Figisufigisu zilivyotawala uchaguzi wa wabunge Eala

Muktasari:

Katika uchaguzi wa awali, Aprili 4, mwaka huu walipatikana wajumbe saba, sita kutoka CCM na mmoja kutoka CUF. Wajumbe wawili wa Chadema – Lawrence Masha na Ezekia Wenje kura zao hazikutosha baada ya kuibuka na kura nyingi za hapana kuliko za ndiyo.

Uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) umefanyika kwa mikupuo miwili kinyume na ilivyotarajiwa ili kuwapata wajumbe tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika chombo hicho.

Katika uchaguzi wa awali, Aprili 4, mwaka huu walipatikana wajumbe saba, sita kutoka CCM na mmoja kutoka CUF. Wajumbe wawili wa Chadema – Lawrence Masha na Ezekia Wenje kura zao hazikutosha baada ya kuibuka na kura nyingi za hapana kuliko za ndiyo.

Walioshinda CCM katika awamu ya kwanza ni Fancy Mkuhi, Happiness Lugiko, Maryam Ussi Yahya, Dk Abdullah Makame, Ak Ngawaru Maghembe na Alhaji Adam Kimbisa.

Kwa upande wa CUF aliyeshinda ni Habib Mnyaa, aliyepitishwa na upande wa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba na kuwaacha waliopitishwa na upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad.

Matarajio ya Chadema kuwapisha wagombea hao bila kupingwa, ikiamini ni wenye weledi wa kutosha kuiwakilisha nchi, yalizamia hapo na nafasi hizo kubaki wazi hadi ulipoitishwa uchaguzi wa pili, Mei 10 kupata wawakilishi hao.

Kutokana na hatua hiyo, Chadema iliulalamikia uchaguzi huo wa awali kuwa ulikuwa na upungufu mwingi wa kikanuni ambao ulitia dosari, lakini hawakusikilizwa na matokeo hayo yaliendelea kusimama.

Nyuma ya pazia, wabunge wa CCM ambao kwa wingi wao ndiyo wenye kisu cha kumpitisha yeyote wanayemtaka, walisema Chadema haiwezi kuwalazimisha kupitisha wateule wao na kwamba uteuzi wa chama hicho cha upinzani haukuwa umezingatia takwa la uwiano wa kijinsia.

Uchaguzi wa pili

Katika uchaguzo wa pili, chama hicho kilichopewa nafasi ya kusimamisha wagombea watatu kwa kila nafasi na kwa kuzingatia usawa wa kijinsia, ndipo Kamati Kuu iliketi Zanzibar na kuwateua wagombea sita.

Walioteuliwa na kupitishwa kuwa wagombea ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Profesa Abdallah Safari, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha. Wengine ni mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje na wanachama wengine wawili, Josephine Lemoyan na Pamela Massay.

Baada ya uchaguzi kufanyika, wanawake wawili kati yao, Lemonyan na Massay walichaguliwa kwa kura nyingi, ikionyesha wazi kuwa wamepita kwa mkono wa CCM.

Tatizo halikuwa jinsia

Mara tu baada ya uchaguzi huo ulioonekana dhahiri kukigawa chama hicho, Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene alitoa tamko la chama kuwapongeza washindi hao.

Katika viwanja vya Bunge, baadhi ya wabunge wa Chadema, hasa wanawake waliungana na wenzao wa CCM wakiongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson na Mwenyekiti wa wabunge wanawake, Margaret Sitta kushangilia ushindi, huku baadhi wakijitenga kando, kuonyesha kutowaunga mkono waliochaguliwa.

Awali, viliitishwa vikao viwili vya wabunge; kimoja cha wabunge wa CCM kwa ujumla na kingine cha wabunge wanawake (wa vyama vyote) ambavyo ni dhahiri vililenga kujipanga kwa ajili ya uchaguzi huo.

Lakini Makene, anasema uchaguzi huo wa pili uliendeshwa kihalali na hakukuwa na ukiukaji wa kanuni, bali kilichobaki ni mitazamo ya watu binafsi.

“Kamati Kuu ndiyo ilipitisha wagombea na wabunge wamechagua. Kwa vyovyote jinsi Bunge letu lilivyo CCM ndiyo inayoamua nani achaguliwe, hivyo yeyote kati ya wale angeweza kuchaguliwa,” anasema na kufafanua kuwa kila mmoja alikuwa na timu ya kampeni, hivyo baadhi wangeweza pia kununa baada ya matokeo. 

       Kuhusu suala la jinsia, Makene anasema uchaguzi huu umethibitisha kuwa tatizo la CCM halikuwa jinsia, maana kama ingekuwa hivyo baada ya kuwakataa wanaume wawili wa mwanzo – Masha na Wenje, safari hii wangechagua mwanamume na mwanamke, lakini haikuwa hivyo wakachagua wanawake wawili na kuwaacha wanaume wanne.

Mapema akizungumzia suala la jinsia, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema kwa nafasi mbili walizokuwa nazo huwezi kupata theluthi moja ya wanawake kama kanuni inavyohitaji.

