KUZA FURSA : Faida na hasara ya punguzo la bei ya bidhaa sokoni

Muktasari:

Kama bidhaa huzalishwa kwa Sh2,000 na nyongeza ya faida ni Sh500, hivyo bidhaa itauzwa kwa Sh2,500. Huu ni mfano rahisi wa namna ya kupanga bei.

Bei ya bidhaa na huduma huwekwa kwa kuzingatia vitu vingi ikiwamo gharama za uzalishaji na faida.

Kama bidhaa huzalishwa kwa Sh2,000 na nyongeza ya faida ni Sh500, hivyo bidhaa itauzwa kwa Sh2,500. Huu ni mfano rahisi wa namna ya kupanga bei.

Tukisimama katika mfano wa bei hapo juu, punguzo la bei maana yake ni kupunguza bei kuwa ya chini ukilinganisha na bei ya awali.

Pia, mfano wa hapo juu unaonyesha punguzo la bei linaweza kuwa bidhaa ikauzwa kwa Sh2,200 kutoka Sh2,500.

Kuna sababu nyingi za kufikia uamuzi wa kupunguza bei na kila sababu ina matarajio yake katika biashara.

Punguzo la bei inaweza ikafanyika katika mazingira ya aina tofauti.

Miongoni mwa mazingira makubwa yanayosababisha uamuzi wa mfanyabiashara kuweka punguzo la bei ya bidhaa ni pamoja na lile la muda maalumu la mwezi mmoja, miwili au mitatu kulingana na malengo ya muhusika. Katika mfano wa bei, inaweza kupungua hadi Sh2,200 ikadumu kwa miezi miwili na baada ya muda huo kwisha, bei ya awali ikarejea pale pale.

Lakini pia bei inaweza ikapunguzwa kutoka Sh2,500 hadi Sh2,200 kwa muda wote haitapanda tena.

Hii pia inatokana na mazingira ya biashara sokoni pamoja na malengo ya wahusika.

Na hata kutokana na kupungua kwa gharama za uzalishaji, bei inaweza kupunguzwa.

Tukirejea mfano wa hapo juu, gharama za uzalishaji zikipungua kutoka Sh2,000 hadi Sh1,500, mfanyabiashara anaweza kupata punguzo la 1,500 kwa kujumlisha na faida Sh500 atakuwa amepata Sh2,000.

Hapa bei inakuwa imepungua kutokana na kupungua kwa gharama za uzalishaji ingawa faida haijapungua imebaki ile ile. Bei inaweza kupunguzwa pia pale mfanyabiashara anapotaka kumalizia bidhaa ambazo huenda zinakaribia kuharibika ama fasheni yake imepitwa na wakati.

Katika punguzo hilo lengo kuu ni kuepusha bidhaa kudoda zikasababisha mtaji kukatika.

Katika mfano wa awali, kama gharama za uzalishaji ni Sh2,000 na bei ni Sh2,500, bei inaweza kuwa Sh2000 ama chini ya hapo kwa maana angalau mtaji urudi ama kama mtaji utakatika basi ukatike kidogo kuliko kuupoteza wote.

Faida za punguzo la bei zipo kama kazi ya kupunguza itafanywa kitaalamu baada ya kuzingatika kila kitu ikiwamo aina ya bidhaa, huduma na wateja, hali ya uchumi wa nchi na mazingira ya soko.

Miongoni wa faida ni pamoja na kuongeza mauzo. Lakini bei ikipungua wateja watanunua zaidi.

Kuongeza soko la bidhaa kunalenga pia kupata faida zaidi kwa kuwa mauzo yataongezeka.

Kuokoa mtaji kwa kuuza stoku kabla haija haribika au kupitwa na wakati.

Njia ya kuongeza wateja katika biashara inawezesha kusaidia kumaliza akiba kwa muda mfupi.

Pamoja ya kupata faida, kuna wakati unaweza kuweka punguzo la bei ukapata hasara. Unaweza kupoteza wateja ambao wanaamini ukubwa wa bei ndiyo thamani ya bidhaa na pale unapopunguza wanahisi bidhaa hiyo haina viwango.

Lakini inashauriwa punguzo lako ulifanyie utafiti kabla maana sokoni kuna washindani wako na kila mmoja ana namna yake ya kupunguza ghara za uzalishaji.

Unaweza kupunguza bei kwa Sh300 halafu mshindani wako akapunguza kwa Sh500, bila shaka wateja watahamia kwa mshindani wako. Hali hiyo inaweza ikapunguza faida na mauzo kama wateja hawatalichangamkia punguzo lako.

Inashauriwa kuwa makini katika uamuzi wowote katika biashara kuepuka hasara. Kupata misingi ya biashara kwa wafanya biashara na wajasiriamali ni lazima ili kupata uwezo wa kuendesha na kusimamia biashara kwa usahihi.