Furaha ni msingi imara wa mafanikio yako kiuchumi

Muktasari:

Wapo wanaodiriki kusema fedha ni sabuni ya roho au fedha ni kila kitu maishani. Wanazo sababu nyingi wanaoiamini dhana hii.

Kuna mjadala linapokuja suala la kuamua kipi muhimu kati ya furaha na fedha au mali. Kwa majibu mepesi na ya haraka haraka, wengi husema fedha au mali.

Wapo wanaodiriki kusema fedha ni sabuni ya roho au fedha ni kila kitu maishani. Wanazo sababu nyingi wanaoiamini dhana hii.

Ukiwachunguza ndugu, jamaa na marafiki utagundua wengi hawana furaha bila kujua kiasi cha fedha walichonacho. Nilichojifunza, siyo tu watu wengi hawana furaha, ila hawajui maana sahihi ya furaha.

Jambo la kustaajabisha ni kwamba wapo watu wengi ambao wanadhani furaha siyo kitu muhimu kwenye maisha yao. Wengi niliowadadisi wanasema ili wawe na furaha wanahitaji kuwa na fedha za kutosha kuendesha maisha.

Kitu muhimu ambacho kila mmoja anapaswa kutambua ni furaha ambayo ni chanzo cha mafanikio yote ambayo mwanadamu anaweza kuyapata. Mtu asiye na furaha hawezi kuwa na akili iliyotulia.

Vilevile, hawezi kuwa na amani itakayomwezesha kutanua biashara zake, kukua kazini au kuongeza mtandao kwenye jumuiya inayomzunguka. Kanuni ya mafanikio; furaha inatangulia na vingine vinafuata. Zamani niliwahi kusoma hadithi ya mfalme mmoja mashuhuri ambaye licha ya milki kubwa na mali nyingi alizokuwanazo, hakuwa na raha katika maisha yake. Alijiuliza furaha iko wapi ainunue, lakini hakufanikiwa kupapata mahali ilipokuwa ikiuzwa.

Siku moja mfalme huyo aliwaamuru watu wenye busara wamtafute mtu mwenye furaha katika milki yake ili amuone atakuwa wa namna gani. Walipompata na kumleta mbele yake alistaajabu sana.

Alikuwa mtu wa hali ya chini wala hakuwa na mali. Hata nguo alizovaa zilikuwa zimechakaa mno. Lakini kwa vigezo vyote walihakikisha kuwa pamoja na maisha duni alikuwa mtu mwenye furaha kamili.

Hii ni hadithi yenye somo. Tunajifunza kuwa fedha au mali pekee hazitoshi kumfanya mtu kuwa na furaha ambayo kila mmoja wetu anaihitaji. Hii haijalishi hadhi au madaraka kwani hata mtu mwenye wadhifa mkubwa duniani anahitaji furaha ili kuwa na raha ya maisha. Hivyo, hakuna sababu ya kuishi katika huzuni na mashaka.

Ingawa tunakabiliana na changamoto mbalimbali kila siku ambazo pengine siyo rahisi kuzikwepa, hakuna haja ya kukata tamaa. Bado unaweza kuyafanya maisha yako yawe ya furaha iwapo utaamua kufanya hivyo.

Itafute furaha

Wapo watu ambao wanaweza kuishi na mawazo ya kuachwa na wapenzi wao kwa miaka mingi mfululizo huku wengine wakitumia miezi michache kusahau tukio kama hilo.

Wengine hawawezi kuvumilia kutukanwa, kufokewa, kupata hasara ya biashara, kufeli mitihani au kumpoteza ndugu au mtu wa karibu. Hii inadhihirisha kwamba wachache kati yetu wanafahamu namna ya kupambana na huzuni na kuishinda.

Kwa kuzingatia umuhimu wa furaha na mafanikio maishani nimeona ni vema tukajadili na kuelezana namna ya kuondokana na huzuni hata isiyokwepeka na kuukaribisha ukurasa mpya.

Zipo hatua ukizizingatia zitakusaidia kukabiliana na huzuni na ukaendeleza mambo uyatakayo. Unapojikuta kwenye huzuni, punguza mhemko kwa kushughulikia mfumo wa upumuaji.

Wakati wowote unapopata taarifa mbaya, moyo hushtuka na kuufanya uende mbio hivyo ili kuurudisha katika hali yake ya kawaida unatakiwa kuvuta pumzi ndefu na kuitoa taratibu. Hatua hii itasaidia kutuliza mapigo ya moyo.

Ukifanikiwa kufanya hivyo, jitahidi kutabasamu mara kwa mara, hata kama ni kufanya hivyo kutokana na aina ya tukio au taarifa ulizonazo. Kutabasamu husaidia kuchangamsha akili. Ingawa inaweza kuchukua muda fulani, wataalamu wanasema inasaidia kuamsha hisia za furaha zilizoshambuliwa na huzuni.

Huzuni inapokutokea huyakuta mawazo mengine akilini ambayo huyaondoa. Nafasi hiyo punde huchukuliwa na huzuni. Hali hii ikitokea unashauriwa kujilazimisha kurudisha akilini mawazo ya awali kabla mambo hayajabalika. Lengo likiwa kufufua furaha iliyokuwepo. Ikiwa hutafanikiwa licha ya kufuata hatua hizo zote, wasaidie walio karibu yako kufurahi jambo walilonalo. Kwa mfano, unapokuwa msibani, chukua jukumu la kuwanyamazisha wenzako na kuwapa faraja. Ukifanya hivyo utakuwa umejisaidia kuondokana mawazo yaliyokufanya ulie.

Kosa linalofanywa na wengi wanapokuwa na huzuni hudhani wanatakiwa wahurumiwe. Hawachukui hatua kutafuta nafuu ya hali waliyonayo. Husononeka kwa kutojaliwa hata kama hali halisi haiko hivyo. Wakipatwa na jambo la kuhuzunisha hutaka jamii nzima ifahamu na iwajali na hilo lisipotokea huendelea kuhuzunika.

Baada ya kupoteza furaha kwa muda jambo muhimu ni kuujali mwili wako kwa kula chakula kizuri, kunywa maji ya kutosha na kujitibia kama kuna maumivu ya kichwa au mwili. Jambo la kushangaza, wengi huacha kula hivyo hudhoofu afya zao na kuongeza matatizo zaidi.

Namna nyingine ya kukabiliana na mawazo ya kuumiza ni kupunguza hasira juu ya watu wengine. Kwa kawaida, huzuni husababishwa na watu, kumkasirikia aliyekusaliti au aliyekufilisi ni sawa na kujipa adhabu nyingine mwenyewe. Samehe usonge mbele.