Elimu bure nchini ikitekelezwa vibaya linaweza kuwa bomu

Muktasari:

  • Mgombea wa Chadema aliyekuwa akiungwa mkono na vyama mbadala vya CUF, NCCR na NLD kupitia muungano wa Ukawa, Edward Lowassa alisisitiza kuwa Ukawa ikishinda Serikali yake ingetoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.

Wiki hii Rais John Magufuli aliwaita mawaziri wanaohusika na utoaji wa elimu msingi nchini na kuwaeleza anavyosikitishwa na namna wazazi wanavyolipishwa michango mbalimbali ambayo inaathiri uwezo wao kiuchumi na wakati mwingine kushindwa kulipa michango hiyo na watoto wao kutishiwa kufukuzwa shule.

Rais akasisitiza kuwa kinachotendeka ni kinyume na yale ambayo aliyaagiza wakati anatangaza mpango wa utoaji wa elimu bure kwa shule zote za msingi za umma nchi nzima. JPM amekwenda mbali zaidi, ameeleza kuwa atawachukulia hatua watendaji wenye mamlaka mbalimbali kuanzia wizarani hadi ngazi za shule ikiwa watajihusisha na mkakati wa kuweka michango kwenye shule – na mwisho akaelekeza kuwa michango yote kama ni ya lazima, ipokelewe na wakurugenzi wa halmashauri na siyo walimu.

Ilani za uchaguzi 2015

Kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, masuala ya utoaji wa elimu bure yalikuwa moja ya ajenda iliyopigiwa debe na kutangazwa zaidi. Chama cha CCM na mgombea wake JPM kiliweka mkazo kuwa kikishinda kitatoa elimu ya msingi bure yaani darasa la kwanza hadi kidato cha nne.

Mgombea wa Chadema aliyekuwa akiungwa mkono na vyama mbadala vya CUF, NCCR na NLD kupitia muungano wa Ukawa, Edward Lowassa alisisitiza kuwa Ukawa ikishinda Serikali yake ingetoa elimu bure kwa wanafunzi kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.

Wapiga kura walibaki na chaguo, wanataka nini, elimu ya msingi bure au elimu bure ya shule ya msingi hadi chuo kikuu. Wakaamua kuchagua elimu ya msingi bure.

Ukweli halisi ni kuwa elimu bure kwa shule ya msingi ni jambo linalowezekana kwa asilimia 100 na elimu bure kwa shule za msingi hadi chuo kikuu ni jambo linalowezekana kwa asilimia 100. Baada ya Serikali ya JPM kuanza kutoa elimu ya msingi bure, Serikali hii haijawa ya kwanza, zipo nchi nyingi sana duniani zinazotoa elimu ya msingi kwa utaratibu huo.

Hata kama Lowassa angelishinda urais 2015 kupitia Ukawa, Serikali yake isingelikuwa ya kwanza katika kutoa elimu bure kutoka shule za msingi hadi chuo kikuu. Hapa nina maana kuwa tunazo nchi darasa ambako tunaweza kujifunza walifanikiwaje kutoa elimu bure kwenye ngazi walizoziamua.

Kipimo ni utekelezaji

Ikiwa elimu ni bure kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha peke yake au kutoka darasa la kwanza hadi chuo kikuu – mambo yote mawili yana changamoto zake kwenye utekelezaji.

Changamoto kuu ambayo ndiyo kiini cha makala hii ni bajeti ya utekelezaji. Mathalani, kama Lowassa angelikuwa rais kupitia Ukawa na Serikali yake ikasomesha wanafunzi bure kutoka shule za msingi hadi chuo kikuu – Serikali hiyo ya Ukawa ingelihitaji bajeti kubwa zaidi ili kusimamia jambo hilo. Bajeti hiyo ingeliweza kuwa mara tatu hadi tano ya bajeti inayotumika kuwasomesha watoto bure katika ngazi ya shule ya msingi na sekondari tu.

Ndiyo kusema kuwa hii ya Ukawa ilihitaji gharama za hali ya juu zaidi, lakini nataka kusema kuwa ingeliwezekana kama ambavyo hii inavyowezekana. Na lazima tuwe wazi, kwamba mifumo yote hii ya utoaji wa elimu bure, ule wa Ukawa na huu wa CCM ingelishindikana au kusuasua ikiwa kungekuwa na bajeti kiduchu kwenye utekelezaji.

Kwa lugha rahisi, tunakubaliana kwamba kitovu cha utekelezaji wa programu yoyote ya utoaji wa elimu bure mahali popote, ni bajeti au pesa za kugharamia yale ambayo yangelilipiwa na wazazi na wadau.

Kwa nchi kama zetu ambazo wanasiasa nyakati za kampeni wanasisitiza jambo fulani litakuwa bure kwa asilimia 100 – kunapaswa kuwa na mipango ya kutosha ya utekelezaji ambao hauna shaka. Maana ukishawatoa wazazi kwenye kuchangia jambo, lazima uwarudishe kwa utaratibu maalumu na maelezo ya kutosha.

Tatizo la msingi

Tatizo la msingi linalojitokeza katika mfumo wa sasa wa utoaji elimu bure ni mzigo wa gharama, gharama zimezielemea shule na ruzuku au fedha zinazotumwa na Serikali kwenda kwenye kila shule ni hazitoshi na haziendani na mahitaji halisi ya msingi ya shule husika. Zamani ilikuwa rahisi, jambo lolote likiishinda shule, bodi ya shule au kamati fulani ya shule inaomba kibali na wazazi wanachangishwa.

