Fursa mpya zipatikanazo kwenye soko la mafuta

Muktasari:

  • Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa Mei mwaka jana, inabainisha kuwa zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi kwenye umaskini uliokithiri huku milioni 10 wengine wakiwa juu ya mstari wa umaskini kwa asilimia 10 tu.

Ajira imeendelea kuwa wimbo unaogusa hisia za kundi kubwa la Watanzania waishio mijini na vijijini.Umaskini wa kipato unaongezeka na wahitimu wanalilia kazi.

Ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa Mei mwaka jana, inabainisha kuwa zaidi ya Watanzania milioni 12 wanaishi kwenye umaskini uliokithiri huku milioni 10 wengine wakiwa juu ya mstari wa umaskini kwa asilimia 10 tu.

Aidha, taarifa za Wizara ya Kazi na Ajira kwa mwaka 2014, zinaonyesha kuwa Serikali ina uwezo wa kukidhi mahitaji ya ajira 80,000 hadi 100,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na mzigo wa vijana 400,000 mpaka milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.

Hata hivyo, sekta mpya ya mafuta ya kupikia imeonekana kuwa na fursa lukuki zinazoweza kutengeneza ajira kupitia mlango wa kilimo na biashara.

Fursa hiyo inachagizwa na umuhimu wa lazima kupitia mahitaji ya chakula kwa Watanzania wengi.

Julai 19, mwaka huu kupitia matokeo ya utafiti ulioangalia ‘Sera za kikodi zinazoathiri soko la mafuta nchini,’ yanaweka wazi fursa ya kuzalisha ajira na kupunguza umaskini kama changamoto zilizopo zinaweza kufanyiwa kazi na Serikali kwa kushirikiana na wadau.

Licha ya uzalishaji wa mbegu za mafuta za alizeti, karanga, ufuta, mawese na soya kuongezeka kutoka tani milioni 6.3 za 2015/2016 hadi tani milioni 6.7 kwa mwaka 2016/2017, mazingira ya uzalishaji yamezungukwa na vikwazo mbalimbali.

Mkurugenzi wa Sera, Utafiti na Ushauri wa TPFS, Gili Teri anataja vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na kuendeshwa na wananchi wasiokuwa na elimu ya kutosha ya kilimo cha kisasa.

Kikwazo kingine ni gharama kubwa zinazotumika wakati wa uzalishaji.

Hatua inayosababisha kukosa ushindani na soko la mafuta yanayoingia nchini kwa bei ndogo. Nyingine ni kushuka kwa bei ya soko la dunia, ambayo huathiri bei ya soko la ndani hatua inayosababisha uagizaji wa nje unaongezeka na kuua soko la ndani.

“Kwa hiyo tuwasaidie wakulima waingie kwenye kilimo cha kisasa ili watumie gharama ndogo.Itaongeza ushindani katika soko la mafuta ynayotoka Malyasia na Indonesia, kwa sasa hekari moja inazalisha pungufu ya(mara sita) kilichotarajiwa, kwa hiyo uuzaji wake inakuwa gharama,”anasema Teri.

Mkurugenzi Msaidizi Uhamasishaji na Uendelezaji wa Viwanda, kutoka wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Juma Mwambopa anakili changamoto zilizobainishwa katika utafiti huo huku akitoa mapendekezo ya serikali katika makundi yanayohusika katika sekta hiyo.

Anasema sera zilizopo ni vigumu kuondoa kodi kwa waagizaji wa mafuta au mafuta ghafi kutoka nje kwani serikali inahamasisha uwekezaji wa ndani utakaosaidia ujenzi wa viwanda, kuongeza ajira kupitia uongezaji wa thamani ya bidhaa.

“Kwa sasa anayeagiza mafuta ghafi halipi kodi, anayeingiza mafuta yaliyokamuliwa ambayo hajawa bidhaa analipa asilimia 10 na anayeingiza bidhaa ya mafuta ni asilimia 25, hizi hatuwezi kuziondoa licha ya malalamiko ya uhitaji wa soko la ndani,”anasema.

