Elimu ina watendaji wengi wasio na tija

Muktasari:

Muda mwafaka wa kumpima kiongozi bora si wakati wa tukio la sherehe na furaha, bali wakati changamoto na sintofahamu.

Muda mwafaka wa kumpima kiongozi bora si wakati wa tukio la sherehe na furaha, bali wakati changamoto na sintofahamu.

Elimu yetu imepitia katika changamoto nyingi na bado inakumbana na changamoto nyingi.

Katika kupitia changamoto zote hizo, je, umeshapima na kufahamu uongozi wetu katika elimu una ubora gani?

Uongozi wetu katika elimu umetuvushaje katika changamoto na una mwenendo gani wa kutuondoa nje ya changamoto hizo?

Uongozi katika elimu umetuvushaje katika kukabiliana na mazingira mabaya ya kujifunza na kufundisha shuleni, kushuka kwa hadhi ya mwalimu, uhaba wa madawati, kutokuwepo kwa vitabu vya kiada, uhaba wa vitabu vinavyotumika, upungufu wa walimu wa sayansi, matumizi ya vyeti bandia katika ualimu na kudahili ‘vilaza’ Msururu ni mrefu.

Kushuka kwa kiwango cha elimu sio tena mjadala, ni ukweli tunaoishi nao kila siku. Pengine tumeuzoea kiasi kwamba wanaopigia kelele suala hili wanaonekana wanapoteza muda wao. Tuendelee kupoteza muda na kujiuliza, kushuka kwa elimu tatizo ni nini hasa, wapi tulipokosea?

Kama inavyoelezwa na wasomi wengi kuwa tatizo kubwa la kuwapo maendeleo duni katika bara la Afrika ni suala la uongozi. Je, sababu hiyo ya uongozi haiwezi kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo duni na kushuka kwa kiwango cha elimu nchini?

Uongozi wa elimu nchini unakabiliwa na changamoto nyingi kubwa zikiwa muingiliano na kutoeleweka bayana majukumu ya kiutendaji kati ya taasisi na watendaji wa serikali, utitiri wa vyeo visivyokuwa na tija, udhaifu na kutokuwa na uwazi katika taratibu za uteuzi mbalimbali wa viongozi na udhaifu wa viongozi weteule kusimamia elimu.

Mfano si rahisi kusema kwa hakika uendeshaji wa elimu ya msingi na sekondari kwa sasa unaratibiwa na wizara gani kati ya Tamisemi na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Katika wizara hizi zote mbili kuna wakurugenzi wanaoshughulikia elimu ya msingi na elimu ya sekondari. Wakati Tamisemi kuna wakurugenzi wawili wasaidizi wa sekondari na idara ya msingi walio chini ya Mkurugenzi Uratibu Elimu, Wizara ya Elimu kuna wakurugenzi wawili wa sekondari na msingi.

Zaidi ya hapo wakati elimu ya sekondari na msingi zipo chini ya halmashauri na manispaa, kuna mtu anayeitwa ofisa elimu mkoa. Huyu anashughulika na kitu gani hasa kama walivyo wale wakurugenzi wa sekondari na msingi waliopo wizara ya elimu?

Kama vile haitoshi, Wizara ye Elimu ina mkurugenzi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi na hapo hapo pia tuna Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ambayo nayo ina mkurugenzi wake.

Sasa huyu mkurugenzi wa wizarani kazi yake ni kuisimamia VETA tu au ana shughuli nyingine? Hii ni sawa katika wizara ya Fedha na Mipango kuwe na Mkurugenzi wa TRA au katika Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi kuwe na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari!

Wakati huko wengine wanapigania kuondoa urasimu katika utendaji wa umma, sisi ndio kwanza tunauimarisha tena kwa kuharibu rasilimali chache tulizonazo ambazo zingeweza kwenda kusaidia na kuhudumia sehemu zenye mahitaji zaidi.

