Elimu yetu inatuandaa kukabiliana na tatizo la ajira?

Muktasari:

Inavyoonekana, mzazi huyu kama wazazi wengine, alikuwa na matarajio makubwa alipomsomesha mwanawe. Kwake, mafanikio ya elimu yanatafsirika katika uwezo wa kujiajiri au kupata ajira.

“Kijana wangu amesoma shahada ya ujasiriamali. Huu sasa ni mwaka wa pili sioni kitu anachofanya na huo ujasiriamali wake aliousomea. Hawezi kujiajiri, hawezi chochote; mpaka nauli ananitegemea.” Ni kauli aliyonieleza mzazi mmoja hivi karibuni.

Inavyoonekana, mzazi huyu kama wazazi wengine, alikuwa na matarajio makubwa alipomsomesha mwanawe. Kwake, mafanikio ya elimu yanatafsirika katika uwezo wa kujiajiri au kupata ajira.

Hata hivyo, hali ni tofauti kidogo. Wahitimu  wengi wanapomaliza masomo yao, wanashindwa kuutumia ujuzi walionao kutengeneza ajira kama anavyoeleza  mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Maranya Mayengo:

“Elimu yetu haimuandai mwanafunzi kukabiliana na tatizo la ajira, bali inamuandaa kuwa tatizo anapokosa ajira.”

Mayengo anafikiri, tatizo hili halianzii kwa wanafunzi bali ni suala la mtazamo wa jumla wa jamii kuhusu ajira na kazi.

Anasema, “Watu wengi hawana ujasiri wa kujiajiri, sio tu kwa wahitimu wetu bali hata kwa walimu wao. Msamiati wa kujiajiri ni mwepesi kuzungumzwa na watu walioko kwenye ajira, wanasiasa na maofisa wa Serikali ambao kimsingi wao hawana ujasiri huo.”

Imekuwa kawaida kusikia watu waliofanikiwa, ikiwa ni pamoja na wanasiasa, wakitoa wito kwa vijana kujiajiri na kuacha kuisubiri Serikali iwape ajira. Hata hivyo, ni vyema tukatafakari namna tunavyowawezesha vijana kuitikia wito huo.

 

Elimu inawajengea uwezo wahitimu?

Katika enzi za elimu ya ujamaa na kujitegemea, kwa kiasi kikubwa, kila ngazi ya elimu iliandaa watu wanaoweza kuzalisha kazi bila kulazimika kuwa na elimu ya juu. Mwanafunzi wa ngazi yoyote ya elimu alipatiwa maarifa yaliyomwezesha kufanya kazi bila kulazimika kupitia mafunzo mengine maalum.

Mwalimu Pamela Challo wa Shule ya Sekondari Viwandani, Dodoma anasema aina ya elimu wanayopata wanafunzi inaweza kuwa kikwazo cha kujiajiri kwa wahitimu wengi.

“ “Shule za mapishi, ushonaji, ufundi, zilisaidia kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri wenyewe bila shida. Tulipofuta masomo kama hayo tulitengeneza tatizo. Sasa hivi watoto hawajengewi ujuzi, wanaandaliwa kufaulu mitihani na kusubiri ajira,” anaeleza.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mwalimu Morice Missanga wa mkoani Arusha, anayesema:

“Mfumo wetu wa ufundishaji umejikita zaidi kwenye content coverage (kumaliza yanayotakiwa kufundishwa) zaidi kuliko kwenye ujuzi. Ujuzi ndio unaoweza kuibua ajira zisizoonekana kwa macho ya darasani.”

Anaongeza: “Kama elimu yetu ingetambua nafasi ya ajira zisizo rasmi na kuziingiza kwenye ufundishaji kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, huku kunakoitwa juu (elimu ya juu) kusingesongwa kwa maana ya kuwa na wahitimu wengi kuliko mahitaji. Fedha zinazotumika kuwasomesha elimu ya juu, zingekuwa ndio mtaji wa kuingia kwenye stadi za kazi na ubunifu.”

Tunachuja badala ya kukuza

Kwa muda mrefu, tumelenga kuwachuja wanafunzi kwa vigezo, ambavyo wakati mwingine havina uhusiano wa moja kwa moja na kazi watakazozifanya baada ya kumaliza masomo yao.