Pili, Mwambopa anasema malalamiko ya uhaba wa mbengu za kukamua, kundi la wazalishaji viwandani linatakiwa kuzungumza na halmashauri ili wapatiwe ardhi ya kuanza kulima ili kutosheleza mahiaji yao. Aliwashauri pia kuongeza nguvu katika uingiaji wa mikataba na wakulima ili waweze kuwa na uhakika wa masoko kwao.

“Kuhusu malalamiko ya wakulima katika udhaifu wa mbengu kwamba zinatoa mafuta kidogo, ni suala linalohitaji sasa wadau kuanzia wataalam wizara ya kilimo, watafiti, kufanya utafiti ili kujua ni mbengu gani zinazoweza kutoa mafuta mengi,”anasema Mwambopa.

Matokeo ya utafiti

Utafiti huo uliofanyika Machi hadi Juni mwaka huu, ulihusisha maeneo yanayohusika na uzalishaji na ukamuaji wa mafuta ambayo ni Singida, Dodoma, Manyara,Morogoro ,Dar es Salaam na Mwanza.

Aidha, utafiti huo ulijikita kuangalia mazingira ya utekelezaji wa sera zilizopo katika sekta hiyo endapo zinawasaidia wazalishaji wa ndani au zinawakandamiza. Miongoni mwa kodi ni pamoja na tozo ya serikali ya asilimia 10 kwa wafanyabiashara wanaoingiza mafuta kutoka nje.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, mwandaaji wa utafiti huo, Braison Salisali anasema utafiti umebaini kuwapo kwa fursa kubwa ya masoko ya ndani na nje. Kwa mujibu wa utafiti huo, ifikapo mwaka 2030 mahitaji ya mafuta yatafikia tani 700,000 kwa mwaka katika soko la watanzania milioni 82 kwa wakati huo.

Pia, utafiti unaonyesha kwa sasa Viwanda vikubwa vinatumia asilimia 25 tu ya uwezo wake kukamua mafuta yatokanayo na uzalishaji wa ndani huku asilimia 75 ikikosekana na kusababisha viwanda hivyo kutotumika.

“Utafiti unaonyesha Tanzania ni nchi ya Pili Afrika inayochangia asilimia 35 ya mbengu za mafuta yote ya Alizeti yanayozalishwa Afrika. Sababu ni mahitaji makubwa kwa watu wenye uwezo huko nje ikilinganishwa ndani,”anasema Salisali.

Pamoja na uwezo wa viwanda uliopo, utafiti huo unaonyesha kuna wazalishaji milioni 1.6 wa mbengu hizo wanaoweza kulisha soko la viwanda na matumizi ya nyumbani, lakini wakulima hukutana na changamoto za uzalishaji wa gharama kubwa.

Fursa za soko

Katika fursa za soko Afrika Mashariki na nchi nyingine za SADC, Tanzania kupitia uzalishaji wa mafuta unawezesha kutumia fursa za masoko ya Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, DRC Congo, Malawi, Angola, Zimbabwe, Msumbiji na Sudani.

Lakini kwa mujibu wa takwimu za wizara ya viwanda na Biashara, Tanzania inazalisha mafuta ya Alzeti, Ufuta na Mawese katika kiwango cha tani 180,000 tu kati ya 500,000 ya mahitaji hatua inayosababisha kuingiza wastani wa tani 400,000 kutoka nje.

Teri anasema fursa hizo zitapatikana tu endapo mazingira yataboreshwa na uzalishaji ukaongezewa tija. Anasema hatua hiyo itasaidia kuondoa umaskini kwa watanzania milioni 13 watakaoweza kuguswa na sekta hiyo.

“Kwa sasa kuna watanzania milioni tatu walioko katika fursa za sekta hiyo ambao wanalisha soko la ndani kwa sehemu ndogo(180,000) ya mahitaji, bado mahitaji ni tani 400,000 kwa mwaka,”anasema Teri.

“Tukiondoa vikwazo tutaokoa fedha za kigeni na viwanda vitaongeza ukamuaji kwa asilimia mia moja.ni sekta inayotumia fedha nyingi za kigeni kuagiza mafuta kutoka nje.Mwaka 2013 ilitumia dola 167millioni na mwaka 2016 ikatumia wastani wa dola 294 millioni, hizi fedha zinaweza kubakia ndani tukiamua.”