Fabian-Hatuko ‘serious’ kuzitaka medali za Rio

Mwanariadha mashuhuri wa Tanzania, Fabian Joseph.

Muktasari:

Akizungumzia maandalizi hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, Fabian alisema kuwa matumaini ya kufanya vizuri katika Michezo ya Olimpiki yameyeyuka kutokana na maandalizi duni.

Mwanariadha mashuhuri wa Tanzania, Fabian Joseph ameibuka na kusema wanamichezo wa Tanzania watakaoshiriki Michezo ya Olimpiki kwenye mji wa Rio de Janeiro, hawana dalili zozote za kutwaa medali.

Akizungumzia maandalizi hayo mwishoni mwa wiki iliyopita, Fabian alisema kuwa matumaini ya kufanya vizuri katika Michezo ya Olimpiki yameyeyuka kutokana na maandalizi duni.

Mwaka 2003 Fabian kwa mara ya kwanza alishiriki mashindano ya dunia ya nusu marathoni yaliyofanyika katika mji Vilamoura nchini Ureno na kumaliza nafasi ya pili.

Fabian anasema maandalizi ya ushiriki wa wanamichezo wa Tanzania katika michezo ya mwaka huu ni hafifu na hayataiwezesha Tanzania kufanya vyema katika mashindano hayo.

“Michezo imekaribia lakini kwa hakika maandalizi yetu ni hafifu, hatujawezeshwa kifedha ili kujiandaa kikamilifu kushiriki mashindano hayo,” anasema Fabian alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Fabian anashauri Serikali kuingilia kati kunusuru maandalizi ya wanariadha wa Tanzania ili kuepusha aibu ya kutofanya vizuri katika michezo hiyo.

“Nina imani Rais John Magufuli ni mpenda michezo, tunaiomba Serikali iingilie kati na kuwawezesha wanamichezo wa Tanzania kuandaliwa vyema,” anasema Fabian na kuongeza kuwa bila kufanya maandalizi ya uhakika taifa litavuna aibu.

Mwanariadha huyo mzaliwa wa Manyara miaka 30 iliyopita alishiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwamo Michezo ya Jumuiya ya Madola, mashindano ya dunia ya nusu Marathon ya New Delhi India na Edmonton Canada pamoja na mashindano ya dunia ya nusu Marathon yaliyofanyika mwaka 2003 nchini Ureno na alishika nafasi ya pili.

Wanamichezo wa Tanzania wamepanga kushiriki michezo hiyo itakayofanyika kwenye mji wa Rio de Janeiro, licha ya kuwa kumetolewa ushauri mbalimbali kuwa Tanzania ijitoe ili ijipange kwa Michezo ya 2020 Tokyo.