Kwa mfano, mwanafunzi mwenye kipaji cha kuigiza au kuimba anaposhindwa kufaulu Fizikia anaambiwa hana akili ya kuendelea na masomo.

Kwa utaratibu huu, idadi kubwa ya wanafunzi wenye uwezo usiotambuliwa kwa mitihani wanakosa fursa ya kukuzwa, ili wawe watu wanaofanana na uwezo uliomo ndani yao.

Badala ya kukuza uwezo wa wanafunzi, tunatumia rasilimali nyingi kuwahudumia watu wachache tunaofikiri ndio wenye tija. Lakini mwisho wake wanaishia kuidai Serikali iwaajiri, kwa sababu hawajui wanavyoweza kutumia maarifa waliyofikiri wanayo.

Kwa nini tusiweke utaratibu wa kuwajenga wanafunzi wote kadri ya uwezo walionao? Elimu ikiweza kuibua na kukuza uwezo binafsi wa mwanafunzi, ni dhahiri tatizo la ajira litapungua.

Kukuza thamani ya wahitimu

Dhima kuu ya elimu ni kupanua uelewa wa watu kuhusu matatizo yanayoikabili jamii yao. Hata hivyo, ni muhimu uelewa huo uwasaidie wahitimu kutafuta majibu ya changamoto zinazoikabili jamii.

Kijana anayejengewa uwezo wa kuona na kutatua changamoto, mkononi mwake anakuwa amekabidhiwa ufunguo unaobeba thamani yake.

Kwa kuutumia ufunguo huo, kijana huyu hawezi kukosa kazi ya kufanya akirudi kwenye jamii.

Ili hilo liwezekane, mamlaka za elimu zinawajibika kufanya utafiti kujua shida halisi zinazowakabili watu ili kutengeneza programu zinazojibu changamoto halisi katika jamii.

Hata hivyo, mahitaji ya jamii yanabadilika kila siku. Changamoto ni namna ya tunavyoweza kukabiliana na mabadiliko haya.

Lakini pia, upo ukweli kwamba mazingira yanavilazimisha vyuo kutoa maarifa ya jumla kwa lengo la kuchokoza uelewa. Kazi ya kuyafanya maarifa hayo yajibu matarajio binafsi ya mwanafunzi, inabaki kuwa ya mwanafunzi mwenyewe na mazingira yake.

Hivyo ni wajibu wa mwanafunzi binafsi kuhakikisha anajua kwa hakika kile anachokitaka, ili aweze kuchagua eneo la kitaaluma linalokidhi wito alionao ndani yake.

Tuthamini ujuzi

Wahitimu wengi hawaajiriki, kwa sababu wakati mwingine wanakosa ujuzi. Wanashindwa kutafsiri ufaulu mkubwa wa darasani katika utendaji. Kutojua wafanye kutokana na yale wanayoyajua, kunafanya lugha ya kujiajiri iwe ngumu kwao.

Kasoro hii inaweza kurekebishwa ikiwa tutaanza kuthamini ujuzi na si maarifa pekee. Badala ya walimu kuuliza maswali yanayolenga kupima uelewa wa mambo darasani, waende hatua moja mbele.

Mwanafunzi apimwe namna anavyoweza kutumia maarifa aliyonayo kuboresha hali ya mambo katika jamii yake.

Aidha, ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi za kuoanisha mazingira halisi ya kazi na ujuzi unaotolewa darasani. Ufundishaji ulenge kuwafanya wanafunzi waione jamii yao wakiwa darasani badala ya kuwafundisha mambo ya kufikirika wasiyoyaona katika maisha yao ya kila siku.

Pia, tutafakari sababu iliyotufanya tupanue elimu ya juu na kupunguza uzito wa vyuo vya kati na vyuo vya ufundi.

Kasumba kwamba kufika chuo kikuu ndio kipimo cha kuelimika, inachangia kukuza tatizo la ukosefu wa ajira.

Mwandishi ni mhadhiri wa saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Blogu: http://bwaya.blogspot.com , 0754870815