Ferrao: Baada ya mauzo ya hisa, Vodacom itakua zaidi

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao (kulia) akizungumza na mwandishi wa gazeti hili (kushoto), Julius Mnganga, ofisini kwake hivi karibuni. Picha kwa Hisani ya Vodacom. 

Muktasari:

Gharama za mawasiliano

*Ripoti ya Shirikisho la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Duniani (ITU) ya mwaka 2016 inaonyesha Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 ghali zaidi kwa huduma ya mawasiliano Afrika hasa intaneti.

*Inaonyesha inahitaji Dola 246 za Marekani (zaidi ya Sh540,000) kupata megabit moja kwa sekunde nchini wakati Dola saba pekee zinatosha kupata kiasi hicho cha intaneti nchini Ghana.

*ITU inasema wanaoachwa nje ya mtandao ni kutokana na gharama kubwa, miundombinu isiyokidhi mahitaji, kasi ndogo ya kupakua na kutopatikana kwa huduma husika katika lugha mama kwa nchi husika. Umbali kutoka ufukweni unakopita mkongo wa bahari unaelezwa kuwa changamoto nyingine.

*Hata ripoti ya Benki ya Dunia; Digital Dividend 2016 inaeleza nchi zilizo mbali na bahari, wananchi wake wanalipa Dola 232 za Marekani kwa mwezi zaidi kuliko wa ufukweni.

*Nchi za ufukweni, huneemeka kwa mawasiliano kutokana na kunganishwa kwa fiber cables badala ya satelaiti ambayo kasi yake ni ndogo, gharama kubwa na huathirika na hali mbaya ya hewa, mfano mvua kubwa.

*Takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) zinaonyesha uwapo wa watoa huduma tisa wa kimataifa na kitaifa, saba wa kitaifa pekee na watatu wa kikanda.

Kampuni ya Simu ya Vodacom imefunga uuzaji wa hisa zake za awali (IPO) wiki iliyopita na sasa inafanya tathmini kuona mwitikio wa Watanzania ulivyokuwa katika mchakato huo.

Kampuni hiyo inayoongoza kwa idadi ya wateja nchini, iliorodhesha hisa milioni 560 kwa bei ya Sh850 kila moja na ilitarajia kupata mtaji wa Sh476 bilioni. Mwananchi limepata nafasi ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Ian Ferrao. Fuatilia mahojiano hayo:-

Swali: Uuzaji wa hisa zenu ilikuwa ni utekelezaji wa agizo la Serikali. Kama isingekuwa kwa matakwa hayo, mlikuwa na mpango wowote wa kufanya hivyo?

Jibu: Tumekuwa kampuni ya kwanza kutekeleza agizo la Serikali na matakwa ya sheria, tunajisikia fahari kwa hili. Mauzo ya hisa (IPO) yamekwenda vizuri na tulipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau hata Serikali.

Tumejifunza mengi kutokana na mchakato huo, ningeshauri juhudi za kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuwekeza kupitia hisa ziongezwe ili Watanzania wengi zaidi wanufaike. Tulichokiona, wateja wengi walikuwa wanajitokeza dakika za mwisho.

Kukamilisha suala hili kulikuwa na changamoto nyingi. Isingekuwa kwa agizo la Serikali, tungefikiria namna nyingine ya kufanikisha suala hili.

Vodacom ilianza kuuza hisa Machi 9 na kutarajia kuhitimisha Aprili 19, lakini ililazimika kuongeza wiki tatu zaidi zilizomalizika Mei 11.

Swali: Unadhani kwa nini watu hawakuzichangamkia hisa za kampuni yako hata kulazimika kuongeza muda. Zikoje hesabu zenu za fedha?

Jibu: Hakujawahi kuwa na usajili wa kampuni ya mawasiliano nchini, inawezekana hii ni sababu iliyochangia wengi kuchelewa kufanya uamuzi. Hata hivyo, biashara imekwenda vizuri. Nina imani mpaka katikati ya wiki ijayo tathmini ya mauzo hayo itakuwa imekamilika.

Baada ya tathmini, iwapo walioomba kununua hisa hizo watakuwa wachache kama ilivyotarajiwa, basi tutalazimika kupata ushauri kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mtaji na Dhamana (CMSA) ili kujua tunachotakiwa kufanya.

(Ikumbukwe, IPO hii imewahusisha Watanzania pekee, hivyo ikionekana wameshindwa kukidhi mahitaji yaliyotarajiwa na kampuni husika, Serikali inaweza ikaruhusu ama wananchi kutoka wanachama wa EAC au popote duniani kushiriki.)

Kwa mwaka unaoishia Machi, hesabu za fedha za Vodacom zinaonyesha tumepata faida kubwa kuliko makadirio yaliyokuwamo kwenye waraka wa matarajio (prospectus).

Tumepata faida ya Sh47.55 bilioni dhidi ya Sh47.28 bilioni iliyokadiria. Hii ni habari njema kwetu na wanahisa wetu pia. Tumetimiza malengo tuliyojiwekea. Bila shaka, imani ya wanahisa wetu haitayumba kwa mwanzo huu mzuri. Hii imesaidia kukuza pato kwa kila hisa (EPS) kwa asilimia 63.4 sawa na Sh28.3.

