Fahamu jinsi ya kujenga ujasiri wa kukabiliana na changamoto katika maisha

Muktasari:

Watu wa aina hii ya pili wako wengi. Wao huwa wanasalimu amri na kuziachia changamoto ushindi. Hukubali kuwa hawana wanachoweza kufanya na kubaki wamenyongea kwa huzuni. Tena hata huwa hawafikirii kuitumia fursa hiyo kwa kujifunza maarifa mapya ya kukabiliana na mitihani inayomkabili mtu katika maisha.

Je unapokabiliwa na changamoto katika maisha huwa unaweza kukabiliana nazo? Je huwa unakabiliana nazo hadi uzitatue? Au wewe ni miongoni mwa wale watu ambao baada ya kujaribu kidogo tu na kushindwa hukubali kuwa wamefikwa na bahati mbaya na wala huwa hawahangaiki zaidi kutafuta mbinu ya kuzitatua.

Watu wa aina hii ya pili wako wengi. Wao huwa wanasalimu amri na kuziachia changamoto ushindi. Hukubali kuwa hawana wanachoweza kufanya na kubaki wamenyongea kwa huzuni. Tena hata huwa hawafikirii kuitumia fursa hiyo kwa kujifunza maarifa mapya ya kukabiliana na mitihani inayomkabili mtu katika maisha.

Inatupasa tutambue kuwa kadri unavyoziacha huzuni ikatuzonga na kuiruhusu zitawale fikra zetu, ndivyo kadri tunavyofanya uwezo wetu wa kuishinda mitihani ya maisha uwe mdogo zaidi. Hatutaweza kukabiliana na shida na matatizo yanayotufika kwa kuwa wanyonge na wenye majonzi. Kadri huzuni na majonzi yanayoingia katika akili zetu ndivyo kadri uwezo wetu wa kukabiliana na mitihani unavyozidi kuwa mdogo.

Inatupasa tufahamu kuwa sisi wote tunapozaliwa huwa ndani yetu kuna mfumo wa neva unaofanya mwili ujihami. Kila tunapokuwa mfumo huu hukomaa na kadri unavyokomaa ndivyo unavyotusaidia kuepuka fadhaa au kuvurugika kwa akili na kutuongezea uwezo wa kuhimili mitihani mbalimbali inayotupata katika maisha.

Changamoto kubwa katika mitihani inayotupata maishani ni uwezo wa kujifunza jinsi ya kuhimili matatizo yanayotupata katika maisha. Lakini tunaweza kujifunza na tutajifunza kutoka wapi? Watu wenye uwezo mkubwa wa kukabiliana na matatizo ya maisha hawakujifunza shule au chuoni. Hawa wamejifunza kutokana na uzoefu walioupata katika maisha. Kuna usemi maarufu usemao” Ukimuona ngiri amezeekea msituni ujue amekwepa mishale mingi” Hii ina maana kuwa kadri unavyoishi na kukua na ukapambana na changamoto za aina mbalimbali ndivyo kadri unavyopata uzoefu ambao hauna budi kuutumia kadri uanvyoendelea kuishi. Kama ni changamoto, utakuwa umewahi kukutana nazo nyingi na umejifunza njia nyingi za kukabilina nazo.

Tunawezaje kujifunza kutokana na uzoefu wa maisha?

Huenda kuna wakati fulani ulikumbwa na changamoto fulani zikakuelemea na ukashindwa kuzitatua hadi zikayafanya maisha yako yakawa magumu sana. Lakini haiwezekani changamoto hizo zikawa zilikukumba wewe peke yako tu katika mtaa au kitongoji kizima. Lazima watakuwapo watu wengine hapo ulipokuwa waliokabiliwa na changamoto kama zako ambao walizivuka na wewe ukabaki umesononeka tu. Hao watakuwa wale ambao hawakukubali kukumbwa na wimbi la kupigwa na butwaa hadi wakawa na hali ngumu kama wewe. Wao walikataa kushindwa na changamoto hizo wakajitahidi kutafuta kila njia ya kuzitatua. Kubwa zaidi walihakikisha wanapata faraja ndani ya dhiki. Hivyo wakaweza kufurahia na kufaidi kitu kimoja kilicho bora zaidi yaani uhai. Kuna mwanamuziki mmoja aliwahi kuimba kuwa “Furaha iliyoje kuwa hai, kwani utaweza kuiona kesho”. Watu wanaonusurika na changamoto hutumia vipaji na uwezo wao wote kujenga katika fikara zao mtazamo wa matumaini kwa wao wenyewe na familia zao. Pamoja na kujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto kutoka kwa wazazi, walimu na watu wengine, wanalichukulia suala la uzoefu katika maisha kama shule inayoendelea katika uhai wote wa binadamu.

