Fahamu nini cha kufanya kwa mpenzi mwenye hasira

Muktasari:

  • Hapa nataka nikusaidie jinsi ambavyo unaweza kufanya pale mpenzi wako anapowaka kwa hasira kali. Kujua hili kutakusaidia kupooza au kuponya hasira za mwenzako na siyo kuchochea moto mkubwa zaidi ambao unaweza kuleta madhara makubwa zaidi.

Katika uhusiano wa aina yeyote, hakuna anayeweza kusema hajawahi kukasirika. Mara kwa mara tuna kwazana na kukasirishana, ingawa wako wale ambao hasira yao iko karibu zaidi na huja kwa ukali zaidi na mara nyingine huleta madhara katika vitu, watu, au hisia za mpenzi mwingine.

Hapa nataka nikusaidie jinsi ambavyo unaweza kufanya pale mpenzi wako anapowaka kwa hasira kali. Kujua hili kutakusaidia kupooza au kuponya hasira za mwenzako na siyo kuchochea moto mkubwa zaidi ambao unaweza kuleta madhara makubwa zaidi.

Nini cha kufanya

Ikubali hasira ya mwenzako kama ndiyo njia yake ya kuonyesha hisia zake.

Hasira yake na kulipuka kwake kunaweza kuja kwa staili ya kuleta maudhi sana na wala kusikokuwa na sababu ya msingi, lakini kubali kuwa ana haki ya kuwa na hasira. Hasira yake yaweza isiwe nzuri kwako, lakini kumbuka haiashirii mwisho wa uhusiano wenu. Uhusiano uliobora huruhusu kwa kiasi fulani vimikikimikiki kama hivi, huwezi kupinga visiwapo kwa asilimia mia.

Mfanye mpenzi wako awajibike kwa hasira yake mwenyewe

Najua anaweza kukulaumu wewe kwa hasira zake, iwapo hali hii inatokea kataa kukubali wazo hilo, wewe huuhusiki kwa chochote, wala wewe siyo sababu ya hasira hizo bila kujali yeye anasema nini. Yeye ndiyo amechagua kukasirika na kufanya hivyo anavyofanya na mara nyingi ni mbinu yake ya kukufanya ukubaliane na matakwa yake. Kwa hali yoyote kataa kuchezewa kupitia hasira yake.

Tulia na uwe na sababu ya utulivu huo

Hata kama mpenzi wako kavuka mipaka kwa kukutukana, kukulaani, kukupayukia au hata kukupiga, bado unaweza kuchagua kuwa mpole na mwenye sababu maalumu ya kutulia kwako.

Taratibu na kwa upole mtulize kwa kumwonyesha uhalisia wa tukio. Kwa busara na kujizuia kwa hali ya juu, jitahidi kumueleza mawazo yako, hisia zako na ukionyesha jinsi hali hiyo inavyokusumbua mara inapotokea, kamwe usitumie sentensi za “wewe” mfano “wewe unaudhi sana”,

“Wewe sikuelewi kabisa” bali tumia sentensi za “mimi”, mfano “mimi ninaumia sana unapofikia hali hii”. Endelea kutoa mawazo yako kwa ufasaha na katika hali ya kumjali.

Weka mipaka kwa hasira zisizo na sababu ya msingi

Kama mwenzako anazidi kuonyesha hasira yake isiyo na msingi, anatukana na kuendelea kubwatuka na wala hakusikilizi unachotaka kukisema, basi unaweza kuamua kutoka na kuwa pembeni ya eneo hilo, kwa upole mwambie kuwa utafurahi kuzungumzia jambo hilo mara atakapopoa ukali na baada ya hapo nenda chumba kingine mpaka atulie.

Jizuie usiombe msamaha au kumtaka radhi

Najua watu wengi, hususan jinsia ya kike wakifikia hatua hii hujiona wao ndiyo wakosaji na hivyo hukimbilia kuomba radhi. Kumbuka kuwa mpenzi mkorofi na mtukanaji hastahili kuombwa radhi. Ni kweli yawezekana wewe ni sababu kwa kiasi fulani kwa tatizo hilo, lakini kwa kule kukasirika kwa staili hiyo hakumfanyi astahili kuombwa radhi maana kwa kufanya hivyo utaendeleza tabia yake hiyo mbaya. Msamaha au radhi yaweza ikafaa baadaye kidogo wakati mpenzi wako ametulia na ameiweza hasira yake. Jaribu kuihifadhi samahani yako mpaka wakati huo ufike.

Mpongeze mpenzi wako mara tu anapoamua kufanya lile lenye staha na wala siyo anapoonyesha hasira.

Wakati wowote mpenzi wako anapoonyesha kushuka na kuelewa kuwa analofanya siyo jema, mpongeze, mtiemoyo aendelee na tabia hiyo njema kwa kumwonyesha utayari wa kumsikiliza kile anachotaka kusema ili mfikie mwafaka. Katika uhusiano jifunzeni kuzipongeza na kuzitia moyo tabia na matendo mema na pia kuyazuia yale yasiyo mema yasiendelee.

Jipongeze pia

Kamwe usiruhusu matusi, kejeli na kashfa za mpenzi wako zikuvunje moyo na kukushusha thamani yako. Usijione mnyonge kwa lawama zake labda tu uchague kukubali anachokisema kwako.

Jione bado kuwa wewe ni mwema na ulikuwa unafanya mambo kwa nia njema. Ukiweza jipongeze kwa kufanya kile ambacho hisia zako zitaona zimepongezwa. Mfano, jitoe mtoko, nenda kwenye filamu, jipikie kitu kizuri, fanya nafsi yako ijisikie iko juu.

Kama unajiona huwezi au unapata shida zaidi kuzifuata njia hizi basi jitahidi kumtafuta mshauri wa kisaikolojia kwa msaada zaidi.