Flora Chirstandus : Binti aliyebuni kifaa cha kukalia chooni

Flora Chirstandus

Muktasari:

Hiki ndicho kilichomtokea Mkurugenzi wa Anuflo Flora Chirstandus ambaye baada ya kusugua kichwa alikuja na ubunifu wa aina yake nchini.

Unapoambiwa kujiongeza ni kuziangalia fursa zinazokuzunguka. Matatizo au mahitaji yaw engine yanaweza kuwa nafasi yako ya kujikwamua.

Hiki ndicho kilichomtokea Mkurugenzi wa Anuflo Flora Chirstandus ambaye baada ya kusugua kichwa alikuja na ubunifu wa aina yake nchini.

Pengine hii ilitokana na mahitaji ya watu waliomzunguka, kwa maana baada ya ya utafiti wake aligundua uhitaji wa bidhaa hii ya aina ya kipekee.

Msichana huyu ambaye kwa sasa pia ni muhudumu wa ndege akihudumu katika shirika kubwa la ndege nchini Dubai, pia amejiingiza katika biashara kwa kubuni karatasi maalumu za kuweka katika sinki la choo kabla ya kujisaidia.

Flora anasema tangu akiwa mdogo amekuwa akihusudu sana biashara na amekuwa na ndoto ya kuwa na makampuni ambapo kwa sasa amefanikiwa kuanzisha ya utengenezaji wa karatasi za kukalia chooni.

Awali aliwahi kufanya biashara kadhaa ikiwamo ile aliyofanya kama mtu wa kati kwenye uuzaji wa suti, soseji na dagaa.

Mbali na biashara hizo pia Flora anasema kuwa anaukubali sana mradi wa kilimo cha kitaalamu cha Green House na cha uyoga.

Akizungumzia suala la vijana kujiingiza kwenye biashara na umiliki wa kampuni, Flora anasema kuwa wakati umefika kufanya maajabu katika nchi hii.

“Naamini tukikusanya nguvu kila mtu akaja na ubunifu wake ni wazi kuwa Tanzania ya viwanda itazaliwa, kwa kuwa naamini siku zote vijana ndiyo wenye mawazo yenye tija yanayoweza kuibadilisha nchi,” anafafanua.

Flora anasema wakati umefika kwa Watanzania kuiga mfano wa jirani zetu wa Kenya ambao kwa sasa ni kawaida kwa kijana wa miaka 20 kumiliki kampuni ya kibiashara.

“Hivyo kama kwao wameweza ambao fursa ni chache, kwa nini sisi wenye nyingi na kutosha tusisimame katika kuhakikisha kuwa tunafanya utafiti na tunakuwa wabunifu kuangalia soko la bidhaa sio tu kufanya biashara, bali kutoa fursa za ajira kwa vijana wenzetu”anafafanua

Akizungumzia kuhusu namna alivyogundua fursa katika usambazaji wa bidhaa anayozalisha Flora anasema kuwa akiwa nchini nchina alipata wazo hilo kupitia rafiki yake.

Baada ya mizunguko yao ya kawaida wakibadilishaa mawazo wawili hao walijadiliana kuhusu uzalishaji wa bidhaa hizo ndipo alipolazimika kuja kufanya utafiti hapa nchini na kugundua bado kuna uhitaji.

“Kwa kuwa niliona kuna uhitaji, nilijitahidi kuwekeza pesa zangu za mshahara na marupurupu mengine hatimaye nikapata mtaji na leo hii natengeneza na kusambaza bidhaa hizi mpya,” anafafanua.

“Naamini huu ni mwanzo tu, ipo siku nitakuwa na bidhaa nyingi zaidi na zenye ubora wa kimataifa kama ilivyo kwa hizi.”

“Wito wangu kwa wanawake hususani vijana, wajiongeze hakuna njia rahisi katika kufanikiwa, unatakiwa upambane ili kufika pale ulipokusudia,” anamalizia.