Watu wenye maisha yasiyo na huzuni au wasiwasi ni wale ambao huwa tayari hata kuthubutu kuchukua hatua za kufanya mambo yenye kashaka ili mradi kuvuka changamoto inayotishia kuyafanya maisha yao kuwa magumu.

Katika mchakato wa kujifunza kukabiliana na changamoto jiulize maswali yafuatayo:-

• Je katika changamoto hi inayonikabili kuna jambo linalonibidi nilifanye ambalo sijawahi kulifanya. Kila unapokabiliwa na changamoto ichukulie kama tukio jipya litakalokuwezesha kupima kiwango cha uwezo wako. Kama unalotakiwa kulifanya hulijui ichukulie hiyo kama nafasi ya kujifunza kutoka popote hata kama kwa watu wengine mradi tu uitatue changamoto hiyo.

•Kila unapopata changamoto jiulize kama inaweza kuwa imesababishwa na jambo fulani au inaweza kuwa imetokea tu bila kusababishwa na jambo lolote maalumu. Baada ya kuitambua sababu itumie kama chanzo cha kuitatua changamoto hiyo. Kwa hakika itakusaidia kuikabili, hata kama haitalimaliza kabisa tatizo hilo itaweza walau kupunguza makali yake. Aidha, baada ya kuijua sababu, hakikisha sababu hiyo haisababishi changamoto nyingine siku nyingine.

•Inapotokea changamoto ifikirie na ichunguze kwa makini huku ukiilinganisha na changamoto nyingine zilizowahi kukukabili zamani na ambazo uliwahi kuzitatua. Tafakari vitendo ulivyofanya wakati ule na uone kama unaweza kuvitumia katika changamoto hii. Jiulize ulifanya vizuri kiasi gani? Swali jingine liwe kama ingebidi arudie kutenda alichofanya wakati ule ni mambo gani angeyafanya tofauti na wakati ule?

•Unapopata changamoto inayokukabili jiulize inakuongezea funzo gani katika uzoefu uliokwisha kuupata katika maisha yako. Pamoja na kujifunza wewe binafsi kuna mafunzo gani unayopata kutokana na changamoto hiyo kuhusu familia na jamii inayokuzunguka.

Kutokana na majibu ya maswali tuliyoyatafakari na uzoefu tulionao ni dhahiri kuwa tunapata mwanga na jinsi tunavyoweza kuvuka vikwanzo mbalimbali vinavyotokana na changamoto zinazokukabili katika maisha. Jambo muhimu zaidi ni kila mmoja wetu kuwa na uwezo wa kuongea na nafsi yake yeye mwenyewe. Kuna watu ambao huweza kujisemeza wao mwenyewe zaidi kuliko wengine. Tunapojisemeza sisi wenyewe huwa tunatafsiri fikra zetu katika vitendo kutokana na upeo na uelewa wetu na uzoefu. Tukilifanya zoezi hili vyema tutaweza kushinda changamoto zote zitakazotukabili katika maisha yetu.

Hitimisho

Watu wenye ujasiri wa kukabiliana na mitihani ya maisha mara chache huwa wanakubali kuzungukwa na jambo lililokwishapita. Huwa hawapendi kubaki katika hali ya kutatizika kwa mambo ambayo hayakwenda vizuri. Hulenga fikra zao katika wakati ujao. Huamua kuchukua dhamana na jukumu la kurekebisha hali. Aidha, huamua kudhibiti hali ya jinsi wanavyozichukulia changamoto hizo ili kuhakikisha haziathiri maisha yao na amani ya akili.