MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Fasihi ya Kiswahili na ajira kwa wasomi

Muktasari:

  • Vijana wengi wa kileo wanapokuwa vyuoni huwa na ndoto nyingi. Huwaza kupata kazi nzuri mara baada ya kuhitimu masomo yao.
  • Aidha, wengi huwaza kumiliki nyumba za kisasa, magari mazuri na fedha nyingi.

Kazi ni kazi ilimradi mkono uende kinywani,” ni msemo wa Kiswahili unaosisitiza watu kufanya kazi yoyote halali ili kujipatia kipato cha kukidhi mahitaji yao muhimu maishani. Kumekuwa na tabia ya kulalamika miongoni mwa wanajamii kuhusu kukosekana kwa ajira hususan kwa vijana waliohitimu masomo yao katika vyuo na vyuo vikuu.

Vijana wengi wa kileo wanapokuwa vyuoni huwa na ndoto nyingi. Huwaza kupata kazi nzuri mara baada ya kuhitimu masomo yao.

Aidha, wengi huwaza kumiliki nyumba za kisasa, magari mazuri na fedha nyingi.

Kwa jumla, huwaza kuwa na maisha ya kifahari kupitia elimu yao. Pamoja na fikra hizo zote, chanzo cha fedha wanachokitegemea ni kuajiriwa.

Ni wachache miongoni mwao wanaowaza kujiajiri. Baada ya kuhitimu, ajira zinapokosekana, vijana hubaki wakiilaumu Serikali.

Riwaya ya Utubora Mkulima iliyoandikwa na Shaaban Robert na kuchapishwa mwaka 1968 inatubungua bongo tuwe na mtazamo tofauti.

Katika riwaya hii msanii anamchora mhusika Utubora kuwa kijana mwenye elimu ya chuo kikuu, aliyekuwa karani kwa bwana Ahmed.

Kijana huyu anachorwa kuwa mchapakazi hodari aliyependwa sana na tajiri wake. Hata hivyo, Utubora hakuona kuwa ajira hiyo ni jambo la kuling’ang’ania. Tamaa yake kubwa ilikuwa kujiajiri mwenyewe na kujipatia kipato kitokanacho na kazi ya ubunifu wa akili yake.

Utubora alikata shauri la kwenda kuishi Mrima (kijijini) akakae shambani karibu na pahali alipokuwa akikaa mama yake. Akiwa huko alijishughulisha na kilimo. Alilima na kufuga mifugo mbalimbali. Moyo wake ulikuwa radhi na wenye furaha katika shughuli zake za kilimo alizokuwa akizifanya. Pamoja na hilo, alifanikiwa kujenga uhusiano mzuri na kila mmoja.

Tumetumia mfano wa kitabu hiki ili kuonyesha kuwa licha ya kuwako kwa ajira za kuajiriwa kuna upande wa pili wa ajira. Kama tulivyokwisha kueleza hapo awali, vijana wengi siku hizi huwaza kuajiriwa.

Ikiwa hawapati ajira hizo, huendelea kubaki mtaani wakisubiri ajira zitoke hata kwa miaka kadhaa. Kilimo kwa baadhi ya vijana huonekana kama ni shughuli ya watu wa tabaka fulani lisilowafaa wao.

Ipo haja ya vijana wasomi kujifunza kutoka kwa msomi mwenzao Utubora (mkulima). Kijana huyu hakuwa na tatizo la ajira lakini pamoja na sababu nyingine za kurudi Mrima, yeye alipenda zaidi kujiajiri mwenyewe. Maisha ya mjini hayakuwa na la pekee kwake.

Alifurahi kuitumia elimu yake ya darasani katika kile alichojipangia mwenyewe yaani kujishughulisha na kilimo. Laiti vijana wangalikuwa na ubunifu wa kutumia elimu yao kubuni ajira binafsi huenda leo hii maisha ya vijana wasomi yangalikuwa na sura tofauti.

Ile hali ya kusubiri ajira za ofisini kwa miaka kadhaa na kulalamika ingepungua. Vijana wanaohitimu ‘wajenge ofisi’ zao katika shughuli za kujitegemea wenyewe kama vile kilimo cha kisasa na viwanda vidogovidogo na hivyo kutoa nafasi za ajira kwa wengine.

Vijana wanaokimbilia mijini kutoka vijijini nao wanalo la kujifunza kutoka kwa Utubora. Mijini ambako vijana wengi hufikiri kuwa maisha ni rahisi, hali ni kinyume chake!

Kila kitu hutegemea fedha. Kutokuwa na fedha husababisha vijana wengi kujiingiza katika wizi na kufanya shughuli haramu hivyo kuhatarisha maisha yao. Msanii Shaaban Robert kwa kumtumia Utubora anataka kuieleza jamii kuwa shughuli za uzalishaji au ujenzi wa jamii kiuchumi, huweza kufanyika kwa namna yoyote halali na popote si lazima iwe mjini.