Tuesday, November 14, 2017

Fundi ujenzi alivyokatisha ndoto za Secelela

Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanae

Msichana Secelela Juma akiwa amembeba mwanae aliyezaa na mwanaume aliyekuwa na uhusiano nae wakati akisoma sekondari. Picha na Habel Chidawali 

By Habel Chidawali,Mwananchi hchidawali@mwananchi.co.tz

“Sijawahi kuwaza kitu kingine zaidi ya kazi mbili hadi leo, moja ni udereva wa magari makubwa na kazi ya pili ni kuwa muuguzi katika hospitali zenye wagonjwa wengi kutoka vijijini, lakini ndiyo basi tena,”

Ni simulizi ndefu ya msichana Secelela Juma (17) binti ambaye anashuhudia ndoto yake ikiyeyuka kwa sasa, licha ya kujitia moyo kuwa suala la udereva anaweza kupambana hadi alifikie.

Secelela ambaye kwa sasa anaitwa mama John, anaanza kutaja sababu za kupotea kwa ndoto yake ni fundi ujenzi ambaye alikutana naye Julai 2015 wakati akiwahi shuleni. Alikuwa akisoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Ihala ya mjini Mpwapwa.

Anasema umbali wa shule ulimfanya apatiwe msaada wa usafiri wa pikipiki ili kumwahisha na ilifanyika hivyo lakini wakiwa njiani, mtoa msaada alibadil mazungumzo na kuanza kumtaka kimapenzi, huku akiahidi kuendelea kumpa lifti ya kuwahi shule wakati wowote.

“Siku ya kwanza nilipata ukakasi kidogo kumjibu, siku iliyofuata niliamua kumkubalia na siku hiyo hiyo jioni tulianza uhusiano wetu,” anasema.

Msichana huyo ni miongoni mwa wasichana waliotoa ushuhuda kwenye mafunzo ya kujitambua ambayo yaliendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la Utu wa mtoto (CBF) kwa wasichana walioolewa au kuzaa chini ya umri. Alionyesha ujasiri mkubwa wa kuwafundisha wenzake 25 mbinu za kujikinga na wanaume wakware.

Katika simulizi yake anasema hakuwahi kuwaza kujifunza kitu kinachoitwa mapenzi na hakutarajia kufanya katika umri wake, lakini alijikuta akitumbukia kwa sababu ya lifti.

Nini kilitokea

Secelela anasema, alipomaliza masomo ya msingi, alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari Ihala wakati yeye akiishi kwa wazazi wake mtaa wa Igovu mjini Mpwapwa ambako ni mbali na shule aliyopangiwa.

Anasema umbali huo ulikuwa ni changamoto ya kumfanya akutane na vishawishi vingi kutoka kwa wavulana wa mtaani na hata watu wazima. Kila alipokwenda shule au aliporudi nyumbani, hakukosa kukutana na mtu aliyemweleza habari za uhusiano ya kimapenzi.

Kwa maelezo yake, alijitahidi kuwa mvumilivu na mtu mwenye misimamo lakini mwishoni akajikuta ametumbukia kwenye shimo ambalo liliharibu maisha yake kwa jumla.

Anaeleza kukutana na mvulana ambaye alizoea kumuona mtaani hapo, ingawa kwa sasa ana muda mrefu hajamwona zaidi ya kuwasiliana kwenye mitandao. Alianza kama mtu mwema kabla ya kumgeukia na kuwa mpenzi wake kwa muda mrefu.

Aacha shule

Secelela alikwenda shuleni hadi novemba Mwaka 2015 alipofanya mtihani wa taifa wa kidato cha pili na kisha wakafunga shule, huku wakingoja matokea ya kuingia kidato cha tatu.

Hata hivyo, hakuwahi kukanyaga kidato cha tatu kwani walipofungua shule, aliona aibu kwenda kuungana nao kwa kuwa alishakuwa na mimba kubwa.

“Yaani kabla hatujaitwa kwenda kupimwa shuleni, mimi nilikuwa wa kwanza kujiondoa mwenyewe ingawa matokeo nilisikia kuwa nilikuwa nimefaulu na kutakiwa niendelee na kidato cha tatu, ‘’ anasema na kuongeza:

“..nilivyoanza kuhudhuria kliniki nikawa nakutana na wenzangu wengi ambao tulikuwa darasa moja ama walikua na watoto au wana mimba .”

Maisha baada ya kuacha shule

Hali ilikuwa shubiri nyumbani baada ya wazazi wake kuanza kumsimanga kila wakati kuwa amewatia aibu akiwa ni mtoto wao wa mwisho kati ya watoto watano, jambo lililomfanya awaze hata kujidhuru kabla ya kutoroka nyumbani na kwenda kuishi kwa kwa ndugu.

Aliishi nje ya familia yao kwa miezi mitatu lakini mimba ilipofikia miezi 8 aliamua kurudi kwa wazazi wake na kuomba msamaha.

Mwisho wa ndoto yake

Secelela anasema giza nene katika maisha yake lilianzia hapo na kufifisha ndoto yake aliyoanza kuiwaza tangu shule ya msingi kwamba wakati mmoja aje kumiliki leseni ya kuendesha magari makubwa ndani na nje ya nchi.

Licha ya kujipa moyo kuhusu udereva kwamba anaweza kutumia elimu yake ya kidato cha pili na kujifunza, anasikitika kuwa pengine magari atakayoendesha ni ya ndani ya nchi na siyo nje ya nchi.

Kuhusu ndoto ya uuguzi, anasema: ‘’ Ndoto hiyo ni kama imekufa kifo cha aibu kwa kuwa siwezi tena kufikia hatua ya kuwa muuguzi katika zanahati zinazokusanya kinamama wa vijijini ambao nilitamani kuwahudumia. Sasa nawaza kumiliki mgahawa au duka la vyakula ambavyo vinahitaji mtaji.’’

Hatari kwa wasichana wadogo

Selelela anasema kuwa, wasichana kati ya miaka 15 hadi 17 ndiyo kundi linalodanganywa kwa sehemu kubwa na wanaume, kwani bado hawana uwezo mkubwa katika kujibu mashambulizi ya kuepuka vishawishi pale wanapodanganywa.

Sababu nyingine anatajwa ni kuwa wanaume hawaoni tabu kugharimia wasichana wadogo ambao kimsingi hawana mahitaji mengi. Ndiyo maana hata wavulana wadogo nao wamekuwa wakiwarubuni.

“Msichana anatamani chipsi, wakati mwingine kiwi ya viatu tu au nauli au nguo ambavyo wavulana wenye vipato vya chini pia wanaweza kumudu kuvipata,” anaeleza.

-->