Tuesday, November 21, 2017

ELIMU NA MALEZI : Umuhimu wa huduma ya unasihi kwa wanafunzi-1Christian Bwaya

Christian Bwaya 

By Christian Bwaya

        Unasihi si huduma iliyozoeleka katika mazingira yetu ya Kiafrika.

Mara nyingi tunaposikia maneno kama ‘ushauri nasaha’ mawazo yetu yanakwenda kwa watu wenye matatizo ya akili au waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

Hata hivyo, huduma hii imekuwa sehemu ya maisha yetu kwa muda mrefu.

Tunafahamu, kwa mfano, tumekuwa na mila na desturi katika jamii zinazolenga kuwasaidia vijana wa umri fulani kujitambua na kutambua nafasi waliyonayo katika jamii.

Utaratibu huu wa wazee na watu wenye busara kuwaongoza vijana kujitambua, kimsingi ni aina ya unasihi.

Hata katika maisha yetu ya kila siku, tuna mazoea ya kutafuta ushauri kwa watu wanaoaminika tunapotaka kufanya maamuzi.

Ndiyo maana si ajabu kwa mfano, mtu anayefikiria kununua kiwanja mahali fulani, kutafuta watu anaoamini wanaweza kumsaidia.

Katika mazingira ya shule, unasihi hivi sasa una nafasi ya kipekee pengine kuliko ilivyopata kuwa hapo zamani.

Hii inatokana na ukweli kuwa mafanikio ya mwanafunzi darasani, kwa kiasi kikubwa yanategemea maisha yake ya kawaida nje ya darasa.

Kwa mfano, ili mwanafunzi aweze kusoma kwa utulivu, uhusiano wake na familia yake lazima uwe mzuri.

Mwanafunzi anayetoka kwenye familia yenye migogoro na misukosuko, anakuwa kwenye mazingira yanayoweza kuathiri uzingativu wake darasani.

Sambamba na hilo, kuna changamoto ya wazazi wengi kuwaachia walimu jukumu la kuwalea watoto wao.

Walimu nao wakati mwingine shauri ya idadi kubwa ya wanafunzi, hushindwa kupata nafasi ya kutosha kubeba jukumu hilo la malezi ipasavyo.

Mwanafunzi huyu anayesoma kwenye mazingira ya namna hiyo, hupita kwenye mabadiliko mengi ya kimwili yanayoweza kuathiri mtazamo na tabia yake kwa jumla. Bila kupata msaada mzuri, anaweza kupata shida kufanya vizuri darasani.

Jitihada za Serikali

Serikali imefanya jitihada kadhaa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata msaada wa kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mfano, mwaka 2000, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni ilianzisha mpango unaolenga kukabiliana na changamoto ya Ukimwi.

Waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2000 ulikuwa na madhumuni ya “kuwawezesha mwanafunzi wa shule na mfanyakazi wa wizara kufanya uamuzi wa busara, kuhusu tabia na mwenendo katika mahusiano ya ujinsi.”

Waraka huo uliolenga shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, ulikuwa na lengo kuu la “kuwaelimisha na kuwashauri wanafunzi na wafanyakazi, ili wajenge na wakuze tabia na mwenendo utakaozuia kuambukizwa na kuendea virusi vya Ukimwi na magonjwa ya zinaa kati yao na katika jamii.”

Kama inavyoonekana lengo hasa la wizara wakati huo lilikuwa kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi.

Wakuu wa shule na vyuo vya ualimu walielekezwa kuunda kamati ya malezi na elimu dhidi ya ugonjwa huo.

Pia, wizara iliziagiza shule na vyuo vya ualimu kutenga siku maalum kwa ajili ya kuwaelimisha wanafunzi na jamii nzima ya shule kuhusu mambo yanayohusiana na maambukizi ya VVU.

Kazi kubwa ya kuwaelimisha wanafunzi ilifanywa na walimu na wakufunzi, ingawa wakati mwingine watalaamu wengine walikaribishwa kutoa mada.

Hii kwa hakika, ilikuwa hatua nzuri ya wizara katika kutambua ukweli kwamba maisha ya mwanafunzi nje ya darasa yanahusiana kwa karibu na maendeleo yake kitaaluma.

Mpango huo, hata hivyo, ulikuwa sehemu ya mpango wa mapambano ya kitaifa dhidi ya Ukimwi na haukulenga kukabiliana na changamoto nyingine zinazomkabili mwanafunzi.

Masuala kama mwanafunzi kujitambua, kutengeneza malengo yake ya ajira aipendayo, kukabiliana na mabadiliko yanayotokea mwilini mwake na hata kwenye jamii kwa ujumla hayakupewa uzito.

Matokeo yake nidhamu iliendelea kuwa changamoto kwenye shule zetu na vitendo vya wanafunzi kushiriki vitendo vya jinai na kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya, pombe na uasherati, viliendelea kushamiri.

Waraka wa elimu namba 11

Pengine kwa kutambua upungufu huo, Waraka wa elimu namba 11 wa mwaka 2002, ulianzisha huduma za malezi na ushauri nasaha katika taasisi za elimu.

Kupitia waraka huo uliosainiwa na Kaimu kamishna wa Elimu Mei 2, 2002, wakuu wa shule na vyuo vya ualimu walielekezwa kuanzisha kamati ya malezi na kuteua mwalimu mlezi na mshauri.

Kazi kubwa ya mwalimu mlezi zilizoainishwa kwenye waraka huo ni pamoja na kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi wote na kuzungumza na wanafunzi kuhusu ukuaji wao na mabadiliko wanayoyapata katika miili yao kabla na baada ya kupevuka.

Pia, kazi nyingine iliyoainishwa kwenye waraka huo ni, “kufanya mkutano na wanafunzi/wanachuo ili kujadiliana nao kuhusu matatizo wanayokabiliana nayo kielimu, kiafya na kijamii na kuwasaidia kupata mbinu za kukabiliana na matatizo hayo.”

Pamoja na nia njema ya mpango huo kutambua na kushughulikia matatizo mapana yanayomkabili mwanafunzi, changamoto ikawa kukosekana kwa wataalamu wa unasihi shuleni na vyuoni, ambao wangeweza kutekeleza kazi hiyo kwa ufanisi.

Sababu mojawapo ni vyuo vyetu kutokuwa na programu za shahada na stahahada zinazoandaa wataalamu waliobobea katika eneo la unasihi.

Ingawa unasihi na saikolojia ni sehemu ya mtalaa wa mafunzo ya jumla ya walimu kwa kila ngazi, bado ufanisi wake umekuwa na changamoto.

Katika vyuo vingi mathalani, somo hili hufundishwa na wakufunzi ambao wao wenyewe hawajawahi kufanya unasihi.

Katika mazingira kama haya, inakuwa vigumu kwa mwanafunzi wa ualimu kupata ujuzi madhubuti, utakaomsaidia kufanya kazi vizuri na wanafunzi wake.

Pengine kwa kuelewa kikwazo hicho, ilipofika mwaka 2007, iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na mradi wa kuzuia na kuelimisha wanafunzi kuhusu masuala yanayohusiana na VVU/Ukimwi (PASHA), iliandaa mwongozo wa kuendeshea mafunzo ya unasihi kwa walimu shuleni.

Mwongozo huo, pamoja na mambo mengine, ulilenga kupanua uelewa wa walimu kuhusu mbinu za kufanya unasihi, afya ya uzazi na VVU/Ukimwi, tabia hatarishi na elimu ya maisha. Itaendelea wiki ijayo     

-->