Echesa: Nikikumbuka nilivyowanyonga Yanga nacheeka

Muktasari:

  • Echesa raia wa Kenya, katika mahojiano maalumu jijini Nairobi anasema amecheza mechi nyingi, lakini mechi ya Simba na Yanga ambayo Simba ilipiga mabao 4-3, hatoisahau maishani.

 Kati ya wachezaji ambao hawasahau historia ya soka Tanzania ni straika wa zamani wa Simba, Hilary Echesa, anasema akikumbuka anacheeka.

Echesa raia wa Kenya, katika mahojiano maalumu jijini Nairobi anasema amecheza mechi nyingi, lakini mechi ya Simba na Yanga ambayo Simba ilipiga mabao 4-3, hatoisahau maishani.

Echesa akiitumikia Simba SC alipachika bao la ushindi dhidi ya Yanga kwenye debi la Dar es Salaam mwaka 2010.

“Ninahisi ni kama jana. Nimecheza nchi nyingi lakini sijapata mazingira matamu kama yale Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

“Wakati huo nilikuwa na Wakenya wenzangu Jerry Santo na Mike Baraza waliokuwa wamesajiliwa Simba.

“Ilikuwa mechi ngumu, mara tatu tuko nyuma ghafla bin vu Okwi (Emmanuel) akanitolea pasi, nikaiunganisha hadi wavuni, tena nilifunua dari.

“Nilifurahi kiasi cha kwamba nilivua jezi bila kufahamu tayari nilikuwa na kadi ya manjano na ndivyo mechi yangu ilivyoisha nilipopigwa kadi nyekundu.

“Sasa angalia, wakati nakwenda katika chumba ya kubadilisha mavazi, refa si akamaliza mchezo, mbio nikarudi uwanjani kuzidi kushangilia ushindi huo mnono.

“Yanga walinywea sana, walichoka maana hawakuamini kama nitawatungua. Walijua kuwa mchezo utamalizika kwa sare ya 3-3, nikawatandika lile bao.”

Echesa anaamini kwamba wachezaji wa Kenya bado wanaweza kuonyesha makali yao nchini Tanzania licha ya tetesi za hivi karibuni kwamba wengi wanashindwa sababu ya nguvu za gizani.

“Wapo wachezaji kama Allan Wanga (Azam FC), Joseph Shikokoti na Paul Kiongera (Simba SC) ni baadhi yao walioteseka sana Bongo.

“Nafikiri kila kitu kipo akilini mwa mtu. Watanzania wanachukulia soka lao siriaz na pindi tu utakaposaini klabu mojawapo kubwa utakuwa nyota wa mjini.

“Si magazeti, si mashabiki wote watakufuata ni wajibu wako kujichunga. Mfano Ambani (Boniface) alipachika magoli mengi sana Ligi Kuu ya Tanzania kumaanisha alifahamu kazi yake na aliiaminika, mambo mengine ya nje ya uwanja ni stori tu.”

Akizungumzia Wakenya wanaocheza soka nje, Echesa anasema: “Zaidi ya Wakenya 20 wanapiga soka la kulipwa nje ya nchi. Ni mazingira tofauti sana na nyumbani kila mtu akikutana na utamaduni tofauti inakuwa ni miongoni mwa changamoto nyingine kwa mchezaji husika.

Echesa anayekipiga Sofapaka FC inayoshiriki Ligi Kuu hivi sasa. Ni huyu Echesa mmoja amesafiri mataifa kadha wa kadha na lengo la kusaka posho.

“Miongoni mwa nchi nilizocheza, sitasahau maisha yangu nchini Damascus. Hata sikumbuki ni klabu gani nilichezea huko lakini maisha yalikuwa magumu kweli. Ndani ya miezi mitatu niliyokuwa huko, lugha ngumu pia ubaguzi wa rangi,” anasimulia Echesa (36).

“Singapore, Indonesia, Malaysia na mataifa mengine angalau maisha hayakua mabaya. Kule hata nilijifunza maneno mawili matatu ya lugha yao na nilikawia sio kama Damascus.

“Kitu cha kuhuzunisha sana nje ni uende majaribio na Wakenya wenzako kisha wafeli.

Cheki niliitwa Malaysia majaribio ya majuma mawili katika klabu ya Police de Raja Malaysia na wenzangu Eric Muranda, John Baraza, Abdi Simba na Francis Chinjili.

Ni mimi tu nilikabidhiwa kandarasi wengine hawakuwahi, kwa kweli iliniuma sana lakini bahati nzuri walipata klabu nyingine.”

Katika maisha ya mchezaji, Echesa anakiri wakala ni mtu muhimu sana. Ni wajibu wake kumtaftia mchezaji wake klabu alimradi umuheshimu na kumwamini.

“Kilicho cha msingi ni kwamba mnaelewana na wakala wako na unaheshimu kandarasi mlionayo kati yenu.

“Wakati mwingi wachezaji hukosana na mawakala wao kwa sababu ya kutoelewana lakini kwangu sikuwahi kukosana naye tangu nimpate kupitia mwenzangu Muranda (Eric). Wakala Ahmad alinifaidi sana wakati wangu nikiwa nje,” Echesa anasema.

Kwa sasa Echesa anaishi maisha mazuri tayari amejenga kwao na kuanzisha biashara kadhaa