Fursa kwa Watanzania kupitia lugha ya Kifaransa

Muktasari:

  • Mjadala huo sasa umebadilika na kuangazia umuhimu wa Watanzania kutumia lugha nyingi bila kuathiri lugha ya kufundishia.

Suala la lugha ya kufundishia limekuwa likiibua mjadala mpana hapa nchini, baadhi wakitaka iwe Kiswahili kuanzia shule za msingi mpaka elimu ya juu, wengine wakisisitiza Kiingereza kitumike kama ilivyo sasa.

Mjadala huo sasa umebadilika na kuangazia umuhimu wa Watanzania kutumia lugha nyingi bila kuathiri lugha ya kufundishia.

Baadhi ya wanazuoni wanasema kuwa na lugha nyingi ni kufungua fursa kwa wanafunzi; wanapata elimu au ajira nje ya mipaka ya nchi yao. Pia, wanasaikolojia wanasema umahiri wa lugha nyingi unaongeza uwezo wa kufikiri.

Lugha mbalimbali zinafundishwa hapa nchini mathalani Kifaransa, Kikorea, Kichina, Kiarabu na Kijapani. Hata hivyo, mafunzo ya lugha hizi yako chini kwa sababu ya uhaba wa walimu na kukosekana kwa mikakati madhubuti wa mafunzo.

Licha ya kufundishwa kwa lugha hizo, Kiswahili kimesimama kama lugha ya Taifa na lugha ya kufundishia kwa shule za msingi. Hata hivyo, nafasi ya lugha nyingine ipo na tayari Ufaransa kupitia jumuiya ya Francophone imeanza kuhamasisha mafunzo ya Kifaransa kupitia elimu ya juu.

Machi 15, Serikali za Tanzania na Ufaransa zilizindua mkakati wa ushirikiano kwenye elimu ya juu unaolenga kuboresha vyuo vikuu hapa nchini ili kuongeza idadi ya wataalamu kwenye kada mbalimbali sambamba na kuboresha elimu inayotolewa.

Mkakati huo utaenda sambamba na kuweka msukumo kwenye mafunzo ya lugha ya Kifaransa ili wanafunzi wa Tanzania wapate fursa mbalimbali huko Ufaransa na kwingineko duniani ambako lugha hiyo inatumika.

Balozi wa Ufaransa nchini, Frederick Clavier anasema nchi yake iko tayari kuingia kwenye majadiliano na Serikali ya Tanzania ili nchi hii ijiunge na Shirika la Kimataifa la Francophone (OIF).

Clavier anasema lugha ya Kifaransa ina wazungumzaji zaidi ya milioni 300, nusu yao ikiwa ni Waafrika. Pia, amesema nusu ya nchi za Afrika hukutana kwenye Umoja wa Afrika (AU) na OIF.

“Inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2050, idadi ya wazungumzaji wa Kifaransa duniani itafikia watu milioni 750. Hii itaimarisha umoja wa nchi zinazozungumza Kifaransa kama kikundi kikubwa cha ushawishi katika uhusiano wa kimataifa,” anasema Clavier.

Anasema lengo la umoja huo siyo tu kutumia lugha na utamaduni wa Kifaransa, bali pia kuhamasisha demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu miongoni mwa mataifa wanachama.

Balozi huyo anasema Kiswahili kina uwanda mpana wa wazungumzaji milioni 100, kitu alichokiita urithi wa ajabu ambao unapaswa kuungwa mkono. Hata hivyo, anasema biashara na mabadilishano ndani ya Afrika yanahitaji lugha nyingi.

“Mchanganyiko wa lugha ya Kiswahili na za kigeni, pamoja na wa Kifaransa kati yao, kunafungua milango ya ajira nchini Tanzania, Afrika na popote duniani,” anasema Clavier na kusisitiza kwamba Francophone imekuwa na maadili ya amani na uvumilivu.

Kaimu Balozi wa Canada nchini, Susan Steffen anasema licha ya kuwa nchi yake ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola, pia ni mwanachama wa Francophone, na hiyo imewapa fursa ya kuchangamana na nchi mbalimbali duniani.

“Mimi binafsi nilipata nafasi ya kujifunza lugha ya Kifaransa, ikaniwezesha kuchangamana na kujua tamaduni za watu wengine duniani,” anaeleza.

Mtazamo wa Tanzania

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha anazungumzia mkakati huo kwamba utasaidia kuunganisha uchumi na vyuo vikuu na pia sekta binafsi itapata wataalamu wa kutosha.

“Tunatambua kwamba kujua lugha nyingi kunamwongezea mwanafunzi fursa ya elimu na ajira sehemu mbalimbali. Sera yetu ya elimu inaruhusu lugha mbalimbali kufundishwa, na tayari Kifaransa kinafundishwa kwa baadhi ya shule,” anasema Ole Nsha.

Naibu waziri huyo anabainisha kwamba katika majadiliano yao na Wafaransa watajadiliana namna ya kuipa msukumo lugha hiyo ili Watanzania wengi wahamasike kujifunza na kutumia fursa zinazopatikana.

Hata hivyo, Ole Nasha anasema Watanzania wachache wanaopata fursa ya kwenda kusoma Ufaransa, wengi wanakabiliwa na changamoto ya lugha kwa sababu moja ya masharti ya kusoma huko ni kujua lugha hiyo.

“Changamoto hiyo ndiyo inatufanya leo kuweka mikakati ya kuwasaidia wanafunzi wa Tanzania, na moja ya mikakati hiyo ni kutoa mafunzo ya lugha ya Kifaransa hapa nchini. Tutaandaa utaratibu wa namna gani tutalipa msukumo suala hili,” anasema.

Hata hivyo, Clavier anafafanua kwamba siyo lazima kujua Kifaransa ili kwenda kusoma Ufaransa, kwa sababu kuna programu za elimu ya juu zinatolewa kwa lugha ya Kiingereza na watu kutoka nchi mbalimbali wanakimbilia fursa hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu anasema, uhusiano huo ni fursa kwa Tanzania kujifunza kutoka kwa Wafaransa hasa wakati huu Taifa linapolenga kuwa nchi ya viwanda, kwa sababu Wafaransa wameendelea muda mrefu na wana mambo mengi ya kuwafundisha Watanzania hasa kwenye Nyanja za sayansi na teknolojia.

“Tuna imani wahadhiri wetu wakienda Ufaransa watakwenda kujifunza mambo ambayo yatakuwa na tija kwa taifa letu,’’ anasema Dk Nungu.

Watanzania wakianza kutumia Kifaransa wataungana na nchi nyingine za OIF ambazo zina balozi hapa nchini. Nchi hizo ni pamoja na Ubelgiji, Canada, Misri, Ufaransa, Morocco, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Senegal, Shelisheli, Uswisi na Comoro.