MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Fasihi ya Kiswahili inavyosisitiza uchumi

Muktasari:

  • Bila shaka umeshawahi kumsikia katika masimulizi au kumsoma katika riwaya maarufu ya ‘Wasifu wa Siti binti Saad iliyoandikwa na mwanafasihi gwiji, Shaaban Robert.

Utafutaji wa kipato maishani umegubikwa na changamoto mbalimbali. Mbalamwezi ya Kiswahili leo hii, inakukumbusha mpenzi msomaji habari za mwimbaji maarufu wa taarabu, Siti binti Saad wa huko Fumba, Unguja, aliyepata kuishi miongo kadhaa iliyopita.

Bila shaka umeshawahi kumsikia katika masimulizi au kumsoma katika riwaya maarufu ya ‘Wasifu wa Siti binti Saad iliyoandikwa na mwanafasihi gwiji, Shaaban Robert.

Lengo letu katika makala haya ni kutaka kukuonesha msomaji jinsi utafutaji katika maisha unavyokabiliwa na vikwazo mbalimbali. Shaaban Robert anatutaka tuwe imara katika harakati za kujikwamua kiuchumi bila ya kutetereka.

Anataka tufanye hivyo kwa kumwiga mhusika Siti ambaye pamoja na kuzongwa na changamoto lukuki, hakukata tamaa bali alisonga mbele kwa nguvu zote na kuibuka na mafanikio makubwa huku waivu wake wakibaki kimya.

Siti binti Saad. Alizaliwa kwa wazazi maskini huko Fumba, Unguja. Baba yake alikuwa mkulima na mama yake mfinyanzi. Siti alijifunza kufinyanga vyungu kwa mama yake. Alibeba vyungu hivyo mpaka mjini Unguja kwa ajili ya kuviuza.

Akiwa huko Unguja, alizunguka katika vichochoro mbalimbali akivinadi vyungu vyake katika kila mlango wa nyumba. Katika kunadi vyungu hivyo, aliwahi kumsikia mtu mmoja akiisifia sauti yake kwamba ilikuwa nzuri yenye mvuto kwa kuimba.

Kwa sababu ya moyo wa kuthubutu, Siti aliondoka Fumba akaenda mjini Unguja kujaribu bahati yake ya maisha. Akiwa huko alikutana na mwalimu Muhsin ambaye alimfundisha kuimba. Baadaye alijiunga na jumuiya ya watribu maarufu sana wa wakati huo. Katikati ya wanaume watano, alikuwa mwanamke pekee.

Alifanya mazoezi ya muziki na kuwa mwimbaji mashuhuri wa kutegemewa. Sauti yake ilikuwa kama kinanda iliyowavutia watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.

Waivu wake hawakufurahia mafanikio yake hata kidogo. Walimpiga vita kwa matusi ili kumkatisha tamaa na kumrudisha nyuma. Walitunga nyimbo wakamwimba:

Siti binti Saad;

Ulikuwa mtu lini?

Ulitoka shamba.

Na kaniki mbili chini,

Kama si sauti;

Ungekula nini? (uk. 22)

Pamoja na kuchoshwa na maneno hayo ya kuvunja moyo, hakukata tamaa. Alionyesha uvumilivu wa ajabu. Alipiga moyo konde na kutazama mbele. Kuhusu kusemwa juu ya sura na umbile lake, alijipa moyo kwa methali hizi, “Asiyeweza kutuumba, hawezi kutuumbua”. Aidha, katika maisha yake aliongozwa na mwongozo huu, “Kusema fedha, kujibu dhahabu”. Kwa mwongozo huu aliweza kupambanua jema na baya. Aliwajibu waivu wake akisema:

Si hoja uzuri

Na sura ya jamali,

Kuwa mtukufu

Na jadi kubeli,

Hasara ya mtu-

Kukosa akili (uk. 29)

Kutokana na kazi yake nzuri iliyokubalika, alisafiri sehemu mbalimbali mathalani Bara Hindi, na Afrika Mashariki yote kutumbuiza. Hivyo, alijipatia pesa nyingi zilizomwezesha kuendesha maisha yake kwa ufanisi mkubwa.

Msanii Shaaban Robert, licha ya kutupatia kisa hiki cha kihistoria cha Siti binti Saad, anatupatia mafunzo kwamba, kazi yoyote halali humpa mtu kipato cha kuyakimu maisha yake. Pili, ili kufanikiwa katika maisha ni lazima kuthubutu kufurukuta kutoka katika hatua moja kwenda nyingine. Aidha, katika utafutaji, changamoto ni jambo la kawaida ambalo kila mtafutaji anapaswa kukabiliana nalo ili kufikia mafanikio. Maneno ya kukatisha tamaa hayana budi kuepukwa kwa busara.