Faida za unenepeshaji wa ng’ombe wa nyama

Ng’ombe wa unenepeshaji, wanapaswa kukaa ndani ya banda maalumu kama hili na kuletewa kila kitu, kwa muda wote wa unenepeshaji. Picha na mitandao ya  phys.org na johanerespichius

Muktasari:

MUHIMU

  • Mafanikio katika biashara ya unenepeshaji ng’ombe yanategemea ubora wa ng’ombe unaotumia na upatikanaji wake.
  • Mengine ni upatikanaji wa chakula cha zaida na gharama zake (kama mashudu, pumba, molasesi n.k) gharama ya kuweka miundombinu muhimu  ya unenepeshaji (nyumba, hori la chakula na barabara).

Japo Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa wingi wa mifugo duniani,  bado tunaagiza kiasi kikubwa cha nyama kutoka nje.

Nyama hii ni ile inayotumika kwenye hoteli za kitalii, huku hoja ikitolewa kuwa nyama ya ndani haina viwango na ubora wa kimataifa.

Hata kwa nyama ya soko la ndani, wafugaji wengi hupata hasara wanapouza wanyama wao waliokonda kwa sababu ya malisho duni hasa wakati wa kiangazi.

Sua yaingilia kati

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua) kupitia Idara ya Sayansi ya Wanyama na Uzalishaji pamoja na Kitivo cha Tiba ya Mifugo na Afya ya Binadamu, wameamua  kuanzisha mradi wa utafiti wa unenepeshaji wa mifugo wilayani Hanang.

Lengo la utafiti huu ni kuwasaidia  wafugaji kuzalisha nyama yenye ushindani na viwango vya kimataifa na hatimaye kuuza katika  hoteli za kitalii mkoani Arusha.

Profesa Erikila Kimbita, ni kiongozi wa mradi huu anayesema unenepeshaji ni kitendo cha kumpatia ngo’ombe lishe  bora miezi mitatu kabla ya kupelekwa sokoni pamoja na kumpunguzia umbali na muda wa kutafuta majani ili kumsaidia kufikia uzito na kiasi cha mafuta kinachotakiwa na soko mapema.

‘’Ng’ombe anayenepeshwa huweza kuongezeka kilo 90 katika kipindi cha miezi miatatu na hivyo kumfanya atoe nyama nyingi na laini inayohitajika kwenye hoteli nyingi za kitalii,” anaeleza.

Hatua za unenepeshaji

1. Mfugaji anatakiwa kujenga banda la kutosha ng’ombe anaohitaji kuwanenepesha na ng’ombe mmoja anahitaji nafasi kwenye banda sawa na wastani wa mita 5.5 na banda hilo liwe na hori la chakula na maji humohumo.

2.  Hori liwe na nafasi ya sentimeta 30 - 60 kwa ng’ombe wote waweze kula kwa wakati mmoja na ili kuruhusu usafi kufanyika kwa urahisi, huku  sakafu ikiwa  na mwinuko  wa asilimia mbili.

Baada ya kumaliza uandaaji wa banda mfugaji, anatakiwa kujua sifa za ng’ombe anayefaa kwa unenepeshaji ambapo kwa mujibu wa Profesa Kimbita ng’ombe anayefaa kunenepeshwa anapaswa kuwa na umri wa miaka miwili hadi mitatu.

‘’Vidume visivyohasiwa hukua haraka kwa asilimia 10 - 12 zaidi kuliko vilivyohasiwa yaani maksai, lakini pia ng’ombe chotara hukua zaidi kuliko wale wa kienyeji na mfugaji hashauriwi kutumia ng’ombe waliodumaa kwenye unenepeshaji,’’ anasema.

Baada ya mfugaji kuzingatia hatua hizo, anatakiwa kuandaa ng’ombe wake kwa ajili ya unenepeshaji ambapo atatakiwa kuwachunguza kama wana minyoo na magonjwa mengine na ikigundulika wana minyoo au magonjwa watibiwe haraka kwanza.

