo ya soka Afrika, sasa si kuweka benki tu, fedha lazima zipelekwe kwa wahusika waendeleze soka.

“Nitasimamia utawala bora ambao ndio utakaovuta wadhamini kwa CAF lakini pia lazima tuwekeze katika maeneo ya kukuzia soka. Ni CAF wanaopenda kuweka fedha benki na kuziangalia.”

“CAF itatoa fedha kwa wanachama wake kutengeneza miundombinu kwa maendeleo ya soka na hiyo itasaidia hata kule kwenye maeneo ya watoto,” anasema Ahmad.

 

Infantino ndani

Uchaguzi huo ulishuhudiwa na Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka, Fifa, Gianni Infantino na Katibu Mkuu wake, Fatma Samoura, huku Rais wa Ethiopia Mulatu Teshome akiufungua mkutano huo.

 

Baada ya uchaguzi

Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Ahmad anasema, ataanza kwa kufanya ukaguzi wa hesabu za shirikisho pamoja na kuweka sawa ofisi.

“Nitakwenda Makao Makuu ya Caf kuona kuna nini – baada ya hapo, nitafanya ukaguzi pamoja na kuuitengeneza ofisi,” Ahmad aliiambia BBC Sport.

“Si suala la kuhisi, ni utawala kamili sasa na kufanya uamuzi.”

Aliongeza: “Baada ya kumaliza masuala ya kiutawala na masuala ya fedha, nitazungumza kwa kirefu nini sasa cha kufanya. Hatua kwa hatua, huo ni uamuzi wetu.”

Ahmad, ambaye hakuwa maarufu kabla ya kutangazwa mapema Januari, alichaguliwa, lengo hasa ni kuleta mabadiliko ndani ya CAF.

Kikubwa ni kuleta haki, usawa na uwazi ndani ya Caf na kuahidi kufanya kazi ya kuijenga soka ya Afrika kwa kuanzia na vijana.

Ahmad alichanganyikiwa kwa furaha baada ya ushindi na BBC Sport ilifanya kazi hata kupata mahojiano yake.

Dennis Idrissa, aliyekuwa meneja kampeni wake, alisema Ahmad alichanganyikiwa, alikuwa haamini kwani wakati kura zinapigwa, matokeo kutangazwa, muda wote alikuwa nje ya ukumbi wa mikutano.

“Ahmad aliniambia nisikilize na kisha niende nikamwambie kilichotokea,” Idrissa aliiambia BBC Sport.

“Muda wote huo, Ahmad alikuwa nje ya ukumbi – alikuwa haamini, alichanganyikiwa fulani. Nilipopata matokeo nikamfuata na kumwambia, wewe ndiye Rais mpya wa CAF.’

“Akasema: ‘Kweli? Dennis, ni kweli? Nikarudi tena ndani. Nikatoka na kumchukua kumleta ukumbini.

“Tukamnyanyua juu juu mabegani pamoja na Rais wa Chama cha Soka Djibouti. Ulikuwa wakati mmoja wa aina yake maishani mwangu. Tulipambana sana siku hiyo.”

-->