Fahamu ujenzi wa banda bora la kuku

Kuku wanahitaji sehemu nzuri ya kuishi na kukua vizuri.

Mfugaji wa kuku ana jukumu la kuhakikisha kuku wake wanaishi katika mazingira mazuri kiasi cha kutosha kufanya uzalishaji kwa faida.

Katika mchakato wa ufugaji kuku, ujenzi wa banda ni hatua muhimu na nyeti kwa kuwa inachangia katika uzalishaji wa kuku wako.

Kabla ya kufanya chochote mfugaji anatakiwa kujiridhisha kuwa banda lake linafaa au la.

Mfugaji yeyote mwenye uchungu na mifugo yake hawezi kukwepa kuwa na mahali salama kutunzia mifugo hiyo. Hivyo kabla ya kutoa fedha mfukoni kununua mbegu ya kuku, ni lazima uwe na uhakika na sehemu unayokwenda kuweka kuku wako.

Aidha, mfugaji anaweza kuchagua ufugaji kwa njia ya kienyeji ambayo kuku wanajitafutia chakula. Lakini bado akalazimika kuwa na banda la kuwatunza kuku wake wakati wa usiku.

Hitajio la banda kwa mfugaji yeyote ni la lazima bila kujali anafuga nini au anafuga kwa njia gani. Ieleweke kuwa kuku ni viumbe hai wenye mahitaji sawa na binadamu.

Mtu anayefuga kuku anatakiwa kujua bidhaa yake kuwa ni viumbe hai wenye mahitaji yote. Kama ilivyo kwa binadamu mwili wa kuku ukikosa hata moja kati ya mahitaji yake muhimu utaona upungufu kwenye ukuaji na uzalishaji wake.

Kwa kuzingatia hayo ni vizuri kutengeneza mazingira bora kwa kuku, ili kuepusha gharama za kuanzisha biashara isiyokuwa na faida.

Faida katika ufugaji hutegemea malezi bora kwa mifugo. Ukiondoa gharama nyingine kama vile matibabu, chakula, maji, katika ufugaji wa kuku, gharama ya kujenga banda hufanyika mara moja. Mfugaji akijenga banda imara hawezi kurudia kujenga banda lake kila wakati kama atakavyogharimia maji, umeme, chakula na dawa.

Gharama ya kujenga banda ikipita, imepita hairudi tena hadi mfugaji atakapopata wazo jipya kuongeza banda lingine kupanua biashara.

Kwa mantiki hii mtu akisema nataka kujenga banda ajue kuwa anafanya kitu cha kudumu sio leo na kesho kinaharibika. Na kama wewe ni mmoja kati ya wale wanaoona fursa katika ufugaji wa kuku hakuna sababu ya kuogopa kufuga.

Nakushauri itendee haki biashara yako kwa kuzingatia mahitaji muhimu ya kuku wako, ikiwamo sehemu nzuri ya maisha yao bandani ili uone faida zaidi.

Sifa za banda bora

1.Sehemu ya kujenga banda: Chagua sehemu sahihi isiyo na vikwazo kufikiwa na huduma kama vile watoa huduma za maji, chakula, ulinzi, wanunuzi. Mambo haya na mengine yenye kufanana na hayo ni muhimu kuzingatiwa.

Epuka kujenga sehemu yenye kutuama maji utasababisha mafuriko ya maji bandani, unyevu nyevu wa mara kwa mara na magonjwa yasiyoisha hasa wakati wa mvua.

2.Uelekeo wa banda: Jenga banda pande za marefu ya banda zitizame Kusini na Kaskazini ili kuepusha tabu ya mvua, upepo na jua kupiga kuku bandani. Kitaalamu dunia hujizungusha kutoka Magharibi kwenda Mashariki na pepo huvuma kinyume na uelekeo wa dunia, hiyo pepo nyingi huvuma kutoka Mashariki kuelekea Magharibi.

Mvua hunyesha kwa kutegemea uelekeo wa upepo. Aidha, jua huchomoza Mashariki na kuzama Magharibi. Kama mfugaji atajenga banda lake marefu ya banda yakaelekea Mashariki na Magharibi ajue kuwa madirisha yake yataelekea Mashariki na Magharibi, hivyo mvua itanyesha bandani, upepo utavuma na kusumbua kuku.

Pia, jua litapiga bandani asubuhi na wakati wa jioni. Ili kuepukana na tatizo hili, ni vema mapana ya banda yatizame Mashariki na Magharibi na pasiwe na dirisha lolote kwenye mapana yote kuepuka adha ya mvua, upepo na jua.

3.Usalama wa kuku bandani: Hakikisha banda ni imara kuepusha wizi kwa kuvunja mlango, madirisha au kubomoa ukuta.

Mfugaji anaweza kutumia wavu imara kwenye madirisha, ukuta wa tofali au miti imara na kuezeka vizuri banda lisivuje wakati wa mvua.

4.Nafasi ndani ya banda: Jenga banda kulingana na wingi wa kuku watakao ingia na kuishi humo. Nafasi nzuri katika ufugaji wa kisasa ni: kuku wa mayai wanne kwa kila mita moja ya mraba. Kuku wa kisasa wanaweza kukaa watano hadi sita. 5 – 6.

Kuku wakijaa, hushindwa kula vizuri, hudumaa, kumwaga maji bandani, kupata maradhi mengi, kujenga tabia ya kudonoana na kushindwa kutaga vizuri au kula mayai kwa wale kuku wa mayai.

5.Hewa na mwanga: Kuku wanahitaji hewa safi na mwanga wa kutosha ili wakue na kuzalisha vizuri.

Mfugaji anatakiwa kujenga banda lenye madirisha makubwa na mengi ya kutosha ili hewa safi na mwanga vipate kuingia bandani. Kuku hutengeneza joto la wao wenyewe kutokana na kupumua wakiwa bandani.

Mbolea yao na majimaji wanapojisaidia au kunywa maji vinahitaji kukaushwa kwa hewa inayotoka nje na kuondoa harufu mbaya.

Banda lenye mwanga hafifu na hewa nzito, huwafanya kuku waugue mara kwa mara kutokana na vimelea wa magonjwa hupenda mazingira hayo. Banda lenye hewa safi ya kutosha na mwanga hupunguza gharama za kutibu kuku mara kwa mara.

6.Sakafu ya banda na urefu wake kwenda juu: Banda linaweza kujengwa kwa urefu wowote kwenda juu lakini lisipungue futi nane kutoka sakafuni hadi kwenye paa lake.

Sakafu yake inyanyuliwe kimo cha inchi sita hadi 10 kutoka usawa wa ardhi ili kuepuka maradhi kwa kuku. Udongo ni makazi ya wadudu wengi na vimelea vya magonjwa.

Kimo cha ukuta wa tofali kutoka sakafu hadi mwanzo wa madirisha kisizidi futi tatu, ili kuku wasionekane na mtu akiwa nje, huku ikiruhusu hewa nyingi na mwanga vipite.

Madirisha makubwa yenye wavu imara ni fahari katika ufugaji wa kuku. Usifunge madirisha kama nyumba ya kuishi. Madirisha yakae wazi usiku na mchana kwa kuku wakubwa.

Kwa vifaranga, madirisha yanaweza kuwekwa mapazia kupunguza baridi (inategemea na hali ya hewa). Sakafu ya banda isakafiwe ili kuku wasichimbe mashimo bandani. Pia, usitengeneze sakafu laini yenye kuteleza kama nyumba ya kuishi.