Utaratibu wa zamani ulizua manung’uniko mengi ndiyo maana kila chama kikubwa kikaahidi kuanza kutoa elimu bure. Zamani ilikuwa mtoto wa darasa la kwanza anaandikishwa kwa makumi elfu kadhaa ya pesa. Wazazi walikwazwa na kushindwa kupeleka watoto shule na mpango wa kitaifa wa kuondoa ujinga na kulifanya taifa lisiwe na watoto wasioenda shule ulikwama.

Tangazo na maamuzi ya kutoa elimu bure ni jambo jema kwelikweli. Lakini, sote tunafahamu kwamba ukifanya jambo jema kwa njia mbaya, wema wake unaanza kuharibika, kama siyo muda huohuo, baadaye utayaona madhara yake.

Kinachotokea leo ni madhara ya Serikali kutopeleka fedha za kutosha kwenye shule za msingi na sekondari. Walimu wakuu, waratibu elimu kata, maofisa elimu wa wilaya na mikoa, kamati za shule na bodi za shule – hawajui watatatuaje matatizo ya shule ambayo ni ya lazima, lakini hayagharamiwi na Serikali. Nitatoa mifano miwili tu.

Mifano hai

Mfano wa kwanza ni mlinzi au walinzi wa shule. Msomaji anaweza kuona mlinzi ni jambo dogo tu, halina uzito kabisa. Lakini, nataka kuwaambia kuwa kwa walimu na usimamizi wa shule, uwepo wa mlinzi ni jambo la lazima kwa asilimia 100. Shule ikikaa bila mlinzi, watu wenye nia mbaya haraka sana wataivamia na kupora vitabu vyote, vifaa vya mahabara, nyaraka, samani za shule na vinginevyo. Lakini si hivyo tu, watu wabaya wanaweza kuichoma na kuiharibu shule. Mlinzi tu!

Sasa inapotokea Serikali haipeleki pesa ya mlinzi kwenye shule na shule inakatazwa kuwachangisha wazazi kwa lazima ikitaka wachange kwa hiari wakati sote tunajua kwa hiari si rahisi hata mzazi mmoja kuwa anachanga kila mwezi – kwenye mazingira kama hayo, walimu wakuu na walimu wafanye nini?

Maana tumewakataza kusimama, tumewakataza kuinama, tumewakataza kukaa na tumewakataza kurukaruka.

Mfano wa pili ni masuala ya mitihani ya kujipima. Ili shule yoyote iwe na mafanikio na matokeo ya hali ya juu, lazima iwe na uwezo wa kutoa mitihani ya majaribio mara kwa mara. Miaka ya 1990 ambapo nilikuwa shule ya msingi, mfumo wa kupewa majaribio ya darasani kwa njia ya kuandikiwa ubaoni ulikuwa umepitwa na wakati, miaka ya mwishoni mwa 1990 mfumo ule ulikufa kabisa, ikawa hata majaribio ya darasani mnachangia karatasi na mitihani inachapwa – kila mwanafunzi anafanya mtihani wake peke yake.

Leo hii fedha zinazotumwa na Serikali kwenye shule, hazina bajeti ya kugharamia karatasi kwa ajili ya mitihani ya mara kwa mara ya majaribio, ujirani mwema na mingineyo. Katika utaratibu wa sasa tunataka walimu na shule zifanyeje? Ziache kabisa kutoa majaribio hayo? Au zianze kuyaandika ubaoni kama miaka ya 1980? Hivi tunakwenda mbele au tunarudi nyuma.

Kinachotakiwa kufanyika

Serikali yetu inapaswa kuunda tume. Iunde tume maalumu iende ikabaini changamoto za gharama za utoaji wa elimu bure. Kupitia majibu ya tume hiyo, Serikali ipitie upya viwango vya fedha zinazopelekwa kwenye shule, viwango vipya vitolewe vikijumuisha gharama zote za mahitaji ya msingi kama vile walinzi, karatasi za mitihani ya kila wiki, ya kila mwezi, ya robo mwaka, ya ujirani mwema na kadhalika. Gharama za namna hii na nyingine nyingi zipewe uzito mkubwa na ziwe sehemu ya gharama ambazo Serikali itazibeba.

Hii ndiyo njia ya pekee ambayo itatumiwa na Serikali ili kufanya taifa letu litambe kuwa linatoa elimu bure. Kinyume chake ni tutatengeza manung’uniko ya walimu na wanafunzi, walimu watashindwa kufikia malengo ya mipango kazi yao kwa sababu ya uchache wa rasilimali za kuongeza ufanisi kwenye malengo hayo – na matokeo yake wanafunzi wetu watakosa ufaulu na uelewa wa kutosha kwa sababu walimu walikatishwa tamaa na maamuzi mazuri ya kisiasa yenye utekelezaji wa kisiasa pia, badala ya maamuzi mazuri ya kisiasa yanayotekelezwa kitaaluma.

Wanasiasa wa nchi yetu wanapaswa kujua kuwa elimu haiwezi kutumikia siasa, masuala ya elimu huhitaji kutafitiwa na kupimwa kwenye mizania yenye macho matatu

Julius Mtatiro ni Mchambuzi wa Mfuatiliaji wa Utendaji wa Serikali barani Afrika; ni Mtafiti, Mwanasheria, mwanaharakati na ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama cha Wananchi CUF. Simu; +255787536759; [email protected])