Kwa kuwa kabla ya kuanza zoezi la unenepeshaji ng’ombe hao walikuwa wanakula chakula cha kawaida yaani majani pekee,  lazima sasa mfugaji aendelee kuwapatia ng’ombe hao majani mengi na chakula cha unenepeshaji kwa asilimia ndogo na kuongeza taratibu hadi watakapozoea chakula cha unenepeshaji pekee.

Profesa Kimbita anasema endapo mfugaji atawapatia ng’ombe hao chakula cha kunenepeshea ghafla bila majani, watavimba matumbo na anashauri baada ya siku 14 chakula cha unenepeshaji  kitawale zaidi kuliko majani kwenye mlo.

Chakula cha unenepeshaji

Chakula cha unenepeshaji kiwe na virutubisho nguvu  sawa na 12 MJ/ME kg DM na protini kuanzia 12 hadi 15% CP/kg DM. Virutubisho hivyo vinaweza kupatikana kutoka kwenye mchanganyiko ufuatao: Pumba asilimia 70, mashudu asilimia 27, madini asilimia mbili na chumvi asilimia moja

Ng’ombe mwenye uzito wa kilo 300 anaweza kula hadi kilo saba za chakula cha unenepeshaji kwa siku ambayo ni sawa na asilimia 2.5 ya uzito wake, hivyo mfugaji ahakikishe kwa muda wote  hori la chakula lina nyasi na majisafi ya kunywa.

 Pia, litoe nafasi na sentimeta 30 - 60 kwa ng’ombe mmoja ili ng’ombe wote waweze kula kwa wakati mmoja.

Jambo lingine muhimu linalosisitizwa kwenye zoezi la unenepeshaji  ni kuwapo kwa maji  kwa ng’ombe anayenenepeshwa kwa siku kulingana na uzito wake na hali ya joto.

Mafanikio katika biashara ya unenepeshaji ng’ombe yanategemea ubora wa ng’ombe unaotumia na upatikanaji wake.

Mengine ni upatikanaji wa chakula cha zaida na gharama zake (kama mashudu, pumba, molasesi n.k) gharama ya kuweka miundombinu muhimu  ya unenepeshaji (nyumba, hori la chakula na barabara), kiasi cha ujuzi cha mtunza ng’ombe hao, bei ya ng’ombe sokoni kwa walionenepeshwa ukilinganisha na wale wasionenepeshwa pamoja na udhibiti wa milipuko ya magonjwa ya mifugo.

Mambo ya kuzingatia

Mfugaji anatakiwa kutafiti soko kabla ya kuanza kunenepesha, huku akihakikisha  malighafi za unenepeshaji zinapatikana bila shida.  Pia, ng’ombe wa unenepeshaji wanunuliwe kwa bei ya chini ili kuja kuuza kwa bei ya juu wanaponenepeshwa.

Zipo athari zinazoweza kuikumba biashara ya unenepeshaji ambazo mfugaji lazima azifahamu na kuzizingatia kabla ya kuanza unenepeshaji.

Athari hizo ni pamoja na  vifo, ng’ombe kukataa kula chakula cha kunenepesha endapo mfugaji hatafuata taratibu za uchanganyaji wa chakula na ulishaji kwa siku 14 za kwanza, ukuaji hafifu unaotokana na uchaguzi mbaya wa ng’ombe pamoja na mabadiliko ya bei ya chakula cha kunenepesha.

Ili kukabiliana na athari hizo, lazima mfugaji awe na elimu juu ya matunzo ya ng’ombe anayenenepeshwa, kufuata taratibu zinazotakiwa  kukinga ng’ombe kupata magonjwa, kuhifadhi chakula cha kunenepesha cha kutosha kabla ya kuanza kunenepesha au kwa kuingia mkataba na wauzaji wa chakula hicho.

Ng’ombe wa kunenepeshwa asitembee kwenda kutafuta malisho  wala maji, bali akae kwenye banda na kuletewa kila kitu katika kipindi chote cha miezi mitatu ya unenepeshaji.

Calvin Gwabara ni mwandishi mwandamizi wa masuala ya kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo   [email protected], [email protected].