Vyeo visivyo na tija

Sekta ya elimu imejawa na utitiri wa viongozi mpaka ngazi za chini za uongozi. Katika ofisi za maofisa elimu wa mikoa pia kuna maofisa taaluma wa mikoa na maofisa wengine wengi ambao majukumu yao hayaeleweki bayana kwa umma.

Wilayani nako hakusemeki, kuna ofisa elimu wilaya ambaye naye ana maofisa elimu taaluma na ofisa elimu takwimu na vielelezo. Katika wilaya nyingine maofisa hawa wasaidizi wa ofisa elimu wanaweza kuwa zaidi ya mmoja.

Hapo hapo kuna waratibu elimu kata! Tunapoelekea tunaweza hata kuwa na afisa elimu wa elimu ya juu wilaya! Serikali ambayo imepania kubana matumizi haina budi kuyamulika haya matumizi mabaya ya rasilimali.

Mkanganyiko wa majukumu, utitiri wa vyeo bado unachochewa na namna maofisa hawa wanavyopatikana. Kama kuna vigezo bayana vya kufuatwa ili kuwapandisha watu hivi vyeo basi havitumiki.

Kuna shutuma za udugu, uswahiba, udini na hata utoaji wa fedha katika kuupata ukubwa. Hali hii inapunguza idadi ya rasilimali watu ambao wangetumika kufundisha madarasani.

 

Mchezo mchafu

Kama alivyodokeza Rais John Magufuli katika hotuba yake kwa wakurugenzi wa wilaya kuwa kuna watu wanauza vyeo; je, katika sekta ya elimu kuna watakatifu kiasi gani mpaka biashara hiyo ya kuuza na kununua vyeo isiwepo?

Kutofuatwa kwa umakini vigezo vya kupeana ukubwa pengine ndio kumesababisha kupatikana watendaji wasio na uwezo. Watendaji ambao ilidhaniwa wao wawe ndio chemchem ya mawazo na hamasa ya utekelezaji wameishia kuwa wapiga dili huku wakisubiri kutekeleza maagizo kwa wale waliopaswa kuwashauri.

 

Viongozi wasio na uwezo

Badala ya kuwa washauri wataalamu wamegeuka kuwa wapokea maagizo. Kwa mfano, viongozi wa elimu mikoani na wilayani hawakuwa mawazo ya ujengaji wa shule za kata, lakini maagizo yalipokuja walisukumwa wakatekeleza. Hawakuwa na mawazo ya ujenzi wa maabara lakini waliposukumwa wakatekeleza.

Vivyo hivyo hawakuwazia hata siku moja kuwashauri wakuu wa mikoa, wakurugenzi na wakuu wa wilaya kufanya harambee ya madawati, lakini agizo lilipokuja wanalitekeleza.

Viongozi wetu wa elimu wamebaki kuwa kama matoroli, hawawezi kubuni, hawana maono, hawana maamuzi wanasubiri tu kubebeshwa vitu kisha wasukumwe ili kuvipeleka vinakohitajika.

Japo elimu ni suala nyeti katika kila taifa, katika nchi yetu elimu haionekani kupewa kipaumbele inavyostahili. Hata wananchi na vyombo vya habari wanahamasika na kufuatilia zaidi na habari za viongozi wa kisiasa au taasisi za fedha kuliko viongozi wa elimu.

Umma haujali nani anakuwa kiongozi katika elimu. Umma haujali kama kiongozi wa elimu ni mwizi wa mitihani, ana vyeti feki, au amesomea chuo cha uchochoroni. Hata madudu yanayofanyika katika elimu wala hayatushtui.

Umefika wakati sasa wa kuchunguza na kuhakiki viongozi wetu katika elimu. Tufahamu uwezo wao na wasifu wao kama ilivyo kwa viongozi wengine katika sekta nyingine.


Moustapha Puya ni mdau wa elimu 0713593797