ELIMU NA MALEZI : Yatambue madhara ya adhabu ya bakora

Muktasari:

  • Kwa jumla, tunaweza kusema mzazi aliyelelewa kwa fimbo hujikuta na yeye akiamini fimbo ndiyo suluhu ya matatizo ya kinidhamu anayoyaona kwa mwanawe. Aidha, mzazi mwenye hasira kwa sababu yoyote, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia fimbo anapofikiria kutoa adhabu.

Ingawa wazazi wengi huwachapa watoto wakiamini wanafanya hivyo kwa lengo la kuwaadabisha, wiki iliyopita katika safu hii tulibainisha sababu zilizojificha.

Kwa jumla, tunaweza kusema mzazi aliyelelewa kwa fimbo hujikuta na yeye akiamini fimbo ndiyo suluhu ya matatizo ya kinidhamu anayoyaona kwa mwanawe. Aidha, mzazi mwenye hasira kwa sababu yoyote, anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia fimbo anapofikiria kutoa adhabu.

Matumizi ya fimbo katika muktadha huu, ni namna ya kujisaidia yeye mwenyewe kukabiliana na hasira na msongo wa mawazo na siyo kumsaidia mtoto kama inavyoaminika.

Ndiyo kusema, mzazi anapokuwa na changamoto zinazomkosesha amani, iwe ni hali duni ya kiuchumi, migogoro ya ndoa, kutokuwa na utulivu wa maisha; anakuwa na uwezekano mkubwa wa kutumia adhabu kama namna ya kujituliza bila yeye mwenyewe kung’amua.

Kuna jambo muhimu la kuzingatia kabla hatujatazama madhara ya kumwadhibu mtoto. Ingawa watoto wote bila kujali jinsia ni waathirika wa adhabu ya viboko katika jamii, watoto wa kiume huwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kuchapwa kuliko wenzao wa kike.

Imejengeka imani kuwa adhabu kwa mtoto wa kiume ni lazima iwe nzito na yenye kuleta maumivu zaidi kuliko ile anayopewa msichana. Kwamba unapomwadhibu mtoto wa kiume unaweza kutumia mabavu zaidi kuliko unapomwadhibu mtoto wa kike.

Katika mazingira ya shule, mathalani, watoto wa kike huchapwa viganjani wakati watoto wa kiume wanachapwa kwa namna inayowadhalilisha zaidi. Tunaweza kuwa na tafsiri nyingi kuelezea tofauti hii. Lakini mojawapo, jamii inaelewa maumivu yanayoambatana na mapigo ya fimbo na huzitumia kama namna ya kukuza fikra za ubabe na mabavu kwa watoto wa kiume.

Fimbo zinakuwa namna fulani ya kuendeleza mfumo dume kwenye jamii. Hata hivyo, viboko vimethibitika kuwa na athari kwa watoto. Tukiachana na madhara ya mwili yanayoweza kutokana na majeraha, yapo matatizo makubwa matatu ya kisaikolojia.

Huharibu uhusiano na mtoto

Adhabu ya fimbo, kama tulivyoona, ina uhusiano mkubwa na hasira anazokuwa nazo mzazi. Tunafahamu mtu aliyekasirika anaweza kufanya lolote ikiwamo kutumia nguvu nyingi kupita kiasi, kuliko ambazo angetumia kama angesubiri hasira zipungue.

Mara nyingi, mtu anapotumia fimbo hufanya hivyo akiwa na hasira. Kwamba anayeadhibiwa amefanya kosa linalostahili kichapo, hufanya adhabu iwe ya papo kwa hapo. Hakuna kusubiri.

Matokeo yake adhabu hudhuru uhusiano wa mzazi na mtoto. Mtoto anayechapwa, kwa mfano, hujiona kama mtu asiye thamani kwa mzazi wake hasa kama mzazi hana tabia ya kukarabati uhusiano wake upya na mwanawe baada ya kumchapa.

Wakati mwingine, wazazi huwachapa watoto wao bila staha. Mtoto huchapwa hadharani mbele ya watu mfano rafiki zake na wadogo zake. Kuchapwa katika mazingira ya namna hii humfanya ajisikie kudhalilishwa na kuonewa.

Pia, wazazi wengine hawakumbuki kukaa na watoto baada ya adhabu kufafanua sababu iliyowalazimu kuwachapa na kujadili tabia mbadala. Mzazi mwenye uwezo wa kufanya mazungumzo ya namna hii baada ya fimbo, maana yake angeweza kabisa kuachana na mpango wa fimbo tangu awali.

Kwa hiyo, ni nadra mzazi aliyemchapa mwanawe kufikiria kurudisha uhusiano baada ya adhabu.

Kukosekana kwa ukaribu huu baada ya adhabu ya fimbo, hufanya watoto waachwe na majeraha moyoni ambayo, kama hatua hazitochukuliwa, huathiri mitazamo ya watoto na hata namna wanavyowachukulia wazazi wao.

Hukuza tabia ya usugu

Fimbo zina tatizo la kuzoeleka. Kadri inavyotumika kumsababishia maumivu mtoto, ndivyo inavyobidi iwe kali zaidi. Isipokuwa kali na nzito haiwezi tena kuendelea kumfanya mtoto apate maumivu yanayotarajiwa.

Kama mtoto alikuwa akichapwa fimbo mbili ndogo, baada ya muda, fimbo mbili hazitoshi kumpa wasiwasi. Anajua akikosea, atapata fimbo mbili na mambo yataisha.

Kwa kuwa mzazi hana namna nyingine ya kumrudi mwanawe, mtoto hufanya kosa lilelile. Mzazi naye hutumia mbinu ileile ya kumsababishia mtoto maumivu akifikiri anaweza kumjengea hofu ya kutorudia alichokifanya. Kwa mshangao wake, mtoto hufika mahali hatetemeki kama ilivyokuwa awali.

Suluhu inakuwa ni kuongeza mapigo ili kutengeneza woga unaoonekana kupotea. Kadri mapigo yanavyozidi kuongezeka na kuwa makali zaidi, ndivyo adhabu inavyoendelea kupoteza maana yake na kugeuka kuwa ugomvi kati ya mzazi na mtoto.

Watoto wanaozoea hali ya kupigwa, ni watu sugu hata katika uhusiano wao na watu wengine. Wengi wanapokuwa watu wazima hukosa uwezo wa kujua hisia za wengine kwa sababu wamekulia kwenye mazingira yaliyowazoeza kupuuza hisia zao wenyewe.

Hufundisha ubabe

Fimbo humfundisha mtoto kutumia nguvu katika kutatua migogoro anayokutana nayo. Watoto wanaochapwa, mara nyingi huwa ni wagomvi katika maisha halisi. Hujikuta wakiwa na mazoea ya kupigana na wenzao na hata watu wengine kama namna ya kutatua matatizo yao.

Tabia ya ugomvi anakuwa amejifunza kwa wazazi wake mwenyewe. Amemwona baba akishika fimbo kushughulikia tatizo linalojitokeza na yeye atamshika shati mtu mwingine anayemkosea. Hawezi kuona njia nyingine bora zaidi. Mtoto wa nyoka anaendelea kuwa nyoka.

Matokeo ya mazoea haya ni kumfanya awe mtu wa mabavu, mchokozi kwa wenzake, asiyeweza kuelewa hisia za wengine na mwisho wake na yeye wenyewe hugeuka kuwa mtu anayeunga mkono fimbo kwa watoto wake. Ni namna fulani ya kurithisha utamaduni wa ubabe.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com