Uchambuzi huru

Akizungumzia uchaguzi huo, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Deus Kibamba anasema uchaguzi huo uliingiliwa na mizengwe mingi tangu mwanzo kutoka katika vyama vyote vilivyohusika.

Kibamba anasema mbali na kinachoonekana kuwa CCM imevuruga uchaguzi wa Chadema, hata chama hicho cha upinzani pia kilivuruga uchaguzi wa CCM.

“Mimi nilikuwapo Dodoma na lazima niseme ukweli, niliwaona wanajipanga kuhakikisha wanawanyima kura wale wagombea maarufu, kina Makongoro Nyerere, mtoto wa Kawawa (Zainab) na mwingine Engineer (mhandisi), kwa hiyo walichofanya CCM ni kurudisha majibu kwa Chadema,” anasema.

Kwa mujibu wa Kibamba, siasa za vyama zinavuruga uchaguzi kwenye vyombo kama hivyo vya uwakilishi, akitolea mfano jinsi wabunge wa CCM walivyowachagua akina John Cheyo na John Shibuda kuwakilisha Tanzania kwenye mabunge ya Afrika na Sadc.

Kutokana na hali hiyo, Kibamba anashauri uwakiklishi kwenye mabunge hayo ya Sadc, Afrika na Eala uruhusu wagombea binafsi ambao hawatapitishwa na vyama vya siasa na pale ambapo vyama vinateua basi visipeleke watu wanaoonyesha kuwapo wateule na wengine wasindikizaji.

“Kama Chadema, ilionyesha wazi kuna wateule na wasindikizaji, hii si sawa, maana upepo wa kisiasa unapobadilika na wanaopitisha ni wengine wanaweza kuchaguwa wale wasindikizaji.

Kibamba pia anashauri vyama vya siasa kuajiri watu wa mikakati ya kisiasa ili kuangalia nini cha kufanya, badala ya kuacha watu wa mikakati ya kisiasa kubaki tu kwenye vyombo vya usalama.

Uelewa na muundo wa uchaguzi

Kuhusu uchaguzi wa Eala, Kibamba anasema uelewa wa wananchi juu ya uchaguzi huo ni mdogo na mfumo wa uchaguzi huo si wa demokrasia kamili.

“Ni kama uchaguzi wa Marekani ambavyo Wamarekani hawakumchagua (Donald) Trump moja kwa moja bali kupitia electrol college, yaani chombo fulani kinawachaguliwa wananchi kiongozi au mwakilishi, hii si demokrasia kamili,” anasema.

Anasema ajabu ni pale ambapo kuna baadhi ya wabunge, watu wanahoji walishindaje ubunge, lakini hao hao leo ndiyo wanajipa madaraka ya kuwachagua wawakilishi wengine wa wananchi.

Anasema katika baadhi ya nchi kama Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, wawakilishi wa nchi katika vyombo kama hivyo wanachaguliwa moja kwa moja na wananchi wakati wa uchaguzi mkuu, hata kama wawakilishi wa awali hawajamaliza muda wao.

Malalamiko ya awali

Awali, Lissu ambaye ni mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, alieleza kuwa uchaguzi wa awali wa kuwapata wawakilishi wa Tanzania, akisema uchaguzi huo ulikuwa ni batili kutokana na kuwapo mapungufu mengi ya kikanuni na kisheria.

Anasema uchaguzi huo haukuzingatia Sheria Bunge la Afrika Mashariki ya mwaka 2011 ambayo inataka uwakilishi kuzingatia uwiano wavyama, tofauti za jinsia na maslahi maalumu.

Moja ya upungufu huo anasema ni msimamizi wa uchaguzi kupokea majina ya wagombe awa CUF ambayo hayakutoka kwa Katibu mkuu Maalim Seif Sharif Hamad.

“Sheria inasema kuwa orodha itakayopelekwa kwa msimamizi wa uchaguzi inatakiwa isainiwe na Katibu Mkuu wa chama na mgombea lakini kwa chama hicho haikufanyika hivyo,” anasema.

Hoja hiyo ilijibiwa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah ambaye ni msimamizi wa uchaguzi huo kuwa yeye alipokea majina hayo kutoka kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Lissu anasema pia orodha ya wagombea iliyokuwa katika karatasi ya kupiga kura upande wa CUF ilikuwa na majina manne badala ya matatu yanayohitajika kisheria na kikanuni.

Ingawa mgombea mmoja kati ya wanne wa CUF, Thomas Malima alijitoa katika uchaguzi huo wakati wa kujieleza ndani ya Bunge akitaka kura zake ziende kwa Habib Mnyaa, Lissu anasema, “Mgombea anayetaka kujitoa anatakiwa kuwasilisha barua ya kujitoa kwa msimamizi wa uchaguzi saa 10 kabla ya siku ya uteuzi.

“Kama aliwasilisha kweli, kwanini hata katika karatasi ya kupigia kura bado kulikuwa na jina lake na kwanini aliingia hadi ukumbini kama alishajiuzulu?”

Pia, Lissu anasema wakati kanuni inaelekeza wapigakura kuweka alama (mark) kwa wagombea tisa kati ya walio katika karatasi ya kupigia kura, kwa upande wagombea wa Chadema, waliandika hapana au ndiyo ili kuwaengu Masha na Wenje.