Ndani ya miaka mitatu iliyopita tumewekeza Dola 300 milioni za Marekani na Dola bilioni moja kwa muongo mmoja uliopita.

Swali: Baadhi ya wachambuzi wanasema, hapa ilipo, Vodacom imefika mwisho wa ukuaji wake. Unasemaje kuhusu hoja hii?

Jibu: Tanzania ina zaidi ya watu milioni 53 sasa hivi, lakini sisi tuna watumiaji wa intaneti milioni 6.5 na tumewafikia Watanzania asilimia 89, kama theluthi moja tu ya soko zima. Upo uwezekano mkubwa wa Vodacom kukua zaidi kwani maeneo mengi yanahitaji uwekezaji wa ziada.

Kuna watumiaji milioni 1.5 tu wa simu za kisasa. Kutokana na ongezeko la matumizi ya intaneti nchini na duniani. Kwenye nchi zilizoendelea, mtu anakuwa na kati ya laini sita mpaka 10 kwa matumizi tofauti.

Biashara ni nzuri ingawa inakabiliwa na changamoto ya bei kubwa hasa kutokana na kodi ya kuingiza simu za mkononi na bidhaa nyinginezo za mawasiliano. Kodi ni kubwa sana, idadi ya watumiaji wa smartphone (simu za kisasa) ingeongezeka kodi isingekuwapo. Iwapo Serikali italiona hilo na kulifanyia kazi, Vodacom itakua na sekta nzima ya mawasiliano itashamiri.

Mteja anahitaji laini kwa ajili ya simu yake, moderm, mfumo wa ulinzi wa simu au magari, Ipad na vifaa vingine. Huko kote kuna fursa za kuwekeza na kukua. Ukiangalia vizuri, kila huduma yetu ina fursa ya kukua.

Licha ya fursa hizo, zipo nyingine ambazo ni acquisition (kuzinunua) ya kampuni ndogo na kupanua mtandao wa 4G.

Swali: Inasemwa uthamini wa hisa za Vodacom haukuwa halisia, kwamba bei hailingani na thamani ya kampuni. Unalielezeaje hili?

Jibu: Nina mtazamo tofauti na huo. Tumeuza hisa moja kwa Sh850, bei iliyopendekezwa na kampuni iliyotufanyia tathmini. Ni kampuni ya kimataifa ambayo haina maslahi ndani ya Vodacom,  hivyo isingeweza kutoa majibu ya uongo kwani kufanya hivyo ni kujiharibia heshima iliyojijengea kwa muda mrefu.

Hivyo, bei iliyotangazwa ni halisi. Niwatoe wasiwasi wadau juu ya hilo. Taratibu zote zilifuatwa ili kukamilisha hili. Huwezi kukiuka viwango vinavyohitajika unapotaka kuwekeza soko la hisa. Kila mwekezaji anakuwa macho kuangalia unachokifanya.

Swali: Wananchi wanadhani gharama za intaneti na mawasiliano kwa ujumla zipo juu. Unadhani kuna matumaini yoyote ya gharama hizi kushuka?

Jibu: Vodacom imesambaa kwa asilimia 89 nchini. Tunafanya jitihada za kufika maeneo yote kipaumbele kikiwa vijijini. Tumeomba fedha kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCAF) ili kurekebisha vituo vyetu 165. Wakati tunaimarisha miundombinu yetu bei itaendelea kushuka.

Hata hivyo, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye gharama ndogo ya intaneti. Vodacom ina vifurushi vya wateja wakubwa na wadogo. Tuna mhudumia kila mmoja kulingana na uwezo wake.

Kufanikisha kuwaunganisha Watanzania wote kwenye mawasiliano ya uhakika kunahitaji uwekezaji mkubwa. Kwanza ni fedha na miundombinu rafiki. Tupo kwenye mkakati wa kupata spectrum (spectra) yetu itakayoimarisha kasi ya intaneti na mawasiliano kwa ujumla.

Swali: Unauonaje ushindani uliopo sokoni, washindani wengine waliingi na mfumo tofauti, wakianzia vijijini kuja mjini, kulikuwa na athari zozote?

Jibu: Watoa huduma waliopo ni wengi kuwahudumia Watanzania. Ipo haja ya kuipunguza. Kitu muhimu kinachohitajika ni huduma bora siyo wingi wa kampuni sokoni.

Kuingia kwa washindani wetu walioingia kuanzia vijijini kulikuwa na changamoto miaka mitatu iliyopita, lakini hali imeanza kurudi kawaida. Vodacom tumejitahidi kulinda wateja wetu hivyo hatujateteleka.

Tangu waingie sokoni mwaka 2015, wamefikisha zaidi ya wateja milioni 3.5 ikizizidi waliowatangulia wenye wateja milioni moja, wengine wana watumiaji 800,000 na kampuni ya taifa inahudumia watu 166,000; kwa mujibu wa taarifa za TCRA, Desemba 2016.